BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAUJI YA KIBITI SIO YA KUCHEZEA, CCM YAZIDI KUCHELESHA KUFANYA UCHAGUZI NGAZI YA SHINA HADI WILAYA.


Mauaji yanaoendelea katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji yamesababisha CCM kuchelewesha uchaguzi wake katika ngazi za shina hadi wilaya.

Hayo yalielezwa jana na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole alipokuwa akijibu swali la Mwananchi kuhusu maendeleo ya chaguzi za ndani na hali ya kusuasua katika baadhi ya maeneo.

“Tumechelewesha kidogo kutokana na mauaji yanayoendelea kujitokeza na mauaji hayo yamekuwa yakijitokeza kwa viongozi wa chama chetu. Tulilalamika kwa Serikali na wanaendelea kushughulikia changamoto hiyo,” alisema.

Alisema maandalizi ya kuhamasisha wanachama kushiriki katika uchaguzi huo yameshaanza.

Kabla ya hatua hiyo, CCM na makundi mengine katika jamii wamenukuliwa na vyombo vya habari yakilaani mauaji hayo yanayohusisha viongozi, hasa wa chama hicho, huku Serikali ikiwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kuwashughulikia wauaji hao.

Mauaji yanayoendelea katika wilaya hizo tangu Mei mwaka jana yamesababisha vifo vya watu 38, wakiwamo viongozi wa vijiji na vitongoji na askari wa Jeshi la Polisi.

Akizungumzia uchaguzi huo katika maeneo mengine, Polepole alisema hatua za awali zimeshakamilika.

“Kwa uchaguzi wa mashina ulishakamilika kwa asilimia 98 kote nchini. Hata rufaa mwisho ilikuwa Juni 15. Kwa upande wa matawi umekamilika kwa asilimia 85 hadi 90 kote nchini ila zipo kesi chache tu katika baadhi ya maeneo.” alisema Polepole.

“Uchaguzi wa ngazi ya Kata ndiyo uchukuaji fomu umeanza kwa sasa pamoja na jumuiya. Huyo anayesema uchaguzi umedorora hatoki CCM. Mwamko ulikuwa ni mkubwa sana ila kwenye changamoto ilikuwa ni maeneo ya huko Rufiji, Mkuranga na Kibiti.”

Uchaguzi huo unafanyika kwa kuhusisha nafasi ya mwenyekiti na wajumbe wanne wa shina, mwenyekiti, katibu, katibu mwenezi na wajumbe wa kamati ya siasa (Tawi), mwenyekiti, katibu, katibu mwenezi na wajumbe wa kamati ya siasa (Kata) na Halmashauri kuu ya Kata.

Pia, katika ngazi ya wilaya, uchaguzi huo unahusisha nafasi ya mwenyekiti, katibu, katibu mwenezi, wajumbe wa kamati ya siasa, kikao cha halmashauri na wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya.

Hata hivyo, katika hatua za uchukuaji wa fomu ngazi ya matawi na mashina, baadhi ya madiwani na wanachama walisema mwitikio mdogo wa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama, umetokana sababu kadhaa, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya uendeshaji wa chama na madai ya posho za uchaguzi wa mwaka 2015.

UWT yatangaza uchaguzi wao
Katika hatua nyingine, katibu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Amina Makilagi amewataka wanachama kuanza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ngazi ya kata hadi Taifa. 


“Tumetoa matangazo ya kuchukua fomu kuanzia Julai 2 (leo) hadi 10 na wasitangaze nia, uchaguzi utafuata taratibu zote kwa mujibu wa kanuni na katiba ya chama. Tunataka wachague viongozi waaminifu, wachapakazi, wanaochukia rushwa, ubadhilifu, wapole ila wakali kwa mambo ya hovyo, wanyenyekevu na wanaoheshimu watu,” alisema.Mwananchi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: