BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAKATI PROF LIPUMBA AKIWATIMUA WABUNGE NANE, NAYE MAALIM SEIF HAMAD AMTIMUA SAKAYAkaya

Waliokuwa Wabunge wa viti Maalum wa CUF waliovuliwa uanachama kutokana na mvutano wa uongozi wa chama hicho, wakingia katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam jana kusikiliza maombi yao ya kuzuia kuapishwa kwa wabunge walioteuliwa kuchukua nafasi zao. Picha na Omar Fungo

Waliokuwa wabunge wa viti maalumu wa CUF, waliokimbilia mahakamani wamewekwa njiapanda baada ya kukumbana na pingamizi la maombi yao ya kusimamisha uapishwaji wa wabunge wapya walioteuliwa kuziba nafasi zao.

Wabunge hao walifungua maombi Mahakama Kuu wakiomba itoe amri ya zuio kwa Bunge ili wateule hao wasiapishwe, kusubiri kusikilizwa na kutolewa uamuzi wa kesi waliyoifungua kupinga kufukuzwa uanachama wa chama hicho.

Maombi hayo yalitarajiwa kusikilizwa jana na Jaji Lugano Mwandambo, lakini yalikumbana na pingamizi la awali kutoka kwa wajibu maombi, wakiiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali kwa madai kuwa ni batili na kuwasilisha hoja nne kuyakosoa, jambo ambalo limeyafanya yabaki njia panda.

Waombaji hao ni Miza Bakari Haji na wenzake saba wakati wajibu maombi ni Katibu wa Bunge, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bodi ya Wadhamini wa CUF na wabunge wateule wanane.

Mbali na Miza, waombaji wengine katika maombi hayo ni Saverina Silvanus Mwijage, Salma Mohamed Mwassa, Raisa Abdallah Musa, Riziki Shahari Mngwali, Hadija Salum Al- Qassmay, Halima Ali Mohamed na Saumu Heri Sakala na madiwani Elizabeth Alatanga Magwaja na Layla Hussein Madib.

Lakini, NEC na Bunge waliowakilishwa na jopo la mawakili wanane wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata katika pingamizi lao wamewasilisha hoja tatu, moja wakidai kuwa maombi hayo ni batili kwa kuwa yamefunguliwa kwa kifungu kisicho sahihi.

Walidai kuwa Kifungu cha 2(3) Sheria ya Mamlaka ya Mahakama Kuu kutumia sheria za nje hususan za Uingereza (Jala) siyo sahihi kwani hicho kinatoa ridhaa tu kwa mahakama kutumia sheria za nje pale ambako kunakuwa hakuna kifungu rasmi katika sheria za nchi.

Malata alisema walipaswa kuonyesha kifungu rasmi katika sheria za Uingereza kinachotumika kulingana na mazingira ya maombi yao.

Katika hoja nyingine, Malata alidai kuwa nafuu wanazoziomba haziwezi kutolewa na mahakama hiyo kwa kuwa zinalenga kwenda kuzuia utekelezaji wa majukumu ya kikatiba ya mhimili mwingine (Bunge).

Katika hoja ya tatu ya pingamizi hilo, alidai kuwa maombi hayo ni ya usumbufu na matumizi mabaya ya mwenendo wa mahakama kwa kuwa watoa maombi wanaomba nafuu kwa jambo moja katika mamlaka mbili tofauti.

Alifafanua kuwa licha ya kufungua maombi hayo pia wamekata rufaa kwenye Mkutano Mkuu wa CUF kupinga kufukuzwa uanachama na hivyo kupoteza ubunge jambo ambalo alisema si sawa.

Bodi ya CUF na wabunge wateule wanaowakilishwa na wakili Mashaka Ngole, walikuwa na hoja moja ya pingamizi, wakidai kuwa maombi hayo ni batili kwa kuwa yamewahusisha wajibu maombi ambao hawako kwenye kesi ya msingi ambayo maombi hayo yametokana nao (wabunge wateule).

Wakili Ngole alisema kitendo hicho cha kuwajumuisha wabunge wateule kwenye maombi hayo wakati hawako kwenye kesi ya msingi kinawanyima haki ya kusikilizwa.

Akijibu hoja hizo, wakili wa waombaji hao, Peter Kibatala akisaidiana na wakili Omari Msemo alidai kuwa hoja hizo hazina mashiko kisheria na akaiomba mahakama izitupilie mbali.

Wakili Kibatala alifafanua kuwa kifungu walichokitumia kufungua maombi hayo ni sahihi huku akirejea kesi mbalimbali zilizokwishakuamuliwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani akidai kuwa zilihalalisha matumizi ya kifungu hicho.

Kuhusu hoja ya kuzuia Bunge kutekeleza majukumu yake, alidai kuwa mahakama ndicho chombo cha kutoa haki na kwamba hakuna kanuni ya kisheria inayoizuia kutoa haki kwa mambo yanayohusiana na Bunge na kwamba imekuwa ikifanya hivyo.

Kuhusu kuwajumuisha wajibu maombi wengine kwenye kesi ya msingi alidai kuwa upo uamuzi wa kuteuliwa kwa wabunge wapya uliofanyika wakiwa tayari wameshafungua kesi ya msingi na kwamba maelezo ya jambo hilo yako kwenye hati ya kiapo.

Kutokana na pingamizi hilo, mahakama ililazimika kusitisha usikilizwaji wa maombi ya msingi hivyo kusikiliza kwanza hoja za mapingamizi ya awali yaliyowasilishwa na wajibu maombi hayo ili kuyatolea uamuzi kabla ya kuendelea na maombi hayo. 


Usikilizwaji wa maombi hayo sasa unategemea uamuzi wa mapingamizi hayo utakaotolewa kesho na Jaji Mwandambo.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: