BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALI YA TANZANIA YAHAHA KUWAOKOA MADEREVA 20 WALIOTEKWA DRC NA KIKUNDI CHA MAI-MAI


Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga.

SERIKALI inafanya jitihada kuwaokoa madereva zaidi ya 20 waliotekwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kikundi cha waasi wa Mai-Mai, na tayari wamewasilisha maombi kwa Serikali ya DRC kusaidia kuwaondoa Watanzania hao katika eneo hilo hatari kwa usalama wao.

Waasi hao waliwashikilia madereva hao kwa muda, na baadaye kuwaachia huru kwa sharti la kuacha magari yao na mali zao zote, lakini kutokana na kukosa fedha na uhakika wa usalama wao njiani, madereva hao bado wamekwama kwenye eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, serikali imewashauri wafanyabiashara na watu wengine wanaokusudia kwenda mashariki mwa DRC kuwa waangalifu au kusitisha kwa muda safari zao kwa kuwa matukio ya kutekwa kwa madereva yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga alisema tukio hilo lilitokea katika eneo la Lulimba takribani kilometa 100 kutoka mji wa Baraka, Jimbo la Kivu Kusini.

Kasiga alisema kati ya madereva hao waliotekwa, Watanzania ni 21 na watatu ni Wakenya; na pia malori 21 yaliyotekwa 19 ni ya Kampuni ya Alistair na mengine mawili ni ya Kampuni ya Primefuels zote za Tanzania na walikuwa wanaelekea mgodi wa dhahabu wa Namoya Jimbo la Mainiema, unaomilikiwa na Kampuni ya Banro Gold ya Canada.

“Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzani nchini DRC, waasi wa Mai-Mai walishambulia msafara wa malori uliokuwa unasindikizwa na askari wa Jeshi la DRC (FARDC) na kufanikiwa kupora mali zao zote zikiwemo fedha na kuharibu baadhi ya malori kwa kutoboa matairi na kuvunja vioo,” alieleza Kasiga.

Alisema hatua ambazo serikali imechukua ni pamoja na kusisitiza operesheni inayoendelea itambue uwepo wa madereva hao na umuhimu wa kuwaokoa, na kueleza kuwa pia wanafanya mawasiliano ya moja kwa moja na madereva hao ili kujua hali zao na kiwango cha tishio la usalama kwenye eneo hilo kwa kuwa ipo hofu kwamba wanaweza kutumiwa kama ngao dhidi ya mashambulizi ya majeshi ya serikali.

“Uongozi wa Mgodi wa Namoya umeonesha ushirikiano mkubwa kwa ubalozi ambapo umejulisha hatua inazochukua ikiwemo kuwahamisha kwa muda wafanyakazi wa mgodi wakiwemo Watanzania kwenda katika mji wa Kindu, jimbo la Maniema,” alifafanua.

Alisema uongozi huo umeshauri madereva hao wabaki Lulimba hadi usalama utakapoimarika kutokana na operesheni ya FARDC huku ubalozi ukifuatilia maombi ya miadi ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Ndani na Ulinzi na Mkuu wa Kikosi cha MONUSCO ili kuzungumzia suala hilo na kuomba mamlaka zao zisaidie kadri inavyowezekana.
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment