BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SAIDI BAHANUZI AIPELEKA BARCELONA FC HATUA YA 16 BORA MWINTANGA CUP 2017


Saidi Bahanuzi.


Juma Mtanda, Morogoro.
Klabu ya Barcelona FC imetinga hatua ya 16 bora ya mashindano ya Mwintanga Cup 2017 baada ya mshambuliaji wao tegemeo, Saidi Bahanuzi kufunga bao pekee katika mchezo dhidi ya Chamwino Youth SC katika michezo inayoendelea ya hatua ya pili ya mashindano hayo katika uwanja wa Sabasaba Manispaa ya Morogoro.

Saidi Bahanuzi ambaye ni mshambuliaji wa klabu ya Mtibwa Sugar alifunga bao hilo dakika ya 14 wakati akiichezea timu yake ya mtaani ya Barcelona FC ya Bigwa mjini hapa na kusonga mbele ya michuano hiyo.

Akizungumza na MTANDA BLOG mjini hapa, Katibu mkuu wa chama cha soka Manispaa ya Morogoro (MMFA), Kafale Maharagande alisema kuwa mashindano hayo ya Mwintanga Cup 2017 yalishirikisha jumla ya 58 na timu 30 zilipenya hadi hatua ya pili baada ya kumalizika michezo ya hatua ya kwanza.

Kafale alisema kuwa michuano hiyo ina lengo la kuwakumbuka na kuwarehemu wanamichezo waliofariki dunia na kutoa mchango mkubwa katika tasnia ya soka la Tanzania huku lengo la pili likiwa kutoa burudani katika kipindi hiki ambacho hakuna michezo ya ligi kuu wala ligi daraja la kwanza.

“Chama cha soka Manispaa ya Morogoro (MMFA) kimeandaa jukumu la kuanzisha mashindano ya Mwintanga Cup 2017 kama kutoa fursa kwa makocha wa klabu zetu kutazama wachezaji wenye vipaji kwani michuano kama hii ndiyo inayoibua nyota wa baadaye”.alisema Maharagande.

Timu nyingine zilizofuzu kuingia hatua ya 16 bora kuwa ni pamoja na Ball Talent FC iliyoitandika Miembe Mitatu FC bao 2-1, Moro Kids ikaisambaratisha G.Seven kwa bao 1-0 huku Home Boys FC ikiambulia kipigo cha bao 2-1 kutoka kwa Young Star FC.

Don Bosco FC iliibuka na ushindi wa bao 5-4 iliyoipata kwa changamoto ya mikwaju ya penalti mbele ya Chicago FC baada ya sare ya bao 1-1.

Nyingine ni Masubo United iliyoishikisha adabu Jamaica FC kwa kuitandika bao 1-0 kwa bao la, George Chota aliyekwamisha mpira kimiani dakika ya 43 kwa mkwaju wa penalti wakati Stend Hiace Mjini nayo ilisonga kwa mikwaju ya penalti ya bao 7-6 dhidi ya Mawingu United baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 kumalizika.

Maharagande alisema kuwa michezo ya 16 bora inatarajia kuanza kuendelea kutimua vumbi Julai Mosi baada ya kumalizika kwa mzunguko wa hatua ya pili Juni 28 mwaka huu.
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment