CHADEMA KUANDAA MAANDAMANO KUMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA MGONGO WA WABUNGE WA UPINZANI
BARAZA la Vijana wa Chadema Taifa (Bavicha), limesema litaitisha maandamano ya amani kuwapongeza wabunge wa vyama vya upinzani kwa kuibua mijadala yenye maslahi kwa taifa ikiwamo suala la ulinzi wa rasilimali za taifa ambalo Rais John Magufuli amelishikia bango na kutekeleza kwa vitendo.
Kusudio hilo lilitangazwa juzi na Katibu Mwenezi wa Bavicha Taifa, Edward Simbeyi, wakati akizungumza na wahitimu pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu sita vya mkoa wa Kilimanjaro ambao ni wanachama wa Chadema (Chaso).
“Tutaitisha maandamano ya amani kuwapongeza wabunge wa upinzani kwa kuibua mijadala yenye afya kwa taifa na hasa ulinzi wa rasilimali za taifa kama vile suala la mchanga wa dhahabu (makinikia) ambalo Rais Magufuli amelifanyia kazi,”alisema.
Mahafali hayo ni mjumuiko wa wanafunzi wa vyuo vikuu sita ambavyo ni Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (Mwecau), Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba na Uuguzi cha KCMC, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Kumbukumu ya Mtakatifu Stefano Moshi, kampasi ya Mwika (SMMUCo) na Chuo cha Usimamizi wa Uhifadhi wa Wanyama Pori-Mweka.
Aidha, alipoulizwa yatafanyika lini kwa kuwa mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano vimepigwa marufuku, Simbeyi alisema wanatarajia kufanya maandamano hayo mwezi huu, ingawa hakuwa tayari kutaja tarehe wala siku.
Alipotafutwa kutoa tamko la Jeshi la Polisi kuhusu kusudio hilo la Bavicha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi, Hamisi Issah, aliwaonya vijana hao kutothubutu kufanya maandamano hayo.
ACP Issah alisema: “Tena, waambie wasithubutu, nawaonya wasifanye maandamano maana hata wale waliojitokeza kutaka kumpongeza Rais (Magufuli) hawakuweza kufanya. Kimsingi yamepigwa marufuku na wasijaribu kutokea barabarani.”
Akiwa katika mahafali hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema taifa (Zanzibar), Salum Mwalimu, aliuagiza uongozi wa Bavicha kuitisha kongamano la kitaifa la wanachama wa Chadema wanaosoma vyuo vikuu vyote nchini kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa na mustakabali wa kisiasa.
“Kuna haja ya kuitisha kongamano la kitaifa la Chaso, Simbeyi kaeni na wenzako kwenye baraza la muitishe kongamano hilo kabla ya mwaka huu kumalizika,” alisema Mwalimu.
Awali, akisoma risala ya wanachama hao wa vyuo vikuu vya Kilimanjaro, Mahonia Joseph kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, alisema Chaso inapendekeza Katiba ya Chadema itamke rasmi uwepo wa Chaso na kutoa kibali kwake cha kuwa na mfuko wake maalumu kwa ajili ya kujiendesha. Pia, waliishauri Chadema kupitia mabadiliko yake ya kikatiba kione umuhimu wa Chaso kuwa na uwakilishi wake ngazi ya taifa.Nipashe
0 comments:
Post a Comment