BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAHARIFU WALIOTEKELEZA MAUAJI WILAYA ZA MKURANGA, KIBITI NA RUFIJI WAKIMBILIA MIKOA YA MTWARA, GEITA NA LINDI


Jeshi la polisi limesema baadhi ya wahalifu waliohusika na mauaji ya kutumia silaha katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani wamekimbilia mikoa hiyo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

IGP Sirro alisema jeshi hilo limewakamata wahalifu waliokuwa wakijihusisha na matukio hayo, lakini baadhi walikimbilia mikoa hiyo na nchi jirani zikiwemo Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hata hivyo alisema kutokana na ushirikiano uliopo watashughulikiwa huko walikokimbilia.

Alisema baadhi ya waliokamatwa wamekutwa na silaha nyingi ambazo hata hivyo hakutaja idadi akisema atafanya hivyo wakati mwingine.

Wakati IGP Sirro akiitaja mikoa hiyo, hivi karibuni Polisi mkoani Shinyanga ilisema watu watano wanaosadikiwa kuwa majambazi waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi waliokuwa doria.

Taarifa ya polisi ilisema watu hao waliuawa walipojaribu kuwavamia wafanyabiashara wa madini katika machimbo ya Mwime nje kidogo ya Mji wa Kahama na kwamba watuhumiwa wanadaiwa kuhusika na mauaji ya viongozi wa Serikali ya Mtaa na wanasiasa mkoani Pwani katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule alisema watu hao walijeruhiwa usiku katika eneo la Mwanva katika Halmashauri ya Mji wa Kahama walipokabiliana ana kwa ana na polisi waliofika eneo hilo.

Baada ya tukio hilo, alisema katika eneo la tukio polisi walikuta bunduki moja aina ya SMG na risasi 25 zilizokuwa kwenye magazini. Pia, mabomu mawili ya kutupa kwa mkono.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba akizungumzia matukio ya uhalifu huo hivi karibuni alisema mapambano ni endelevu ndiyo maana kumeanzishwa mkoa wa kipolisi wa Rufiji na kuongezwa vitendea kazi, doria na askari.

Nchemba alisema pia wameboresha utafutaji wa taarifa za kihalifu ili kuwa mbele ya wahalifu.

Watu wapatao 30 katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji wakiwemo askari polisi, viongozi wa serikali za mitaa na raia waliuawa katika matukio hayo yaliyotokea kuanzia Mei mwaka jana hadi katikati ya mwaka huu kwa mujibu wa ufuatiliaji uliofanywa na gazeti hili. 


Rais John Magufuli Mei mwaka huu alitengua uteuzi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu na kumteua IGP Sirro ikiwa ni siku chache baada ya vifo vya askari wanane waliouawa wakiwa katika doria wilayani Mkuranga.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: