BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HUYU NDIYE MWANAFUNZI ALIYEWEKA AHADI YA KUFANYA VIZURI MTIHANI WA KIDATO CHA SITA ILI TU ASHIKANE MKONO NA RAIS MAGUFULI

MWANAFUNZI bora wa kike, Sophia Richard Juma (18) aliyeongoza ufaulu wa masomo ya sayansi katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita mwaka huu.

amesema amepania kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na kwamba kiu yake kubwa ni kuonana na Rais John Magufuli ili amshike mkono kwa nia ya kumpongeza.

Aidha, kinara wa masomo ya mchepuo wa Lugha na Sanaa, ambaye ni wa EGM (Uchumi, Jiografia na Hisabati), Francis Samkyi wa Shule ya Feza Boys ya jijini Dar es Salaam, alisema amefurahi kutimiza lengo la mtihani huo na kwamba sasa nia yake ni kutimiza ndoto yake ya kuwa mtaalamu wa masuala ya fedha.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana mjini Zanzibar na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Musonde, Sophia alikuwa kinara wa masomo ya sayansi, akifuatiwa na Agatha Ninga wa Tabora Girls ya Tabora na Nathaniel Ndagiwe wa Mzumbe ya Morogoro.

Samkyi aliibuka kidedea katika masomo ya lugha na sanaa, akifuatiwa na Jophary Ernest na Andrea Nkondo, wote wa Ilboru ya Arusha.

Katika orodha hiyo ya wanafunzi waliong’ara kwa kila mchepuo, Rajabu Ali Mabaranga wa shile ya Kibaha mkoani Pwani aliongoza katika msomo ya biashara, akifuatiwa na Gasto Theobalo Kimaro wa Umbwe ya Kilimanjaro na Rashid Abdallah wa Tusiime ya jijini Dar es Salaam.

SOPHIA ALIVYOMTAJA JPM
Sophia amehitimu shule ya sekondari St. Mary’s Mazinde Juu iliyopo Lushoto mkoani Tanga, akisomea mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Bailojia).

Pia ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne wa familia ya Richard Tadeo na Joyce Ezra, wakazi wa Pasiansi wilayani Ilemela, mkoa wa Mwanza ambao shughuli zao kuu ni uvuvi. 


Kabla ya kwenda kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kambi ya Msange mkoani Tabora, ambako kwa sasa ndipo alipo, Sophia aliwaahidi wazazi wake, kwamba mwaka huu atatenda maajabu yatakayompa fursa ya kushikana mkono na rais Magufuli.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, mama wa Sophia, Joyce Ezra, alisema licha ya kumsomesha mtoto wao kwa shida ikiwamo kukopa fedha kila mara ili wamlipie ada, matokeo hayo yaliyotangazwa na NECTA na mwanawe (Sophia) kuongoza kitaifa katika masomo ya sayansi, wanaona wazi kwamba amewatendea haki na pia kutimiza kile alichowaahidi.

“Kila tulipokuwa tunaenda kukopa fedha, tulimuonyesha na kumwambia tumekopa fedha, tusije tukafungwa bure… jitahidi maana tulijinyima na hata wakati mwingine kulala njaa ili mtoto wetu asome,” alisema Joyce.

“Mara kwa mara amekuwa akituambia kwamba anataka kuwa daktari bingwa wa moyo ili aweze kutibu watu. Lakini kikubwa zaidi ni kwamba mwaka huu alijitabiria kuwa mwanafunzi bora na kwamba naamini kwa kufanya hivyo atapata fursa ya kuonana na kupeana mkono na Rais John Magufuli,” alisema mama huyo wa Sophia jana.

Kwa kawaida, wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya taifa hupata nafasi ya kwenda bungeni na kupongezwa huku pia wakitunukiwa zawadi mbalimbali.

Akimuelezea Sophia, mama huyo alisema kuwa alisoma katika Shule ya Msingi Mwenge iliyopo Mwanza, kisha kusoma sekondari shule ya wasichana Visitation iliyopo Moshi mkoa wa Kilimanjaro.

Baba wa Sophia, Richard, alisema kumsomesha mtoto wa kike kuna manufaa makubwa na siri nyingine ni kwamba, ni rahisi kwao kutimiza malengo wanaposimamiwa kwa karibu kwa sababu mara nyingi huwa wasikivu.

“Wazazi wawekeze katika elimu, hasa kwa mtoto wa kike. Sikubaliani na usemi wa baadhi ya watu wanaosema kuwa kusomesha mtoto wa kike ni hasara.

Mtoto wa kike ni msaada na huwezi kupoteza. “Tena ni wasikivu sana. Kwakweli tunamshukuru Mungu mwanetu kupata matokeo mazuri kwa kiwango tusichotarajia,” alisema Richard, ambaye aliongeza kuwa amekuwa akijihusisha na uvuvi kwa zaidi ya miaka 20.

Alisema hivi sasa wanamsubiri kwa hamu Sophia ili wampokee kwa furaha wakati atakaporejea nyumbani akitokea kwenye mafunzo ya JKT, Agosti 8 mwaka huu.

ALICHOSEMA SAMKYI
Akizungumza na Nipashe jana, Samkyi alisema ndoto zake siku zote ni kuwa mtaalamu aliyebobea wa masuala ya fedha. Kwa sababu hiyo, Samkyi alisema kuwa alitenga muda wake mwingi kila siku akiwa likizo nyumbani au shuleni akijisomea na pia alimtanguliza Mungu kwa maombi ili amuongoze katika kile anachokipigania.

“Sikutarajia kushika nafasi hii kitaifa, kwa kuwa katika darasani tulikuwa wanafunzi 35 na wote hao kwakweli wako vizuri sana.

Hivyo ushindani ulikuwa mkubwa , haikuwa kazi rahisi,” alisema Samkyi. Baba na mama wa Samkyi, Thomas na Victoria, walisema kuwa walitarajia mtoto wao kufanya vizuri kwa kuwa siku zote, tangu akiwa shule ya msingi alikuwa akishika nafasi ya kwanza.

“Lakini haijawahi kutokea katika familia mtoto kuongoza kitaifa, labda kimkoa… tunamshukuru Mungu kwa matokeo haya,” alisema baba wa Samkyi, akiungwa mkono na mkewe.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Feza, Simon Albert, alisema shule yao imempatia Samkyi ufadhili wa masomo ya Chuo Kikuu nje ya nchi na zawadi ya iPad. 


“Kwa kawaida wanafunzi 10 bora hupewa scholarship (ufadhili wa masomo) pamoja na kompyuta. Lakini zaidi wanakuwa wanatamani kwenda bungeni.. wanajua wakishinda, wataitwa bungeni,” alisema Mwalimu Albert.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: