Tuachane na Jamal Malinzi ambaye anakabiliwa na changamoto ya kisheria. Aliondolewa kwenye uchaguzi, kwa hiyo hakushiriki. Tungoje Mahakama itakavyotafsiri sheria na kutoa hukumu.
Tujadili uchaguzi kama ulivyofanyika na matokeo yalivyodhihirika. Bila shaka lipo jambo la kujifunza kwa kupita katikati ya mchakato na matokeo katika jicho la tathmini iliyo chanya.
Rais ni Wallace Karia. Ushindi wake ni mkubwa kupita kiasi. Hakuna mgombea japo mmoja ambaye alipata kura za kumkaribia. Ni tofauti kubwa na kelele nyingi ambazo zilipigwa kuelekea uchaguzi.
Veterani wa soka aliyepata kung'ara akiwa na Klabu ya Yanga, Ally Mayay, alipigiwa chapuo la hali ya juu ili ashinde Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kama uchaguzi TFF kura zingekuwa zinapigwa nchi nzima, bila shaka leo hii Mayay angekuwa ameshakula kiapo cha kuongoza soka la Tanzania.
Ingekuwa uchaguzi TFF kura zinapigwa kwenye mitandao ya kijamii, Karia angepata kura sifuri. Maana hakuwa akitajwa japo kwa mbali. Mayay angeshinda uchaguzi kwa urahisi mno, kama kipepeo anavyopepea.
Kura za TFF zinapigwa na wajumbe wa mkutano mkuu ambao idadi yao haizidi 130. Mathalan, maelfu ya tweet na ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kumfanyia kampeni Mayay hazikufaa kitu. Kura 128 tu zilipigwa. 95 zikaamua Rais ni Karia.
Kura hizo za Karia maana yake ameshinda kwa zaidi ya asilimia 74.2. Mayay amepata kura tisa, sawa na asilimia saba, akilingana na Richard Shija.
Wakili Iman Madega ameondoka na kura zake nane, Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Frederick Mwakalebela amepata kura tatu na Emmanuel Kimbe amejipatia kura yake moja.
NINI SOMO HAPO?
Somo la kwanza ni kuwa Karia amebebwa na uwepo wake ndani ya mfumo. Yeye ndiye Makamu wa Rais wa TFF, kwa hiyo ilikuwa rahisi kwake kuzungumza lugha moja na wapigakura kuliko wagombea wengine wote.
Ushindi wa tofauti kubwa ambao Karia ameupata maana yake ni kuwa ushawishi wake ulikuwa mkubwa na wajumbe walimwelewa zaidi kuliko wengine wote.
Somo la pili unalipata kutoka kwenye matokeo ya uchaguzi TFF kupitia kauli aliyowahi kuitoa Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump, alipoambiwa kuwa ushindi wake siyo sawa kwa sababu alizidiwa kura za umma na aliyekuwa mshindani wake, Hillary Clinton.
Katika kura za umma (majority votes), Hillary alimzidi Trump kwa zaidi ya kura 2.9 milioni. Hata hivyo, majority votes haziamui mshindi wa Urais Marekani.
Mshindi wa Urais Marekani huamuliwa kwa kura za majimbo (electoral votes). Wanaopiga kura za majimbo Marekani ni wajumbe wanaounda chombo kinachoitwa Electoral College ambao idadi yao ni 538.
Hivyo, unaweza kupata kura makumi milioni kutoka kwa umma lakini wajumbe 270 tu wa Electoral College wakimchagua mpinzani wako, anakuwa Rais, wewe unabaki na kura zako.
Trump alipata kura 304 za Electoral College, sawa na asilimia 56.5. Kura 270 tu zingetosha kumpa ushindi, lakini alivuka mpaka 304. Maana yake ni kuwa Trump alipata ushindi wa kishindo.
Hivyo, Trump alipozodolewa kuwa hakushinda kwa sababu alizidiwa kura za umma na Hillary, alijibu kuwa yeye hakujishughulisha kutafuta kura za umma kwa sababu hazingempa ushindi. Alishughulika na wajumbe wa Electoral College.
Majibu hayo ndiyo yanatuleta kwenye matokeo ya uchaguzi wa Rais TFF na kura za Mayay. Kwamba Karia hakujishughulisha na mitandao ya kijamii kwa sababu alijua watumiaji wake kwa mamilioni wasingeweza kumpa ushindi. Alishughulika na wajumbe wa Mkutano Mkuu TFF.
Mayay na watu wake, nguvu yao kubwa waliielekeza kwenye vyombo vya habari hususan mitandao ya kijamii, hivyo amevuna kura nyingi za umma, lakini amepigwa mwereka mkubwa kwenye kura rasmi zenye kuamua matokeo.
Hiyo ni elimu mahsusi kuwa unapokuwa unahitaji kufanikisha jambo fulani, hakikisha unafanyia kazi mazingira sahihi. Unavuna kile ambacho umepanda. Ukitaka uongozi wa TFF shughulika zaidi na wajumbe. Siyo nje kelele nyingi kumbe umaarufu wako kwa wajumbe ni mdogo.
ELIMU YA KUPAMBANA
Uchaguzi wakati mwingine ni kubahatisha na huwezi kubahatika kama hubahatishi. Ni kweli kuwa lazima kufanya utafiti na kujiridhisha kuhusu nguvu yako kabla ya kuingia kwenye uchaguzi lakini usimchukulie poa anayejaribu.
Katika uchaguzi wa TFF mwaka huu, mashujaa wangu ni Michael Wambura aliyeshinda Umakamu wa Rais na Mwakalebela aliyegombea Urais na kupata kura tatu, sawa na asilimia 2.3.
Kwa nini shujaa wangu asiwe Rais Karia awe Wambura aliyeshinda Umakamu wa Rais? Jawabu langu halina kupinda kwa sababu haikuwa rahisi kwa Wambura kufika alipofikia.
Wambura alikuwa Katibu Mkuu wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (Fat), na ndiye aliyesimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba na mfumo wa uendeshaji wa soka, vilevile kubadili jina kutoka Fat kuwa TFF.
Wambura aligombea Urais TFF katika uchaguzi wa kwanza wa shirikisho hilo mwaka 2004. Alitoka wa pili nyuma ya Leodgar Tenga aliyeongoza kwa vipindi viwili.
Baada ya kuondoka TFF, mwaka 2006 Wambura aliteuliwa na aliyekuwa mlezi wa Simba, Prof Philemon Sarungi kuwa Mwenyekiti wa Simba kabla ya Baraza la Wazee kuuondoa uongozi wake na kuitisha uchaguzi uliomuingiza madarakani Hassan Dalali.
Kuanzia hapo, Wambura aliingia kwenye misukosuko mfululizo kwa kuzuiwa kugombea uongozi Simba na TFF. Kila alipochukua fomu aliwekewa pingamizi na kuondolewa.
Zipo nyakati Wambura alilazimika kwenda mahakamani huku akifahamu kuwa migogoro ya soka haitakiwi kupelekwa kwenye mahakama za kiraia. Alifika huko katika hali ya kutapatapa kutafuta kile ambacho aliamini ni haki yake.
Kuna wakati Wambura alifukuzwa uanachama Simba kisha akasamehewa. Pamoja na kupata misukosuko yote, Wambura hakuwahi kukata tamaa. Kila alipozuiwa uchaguzi huu, uliofuata alishiriki.
Kipindi cha uongozi wa Tenga, Wambura alijaribu kugombea uenyekiti wa soka Mkoa wa Mara lakini aliondolewa kwenye uchaguzi. Wambura alikuwa kama kirusi TFF na Simba.
Wambura hakutakiwa Simba, TFF alipigwa mateke mengi na kufurumushwa mbali kila alipothubutu kujaribu kugombea. Hata hivyo, alibaki kwenye msimamo wake. Aliendelea tena na tena.
Mwaka jana aligombea uenyekiti wa Chama cha Soka Mara (MRFA), ikawa bahati uongozi wa Malinzi haukuwa na kinyongo naye, akashiriki uchaguzi na kushinda.
Baada ya hapo amegombea Umakamu wa Rais TFF na kushinda. Ushindi huo unamaanisha kurudi TFF baada ya kuondoka miaka 13 iliyopita. Ni shule kuwa wakati wowote kabili vikwazo ukibadili mbinu tofauti mpaka ushinde.
Nimejifunza kuwa wakati mwingine ili kufanikisha ndoto inabidi uwe king'ang'anizi hasa. Huwezi kuachiwa njia kisha upite kirahisi. Unatakiwa kupambana kuzibua njia inayozibwa kwa juhudi na uking'ang'anizi mkubwa. Ni muhimu sana.
SHUJAA MWAKALEBELA
Mwakalebela alikuwa Katibu Mkuu TFF nyakati ambazo shirikisho hilo lilifanikiwa kulijengea hadhi kubwa soka la Tanzania. Rais Tenga, Katibu Mkuu Mwakalebela, Kocha Marcio Maximo, soka lilikuwa na mvuto hasa wakati huo.
Mwakalebela aliacha TFF mwenyewe, lengo likiwa kwenda kwenye harakati mpya za siasa. Aliwania tiketi ya CCM kuwa mgombea ubunge jimbo la Iringa Mjini nwaka 2010 na kushinda lakini alikatwa na uongozi wa chama, nafasi yake akapewa Monica Mbega aliyeshindwa na Peter Msigwa wa Chadema.
Mwakalebela alikatwa na CCM kwa madai kuwa alitoa rushwa wakati wa kuwania tiketi. Pamoja na kukatwa, vilevile alikabiliwa pia na kesi mahakamani ambayo baadaye alikutwa hana hatia.
Februari 2015 Mwakalebela aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Waging'ombe. Hata hivyo, miezi mitano baadaye alijiuzulu na kurejea tena kwenye kinyang'anyiro cha ubunge. Aligombea tiketi ya kuwa mgombea ubunge wa CCM Iringa Mjini na kushinda lakini alishindwa na Msigwa wa Chadema.
Kukaa na kusikilizia majeraha ya kushindwa siyo asili ya wapambanaji, ndiyo maana hivi karibuni Mwakalebela aliibuka tena TFF kuwania Urais. Pamoja na kupata kura tatu na kuwa wa pili kutoka mwisho katika wagombea wote wa Urais TFF, lakini ina maana kubwa katika eneo la kupambana.
Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln ndiye anayetajwa kuwa Rais bora kabisa kuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo. Hata hivyo, kupata nafasi hiyo ilibidi apambane sana.
Lincoln alishindwa mara nyingi na hakukata tamaa. Kila aliposhindwa nafasi moja, uchaguzi mwingine aligombea nafasi nyingine na kushindwa. Neno kukata tamaa halikuwemo kwenye misamiati ya kichwani kwa Lincoln.
Kwa maana hiyo, thamani ya Lincoln ilifichwa kwenye moyo wake wa kutokata tamaa. Angevunjika moyo na kuacha kugombea baada ya kuanguka mara kwa mara, leo hii asingekuwa anatamkwa kuwa Rais bora, vilevile asingekuwa anazungumzwa leo kuwa aliwahi kuwa Rais. Angekuwa ameshasahaulika.
Hivyo, moyo wa Mwakalebela wa kupambana ndiyo moyo wa Lincoln. Inawezekana siku za baadaye tukamzungumza katika utambulisho wa heshima zaidi. Kupambana na kung'ang'ana na kile unachokiota mara nyingi huwa inalipa sana.
Natoa salamu nyingi za heshima kwa Mwakalebela. Watu aina yake huwa hawazaliwi kila siku. Kuendelea kupambana kwa malengo ni jambo jema. Yapo matunda kwa wenye kupigania ndoto bila kuchoka.
UJUMBE KWA WALIOSHINDWA
Unapoingia kwenye uchaguzi unapaswa kufahamu kuwa wanaoamua ushinde ni wapigakura. Wakiona mwenzako ni bora zaidi humchagua yeye, kwa hiyo siyo vita.
Wanapoona mwenzako ni bora, haimaanishi kuwa kweli yeye ndiye bora zaidi yako, isipokuwa ni mtazamo wao. Unapaswa kuwaheshimu kwa namna ambavyo wameona. Upo wakati kila mmoja atakuona bora. Kinaweza pia kuwepo kipindi cha watu kujuta kutokukuchagua. Yote yanawezekana.
Kwa Mayay na wote ambao wameshindwa uchaguzi TFF, hayo ni matokeo. Mara nyingi kushindwa uchaguzi hutoa ujumbe kuwa muda bado. Hivyo, muda ukifika hakutakuwa na kipingamizi. Njia itakuwa nyeupe kabisa.
Lincoln alipambana sana lakini muda wake ulikuwa bado. Muda ulipofika aliingia The Oval Office, White House na kuongoza Taifa la Marekani. Muda ulipokuwa bado Wambura alikutana na vikwazo vingi, muda ulipowadia kila kitu kimekuwa mteremko, leo Wambura ni Makamu wa Rais TFF.
Dk John Magufuli aligombea tiketi ya kuwa mgombea Urais kupitia CCM mwaka 2005 lakini hakufika hata Tano Bora. Mwaka 2015, kila kitu kikawa tambarare na leo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais wa Nne, Dk Jakaya Kikwete aligombea tiketi ya kuwa mgombea Urais kupitia CCM akashindwa mwaka 1995. Mwaka 2005, haikuwa rahisi kumzuia. Ni suala la wakati, Ndimi Luqman MALOTO

0 comments:
Post a Comment