BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TUCTA YACHOKONOA, KWA KULIAMSHA TENA DUDE LA VYETI FEKI


SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limeingilia kati sakata la vyeti feki kwa watumishi wa umma kwa kuiomba Serikali iwalipe mafao yao.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya, katika ufunguzi wa kikao cha Bodi ya Wadhamini wa shirikisho hilo.


“Tunawaomba watumishi wote ambao wamepitiwa na kadhia ya vyeti feki wawe watulivu wakati tukiwa tunaendelea kuangalia namna ya kukutana na Rais Dk. John Magufuli, kumweleza changamoto hiyo. Kuna watu wamefanya kazi kwa miaka 40 na walifanya vizuri, hivyo kuwafukuza ghafla tu si haki.

“Kwa sababu waliitumikia nchi kwa weledi na uaminifu na mali za umma zikabaki salama, tunaiomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma walau wapate hata fedha zao za pensheni,” alisema Nyamhokya.

Katika hataua nyingine, Tucta imewataka maofisa utumishi nchini kuacha kuwaandikia barua za kuwafukuza kazi watumishi wenye elimu ya darasa la saba kwani Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, alishaagiza wasifukuzwe.


Alisema kuwa wamepata malalamiko kwa wanachama wao ambao wameandikiwa barua za kuachishwa kazi, licha ya kutokuwa na agizo lolote kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi.

“Rais Magufuli akiwa katika sherehe za Mei Mosi, mwaka huu zilizofanyika Moshi, alisema kama mfanyakazi ana cheti cha darasa la saba, hakuna haja ya kudanganya kwa sababu kuna kazi ambazo anaweza kuzifanya kulingana na elimu yake, kwa hiyo maofisa utumishi kuwaandikia barua za kuwaachisha kazi hawana mamlaka hayo kwani hawajapewa agizo la kufanya hivyo,” alisema Nyamhokya.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Tucta, Dk. Yahya Msigwa, alisema hadi sasa shirikisho hilo limeshapokea malalamiko kutoka kwa zaidi ya wafanyakazi 3,000 nchini ambao wametakiwa kuacha kazi.

Alisema watumishi hao wanatoka katika sekta ya afya na elimu na kwamba katika kila hospitali ya mkoa zaidi ya wauguzi 100 wametakiwa kuacha kazi kwa kigezo cha kuwa na elimu ya darasa la saba.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: