BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS MAGUFULI AFICHUA MAZITO JUU YA USALITI WA VIGOGO NDANI YA SERIKALI


JPM afichua mazito usaliti wa viongozi

RAIS John Magufuli amefichua mambo mazito kuhusiana na uamuzi wa baadhi ya viongozi uliosababisha hasara kubwa kwa taifa, ikiwamo kuingia mikataba ya ovyo. Mikataba hiyo ilisababisha wizi wa rasilimali za nchi bila kuwanufaisha Watanzania.

RAIS John Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli aliyeonekana akizungumza kwa uchungu wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza jana kushuhudia uzinduzi wa mradi mkubwa wa maji wa Sh. bilioni 22 katika sehemu ya ziara yake ya siku mbili Sengerema mkoani Mwanza.


Alifichua mfano mmojawapo wa usaliti wa baadhi ya viongozi kwa taifa kuwa ni kuwapo kwa mmojawapo aliyekuwa tayari ‘kuiuza’ nchi kwa kupewa gari dogo la kubebea mizigo aina ya ‘pick-up’.

Mradi huo wa maji umetekelezwa chini ya mpango wa maji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi bilioni 22.4. 


Mradi wa Maji Safi mjini Sengerema ulioanza tangu mwaka 2011 unatarajiwa kuwahudumia wakazi 138,000 ifikapo mwaka 2030.

Rais Magufuli alisema kwa sababu ya kuwapo na baadhi ya mambo ya ovyo na ya kutisha, ameamua kujitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania na kusisitiza kauli yake ya kila mara ya kutaka aendelee kuombewa kutokana na ukweli kuwa ‘mambo ya ovyo’ ni mengi kiasi kwamba kila anapogusa hukuta ni mahala penye ulaji wa watu.

Hata hivyo, Rais Magufuli aliwatoa hofu Watanzania juu ya vita inayoendelea dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi, akisema aliomba kuchaguliwa kushika nafasi hiyo kwa sababu anawafahamu wala rushwa na alifanya kazi serikalini kwa miaka 20, hivyo anafahamu kila kitu.

Rais Magufuli aliyekuwa akishangiliwa kila mara na wananchi waliojitokeza kwenye tukio hilo, alitaja baadhi ya maeneo ambayo taifa lilikuwa likipoteza fedha nyingi kuwa ni pamoja na mikataba ya ovyo ikiwamo ya madini iliyotoa mwanya wa wachache kunufaika huku nchi ikiibiwa; ubinafsishaji uliosababisha viwanda 197 kuangukia mikononi mwa watu walioishia kuvitelekeza.


Kuwapo kwa watumishi hewa ambao mwishowe waliigharimu serikali mabilioni ya fedha kutokana na mishahara hewa; kuwapo kwa wanafunzi hewa zaidi ya 65,000; kaya maskini hewa zaidi ya 56,000; vyeti hewa zaidi ya 10,000.

Upigaji kwenye miradi ya maendeleo kama ya kuboresha reli ya kati na pia ruzuku pembejeo za kilimo iliyohujumiwa na wachache kwa kuwapo idadi kubwa ya wakulima hewa nchini kote, wakiwamo walioandikwa kwenye vitabu kama wamepewa pembejeo za kilimo ilhali walishafariki miaka mingi.

“Ni mambo ya ajabu yalifanyika katika nchi. Tunalipa mabilioni ya ajabu. Mtu alikuwa yuko radhi auze maisha ya Watanzania kwa pick-up… anaachia vitu vyote. Tumefanya mikataba ya ovyo,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Tanzania tumebinafsisha viwanda vyetu, tukavigawa, sitaki kuwalaumu waliofanya hivyo… lakini sizuiwi kuzungumza ukweli, ndiyo maana kuna viwanda 197 havifanyi kazi, tangu tumewagawia havifanyi kazi.”

Rais Magufuli alitoa mfano wa mkoa wa Morogoro ambako kuna kiwanda kinafugia mbuzi na kiwanda cha kutengeneza ngozi Mwanza kilipewa kwa mtu ambaye amekaa nacho bila kukitumia.

Alisema kiwanda hicho kilikuwa kikitumika kutengeneza ngozi ambazo zilikuwa zikiuzwa nje ya nchi hadi Ulaya, ikizingatiwa kuwa Tanzania ni nchi ya pili au ya tatu katika Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, lakini sasa hakifanyi kazi tena.

“Kiwanda hakipo. Mtu amepewa amekaa nacho kama si uuaji ni nini. Ukimnyang’anya utasema umemuonea?” alihoji Rais Magufuli.

VIWANDA
Rais Magufuli alisema hivi sasa wanahangika kuhimiza ujenzi wa viwanda na katika mkoa wa Pwani. tayari wameshajenga viwanda zaidi ya 371, vikubwa zaidi ya 89 na pia katika mkoa wa Mwanza.

“Tumewapa marafiki zetu tukiamini tukiwapa watajenga ajira na serikali itapata kodi lakini hawakufanya hivyo,” alisema.

Alisema katika nchi za Ujerumani, Ethiopia na Kenya, viwanda vikubwa na mashirika muhimu humilikiwa na serikali; lakini nchini walipatiwa watu binasfi wamiliki jambo alilosema ni makosa.

“Sasa ninapokuta maovu kama haya, nyie watu wa Mungu mlionituma, niache kweli kuwashughulikia? Naomba muendelee kuniombea niendelee kuyashughulikia haya… niyanyooshe.

Nikiyaacha kwanza, nitamaliza kipindi changu cha miaka mitano au 10 na kuyaacha hivihivi,” alisema Rais Magufuli, akisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuendelea kumwombea kwa sababu kila anachokigusa anakuta maslahi ya watu wachache ambao walikuwa wakinufaika.

“Mimi ndiye Rais wa nchi hii na ninajua kila kitu kinachoendelea nchini na ndiyo maana nawaeleza ukweli,” alisema Magufuli.

“Tunataka Tanzania inyooke. Ili nikishaondoka iwe imeshanyooka na yule anayekuja aje atawale vizuri, kwa sababu lazima kuwapo na mtu mtangulizi, kulikuwapo na Yohana Mbatizaji ambaye alikuwa akiandaa mapito ya Bwana, basi na mimi mniache niandae vizuri mapito ya wanaokuja kutawala ili wakute vizuri na Watanzania wafaidi,” alisema.

Alisema zaidi ya Sh. trilioni 378 zimeibiwa ambazo zingeweza kuongoza nchi kwa zaidi ya miaka miwili na dhahabu zilikuwa zinasombwa kama Watanzania hawana ubongo.

Alisema waliokuwa wakihusika ni viongozi waliokuwa ndani ya serikali na kwamba wananchi walitakiwa wawe wanagawiwa mishahara kutokana na fedha zilizoibiwa.

“Fedha zinazochukuliwa hapa pengine ndizo zinazoendeshea nchi nyingine huko ambazo zinasema zimeendelea halafu zinatuletea mitumba hapa,” alisema Rais Magufuli.

MISWADA MADINI, BARABARA
Rais Magufuli alizungumzia pia uamuzi wa Serikali kupeleka miswada mitatu ya dharura bungeni, akisema hilo limetokana na umuhimu wa jambo hilo katika kutetea maslahi mapana ya nchi na kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi.

Akizungunzia ujenzi wa barabara ya kutoka Kamanga hadi Sengerema kwa kiwango cha lami, alisema kwa sasa Serikali imeshampata mkandarasi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu ili barabara hiyo ianze kujengwa katika kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Rais Magufuli pia aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya nchni kufafanua kwa wananchi na kusimamia uamuzi wa Serikali wa kufuta tozo zaidi ya 80 katika mazao ya kilimo, tozo saba za mifugo na tozo tano za uvuvi ambao lengo lake ni kuwaondolea kero wananchi.

ASISITIZA HATASOMESHA WAZAZI
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametoa onyo kwa wanaharakati wanaotaka wanafunzi wanaopata mimba warudi shule kuendelea na masomo baada ya kujifungua, watambue kuwa suala hilo halitokubalika katika utawala wake na wakitaka hivyo wajenge shule zao kwa ajili ya kusomesha wazazi.

''Haiwezekani Serikali itoe pesa kuwasomesha wanafunzi halafu wapate mimba waendelee na masomo hilo haliwezekani, hizo NGO zinazotetea hali hiyo zikitaka zijenge shule kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi watakaopata ujauzito,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Magufuli alitoa onyo kwa walimu pamoja na wakuu wa shule za serikali watakaowapokea wanafunzi walioacha shule kwa kupata ujauzito kuwa watakuwa wamejifukuzisha kazi kwa sababu wanafunzi wa aina hiyo wanaweza kusoma lakini siyo kwa shule za serikali.

UVUVI HARAMU, MAZINGIRA
Rais Magufuli alizungumzia pia uvuvi haramu na kuamuru viongozi wa mkoa wa Mwanza kuwashugulikia watu wote wanaovua samaki kwa kutumia sumu na kuharibu mazingira kwa kulima karibu na vyanzo vya maji.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Jonh Mongella, alimuhakikishia Rais Magufuli kuwa wanaendelea kupambana na uvuvi haramu

WAZIRI WA MAJI, MBUNGE
Awali, akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Greyson Lwenge, alisema mradi huo unatekelezwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kusimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa) na utazalisha hadi lita milioni 20.


Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, alimshukuru Rais kwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi ikiwamo kuufungua mradi huo ambao utawasaidia wana Sengerema ambao walikuwa na kilio kikubwa cha ukosefu wa maji safi na salama.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: