BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MFANYABIASHARA YUSUPH MANJI ASOMEWA MASHTAKA AKIWA WODINI HOSPITALI YA MUHIMBILI KWA TUHUMA ZA UHUJUMU UCHUMI


Mfanyabiashara Yusuph Manji

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana ilihamishia shughuli zake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,-

katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kuwasomea mashtaka ya uhujumu uchumi mfanyabiashara Yusufali Maji (41) na wenzake watatu, ikiwamo kukutwa na vitambaa vya sare za Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Kosa la uhujumu uchumi halidha dhamana kisheria mpaka kwa ruhusa ya Mahakama Kuu na hata hivyo, upande wa Jamhuri uliwasilisha hati ya kuzuia dhamana kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akiomba washtakiwa wasipewe dhamana kwa usalama wao na maslahi ya taifa.

Pia DPP alieleza sababu nyingine kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kushughulikia dhamana dhidi ya kesi hiyo.

Manji na wenzake wanatuhumiwa kukutwa na mihuri ya mbalimbali ya JWTZ isilivyo halali, vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 236.5.

Saa 9:10 alasiri mahakama hiyo ilifika viunga vya taasisi hiyo na moja moja ilielekea wadi namba 1 alikolazwa Manji.

Washtakiwa wenzake wakifikishwa na gari ya polisi aina ya Landcruiser yenye namba za usajili T968 DHS na kuungana na mfanyabiashara hiyo katika wodi hiyo.

Mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, ilianza kusikiliza mashtaka ya Jamhuri saa 9:35 katika wodi hiyo.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga, Mutalemwa Kishenyi na Tulumanywa Majigo.
Upande wa utetezi uliongozwa na Wakili Hudson Ndusyepo, Emmanuel Safari na Seni Malimi.

Majigo aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Ofisa Rasilimaliwatu Deogratias Kisinda (28), Mtunza Stoo, Abdallah Sangey (46) na Mtunza Stoo msaidizi, Thobias Fwele (43).

Katuga alidai katika shtaka la kwanza kuwa Juni 30, mwaka huu eneo la Chang'ombe Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Manji na wenzake walikutwa na askari polisi wakiwa na mabunda (majora) 35 ya vitambaa vinavyotengezea sare za JWTZ vyenye thamani ya Sh. milioni 192.5 na kwamba vilipatikana isivyo halali.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A' Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabando nane ya sare za JWTZ zenye thamani ya Sh. milioni 44.

Upande huo wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa, Juni 30, mwaka huu eneo la tukio la kwanza, washtakiwa walikutwa na mhuri wa JWTZ uliokuwa na maandishi 'Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha Jeshi JWTZ' bila kuwa na uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.

Majigo aliendela kudai katika shtaka la nne, siku ya tukio la tatu, washtakiwa wote kwa pamoja walikuwa na mhuri wenye maandishi "Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma" bila uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.

Katika shtaka la tano, ilidaiwa siku ya tukio la tatu na la nne, mshtakiwa alikutwa na mhuri wenye maandishi "Comanding Officer 835 KJ Mgambo P.O BOX 224 Korogwe" bila kuwa na uhalali kitendo ambacho kinahatarisha uslama wa nchi.

Ilidaiwa katika shtaka la sita, Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A', washtakiwa wote walikutwa na namba za gari zenye usajili wa SU 383 iliyopatikana isivyo halali.

Majigo alidai katika shtaka la saba, eneo la tukio la sita, washtakiwa walikutwa na namba za gari zenye namba ya usajili SM 8573 iliyopatikana isivyo halali.

Kwa mujibu wa mashtaka hayo yaliyofunguliwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Usalama wa Taifa, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao.

Hata hivyo, upande wa utetezi ulidai kuwa upande wa Jamhuri una nia mbaya kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi ya washtakiwa kuwasilisha hati hiyo ni kuwanyima haki.

Hakimu Shaidi alisema upande wa utetezi wawasilishe hoja zao Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kusikiliza kesi yao na kwamba hawezi kutoa amri yoyote chini ya mahakama yake.

Alisema kesi hiyo itatajwa Julai 19 na washtakiwa watatu walipelekwa mahabusu ya Keko huku Manji akiwa chini ya ulinzi wa polisi wodini hapo, wakati akisubiri askari magereza kupokea hati yake ya kuwa mahabusu.

Mahakama hiyo ilimaliza shughuli zake saa 10.35 alasiri na wakati wote Manji alikuwa amelala kitandani huku washtakiwa wenzake wakiwa wamesimama wakati mashtaka yanasomwa. Manji pia anakabiliwa na kesi nyingine ya matumizi ya madawa ya kulevya katika mahakama hiyo.Nipashe
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment