BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TAASISI YA UTAFITI WA MIWA KIBAHA YAWAFUMBUA MACHO WAKULIMA WADOGO KUEPUKA HASARA.


Mhariri Mwandamizi wa kituo cha redio cha Uhuru FM, Stephen Mhina akizungumza jambo wakati wa warsha ya wadau wa zao la miwa ya mpangilio wa vipindi vya redio vya ukulima bora iliyofanyika Morogoro na kuandaliwa na taasisi ya utafiti wa miwa Kibaha inayotarajia kutoa mafunzo kwa wakulima wa zao la miwa wa kutengeneza sukari. Picha na Juma Mtanda.

Juma Mtanda, Morogoro.
Taasisi ya utafiti wa miwa Kibaha imewafumbua macho wakulima wadogo wa zao la miwa wa kutengenezea sukari kuwa wanaweza kuepukana na hasara ya mashamba kuungua moto kama watafuata njia za kulinda shamba iliyofanyika mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa warsha ya wadau wa zao la miwa juu ya mpangilio wa vipindi vya redio vya ukulima bora wa miwa mjini hapa, Mtafiti Kiongozi wa taasisi ya utafiti wa Miwa Kibaha, Dk Hildelitha Msita alisema kuwa kesi za mashamba ya miwa kuungua moto hujitokeza wakati wa mavuno kwa mkulima kuingiwa na tamaa ya kuvuniwa haraka.

Kutokana na majibu ya utafiti mbalimbali uliofanywa na taasisi hiyo wamegundua mambo mengi yanayopelekea hasara kupatikana lakini watajikita kutoa mafunzo ya kuondokana na kilimo cha mazowea na kuingia kilimo cha utalaamu ili kuweza kupata mavuno kati ya tani 90-120 kwa hekta moja.

Warsha hiyo ya siku moja iliwashirikisha watalaamu wa kilimo cha miwa, wakulima, viongozi wa vyama vya wakulima wa miwa, wandishi wa habari, mabwanashamba na waandaaji wa vipindi vya redio kutoka wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi .

“Wakulima wadogo wa zao hili wamekuwa wakilima kilimo cha mazowea ambacho kimekuwa kikiwapatia mavuno madogo kati ya tani 25 hadi 40 kwa hekta moja jambo linalowakatisha tamaa baadhi yao lakini wamekuwa wakipata hasara nyingine kwa mashamba yao kuungua moto.”alisema Dk Msita.

Dk Msita alisema kuwa miwa ikichomwa moto kwa ajili kuvunwa inapaswa kukaa shamba ndani ya saa 70 tu na baada ya hapo huharibika lakini kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakulima kuchoma moto shamba kwa lengo la kuvuniwa haraka na matokeo yake wamekuwa wakiangukia kwenye hasara.

Aliongeza kwa kusema kuwa zipo tafiti, taasisi hiyo imefanya na kubaini baadhi ya wakulima wamekuwa wakichoma moto shamba lao ili wavuniwe haraka na miwa inapokaa shambani kwa zaidi ya saa 70 huharibika lakini wanaweza kujiepusha endapo watafuata taratibu za uvunaji za kiwanda.

Dk Msita alisema kuwa shamba la miwa lipaswa kulindwa kwa kulima nyasi pembe zote za shamba ili kuzuia moto kuingia lakini hata mkulima anayejiandaa kuchoma moto kwa ajili ya kuvuna miwa anapaswa kulinda shamba la mwenzake.

Wakulima hao watapokea mafunzo kwa njia ya redio baada ya jopo la wadau wa zao hilo kuandaa ujumbe wa mafunzo juu ya kilimo bora cha zao la miwa ya kutengeneza sukari na njia za kukailiana na ajali za moto.

Mkufunzi wa warsha hiyo, John Msemo alisema kuwa katika warsha hiyo wadau hao wamefundishwa mpangilio wa vipindi vya ukulima bora wa miwa juu ya njia bora za kilimo cha miwa, aina bora ya mbegu zenye upinzani na magonjwa na matumizi bora ya mbolea katika kukuza miwa na kutambua aina ya viua magugu na njia za kuwadhibiti wadudu waharibifu wa zao hilo.

Msemo alitaja baadhi ya masomo hayo kuwa ni mbegu za miwa na maandalizi ya shamba, maandalizi ya kupanda shamba la miwa, shamba la mbegu na uzalishaji, matumizi bora ya mbole na udhibiti wa visumbufu vya miwa.

Mafunzo mengine yatayotolewa kwa wakulima hao ni udhibiti wa magugu, wadudu waharibifu wa miwa, magonjwa ya miwa, kinga ya moto, Uvunaji na maandalizi yake na usalama wa mazingira.

Kwa upande wa mkulima wa miwa kutoka kijiji cha Luhembe wilayani Kilosa, Lazaro Benard alisema kuwa ana imani mafunzo kwa njia ya redio yatamsaidia mkulima katika kuboresha na kilimo cha kitalaamu na kupata mavuno ya tani 90 hadi 120 kwa hekta moja.

“Mafunzo kwa njia ya redio yatatusaidia kulima kilimo bora ili kuondokana na vikwazo vinavyopelekea sisi kupata mavuno kidogo kunatokana na kilimo cha mazowea na nina imani tutajua njia bora za kilimo cha kitalaam.”alisema Bernard.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: