TAARIFA YA TATHMINI YA UTENDAJI NA UTEKELEZAJI WA AWAMU YA PILI YA MPANGO MKAKATI WA BARAZA LA TAIFA LA USALAMA BARABARANI WA KUPUNGUZA AJALI ZA BARABARANI KWA ASILIMIA 10% KATIKA KIPINDI CHA MIEZI SITA (6) KUANZIA JULAI – DESEMBA, 2017.
Ndugu Wanahabari,
Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Tanzanaia (BARAZA) lilianzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 96 cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168. BARAZA hili ndilo lenye dhamana ya kusimamia masuala yote ya Usalama Barabarani hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuzuia ajali za Barabarani.
Ndugu Wanahabari,
Katika kuhakikisha ajali za Barabarani zinapungua kwa kiwango kikubwa kama si kuzimaliza kabisa hapa nchini, BARAZA liliandaa Mpango Mkakati wa kupunguza Ajali za barabarani kwa Asilimia 10% katika kipindi cha miezi Sita (6). Mpango ambao utekelezaji wake wa Awamu ya Kwanza ulianza Agosti mwaka, 2016 na utekelezaji wake kuendelea hadi Januari, 2017.
Ndugu Wanahabari,
Tathmini ya utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mpango Mkakati iliyofanyika na kubainisha kupungua kwa Ajali kwa asilimia 11%. Asilimia 1% zaidi ya malengo yaliyokusudiwa na Mpango Mkakati huo. Kutokana na tathmini hiyo, BARAZA liliagiza Mpango Mkakati huo uendelee kutekelezwa katika Awamu ya Pili kuanzia Julai – Desemba, 2017. Mkazo zaidi uwe katika kutoa Elimu ya Usalama Barabarani, kufanya Operesheni za kuzuia makosa hatarishi ambayo yamekuwa ni chanzo cha ajali za barabarani na kusimamia Sheria kwa kuchukua hatua kali kwa madereva wazembe wasiozingatia Sheria ili kuwajengea Utii wa Sheria bila Shuruti,Kwa kuwakamata, kuwaweka Mahabusu, kuwapeleka Mahakamani na kufungia leseni zao za udereva.
Ndugu Wanahabari,
Tathimini ya utendaji na utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango Mkakati ilifanywa na BARAZA tarehe 20/2/2018 na kubainisha kuwepo kwa upungufu wa Ajali, Vifo na Majeruhi.Tathimini hii inathibitishwa na takwimu za ajali zinazoonyesha kwamba Katika Kipindi cha Julai – Desemba, 2017 kulitokea Ajali 2,683 zilisababisha Vifo 1,330 na Majeruhi 2,748. Takwimu hizo zikilinganishwa na takwimu za Kipindi kama hicho cha Julai – Desemba, 2016 ambapo kulitokea jumla ya Ajali 4,704 ambazo zilisababisha Vifo 1,676 na Majeruhi 4,299.
Mchanganuo wa takwimu hizi unaonyesha kupungua kwa Ajali 2,021 ambazo ni sawa na asilimia 43%, kupungua kwa Vifo 346 ambavyo ni sawa na asilimia 21% na kupungua kwa majeruhi 1,551 ambao ni sawa asilimia 36%.
Hivyo, malengo ya Mpango Mkakati Awamu ya Pili yamefikiwa kwa zaidi ya asilimia 33%.
Ndugu Wanahabari,
Kutokana na utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango Mkakati, ajali zilipungua mwishoni mwa mwaka 2017 na mwanzoni mwa mwaka 2018 tofauti na hali iliyozoeleka miaka ya nyuma, ambapo Kipindi cha mwishoni na mwanzoni mwa mwaka vilikuwa ni vipindi vyenye ajali nyingi na kuwajengea hofu kwa Wananchi.
Ndugu Wanahabari,
Utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango Mkakati wa BARAZA, uliendana na zoezi la Ukaguzi wa Magari wa lazima (Mandatory Motor Vehicle Inspection) ulioanza tangu tarehe 16/10/2017 wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa Mkoani Kilimanjaro. Ukaguzi huu ulihusisha Magari ya biashara ya kubeba Abiria na Mizigo.
BARAZA limefanya Tathmini ya Ukaguzi huo na kufanikiwa jumla ya magari yote ya Abiria na Mizigo yaliyokaguliwa ni 82,208, kati ya hayo Magari yaliyokutwa mazima na kubandikwa stika ni 79,221 na magari 2,987 yalibainika kuwana dosari, ambazo wamiliki walitakiwa kwenda kuzirekebisha na kuyarejesha tena kwa Ukaguzi kabla ya kubandikwa Stika na kuruhusiwa kutembea barabarani.
Tathmini hii inaonyesha kwamba Ukaguzi umefanyika kwa kiwango kikubwa ambapo 79% ya magari yote yamekaguliwa.
Ndugu Wanahabari,
Kutokana na kiwango hicho kilichofikiwa cha ukaguzi wa Magari na ukaguzi wa Pikipiki, BARAZA limeagiza kuanzia tarehe 01/03/2018, uanze Ukaguzi wa magari ya watu binafsi kwa nchi nzima.Ukaguzi huo utafanyika kwa kipindi cha miezi miwili na Tathimini itafanyika kupima ufanisi kabla ya kuanza Magari binafsi yatakayo kaguliwa na kuonekana yana ubora unaofaa kutembea barabarani (Road worthness) yatabandikwa Stika ambayo italipiwa kwa Tsha. 3,000/=.
Hivyo natangaza rasmi kwamba ukaguzi wa magari binafsi utaanza tarehe 01/03/2018 katika mikoa yote nchini.
Wamiliki wapeleke magari yao katika vituo vya Polisi na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Ukaguzi ili yakaguliwe.
Mamlaka,Mashirika,Idara na Taasisi mbalimbali za serikali zenye wafanyakazi wengi wenye Magari wanaweza kuleta maombi ya wakaguzi wa Magari na magari yao yakakaguliwe katika maeneo yao ya kazi.
Ndugu Wanahabari,
Kwa Wamiliki wa Magari ya biashara na Mizigo ambao Magari yao hayajakaguliwa, wayapeleke haraka yakakaguliwe. Kuanzia tarehe 01/03/2018 tutaanza msako mkali wa kuyakamata magari ambayo yatakuwa hayajakaguliwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Ndugu Wanahabari,
Kutokana na Mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango Mkakati, BARAZA limeagiza utekelezaji uendelee katika Awamu ya Tatu. Kwa kipindi cha miezi 6 mingine. kuanzia tarehe 01/03/2018 hadi tarehe 30/09/2018 na kiwango cha kupunguza ajali kiwe asilimia 25% badala ya asilimia 10% kwa kipindi cha miezi sita (6).
Hivyo natanagaza rasmi kwamba, utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mpango Mkakati wa BARAZA utaanza rasmi tarehe 01/03/2018 hadi tarehe 30/09/2018 nchini kote.
Ndugu Wanahabari,
Katika utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mpango Mkakati, BARAZA limeagiza usimamizi mkali ufanyike katika kudhibiti Pikipiki (Boda boda), Makosa ya mwendo kasi wa magari, Madereva Walevi, Madereva wanayoyapita magari mengine bila kuchukua tahadhali (Improper Overtaking) na kubeba Abiria na Mizigo kupita kiasi na kwa njia ya hatari.Usimamizi huu utaendana na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya Watumiaji wa barabara kufanya Operesheni kali ya kuwakamata madereva wanaofanya makosa hatarishi barabarani na kusimamia sharia kwa kuwakamata madereva wasiotii sheria, kuwaweka mahabusu, kuwafikisha Mahakamani na kufungia leseni zao za Udereva.
Hatua hizi zitasaidia kuwajengea uelewa wa Usalama Barabarani watumiaji wa barabara na madereva wataogopa kufanya makosa barabarani na hivyo kuwa na Utii wa Sheria bila Shuruti. Kitendo ambacho kitapelekea kupungua kwa ajali, na kufikia hata kuvuka malengo ya Mpango Mkakati wa Awamu hiyo ya Tatu.
Ndugu Wanahabari,
Katika kudhibiti makosa ya Pikipiki (Boda boda) ya kupita taa nyekundu, kutovaa Kofia ngumu na kubeba abiria zaidi ya mmoja (Mishikaki), BARAZA linatafuta mfadhili atakayesaidia kufunga Kamera kwenye baadhi ya makutano ya Barabara (Junctions) ili kuwakamata Bodaboda watakaofanya Makosa hayo na kupita katika maeneo hayo.
Aidha, tumebaini kuwa Pikipiki (Boda boda) nyingi zimesajiliwa kwa majina ya Makampuni yanayouza Pikipiki badala ya Majina ya Wamiliki wa Pikipiki hizo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na kimekuwa kikisababisha usumbufu katika ukamataji wa Bodaboda.
Hivyo natamka Kuanzia sasa, Pikipiki ambazo zitakamatwa na kubainika kuwa zimesajiliwa kwa jina la kampuni badala ya jina la Mmiliki, wenye kampuni hizo watakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Naomba nitumie fursa hii kuziagiza kampuni zinazouza Pikipiki kuacha kuuza pikipiki zilizosajiliwa kwa majina ya Kampuni zao.
Wanapouza pikipiki wabadilishe umiliki na majina ya Wanunuzi yasomeke kwenye kadi kama wamiliki badala ya Kampuni, Kampuni itakayokiuka maagizo haya, kama nilivyosema Wamiliki watakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Ndugu Wanahabari,
Napenda nimalizie kwa kuwapongeza, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mtendaji, Wajumbe na Sekretarieti ya BARAZA, Wenyeviti, Makatibu na Wajumbe wa Kamati za Usalama Barabarani za Mikoa, Wilaya, na Sekretarieti zake Watendaji wote kwa kusimamia na kutekeleza kwa ufanisi mkubwa wa Mpango Mkakati huu wa Awamu ya pili wa BARAZA.
Pia, niwashukuru Wadau na jamii kwa ujumla kwa Ushirikiano mkubwa walioutoa kwa BARAZA na kwa Watendaji wote wakati wa utekelezaji wa Mpango Mkakati huu wa Awamu ya pili.
Aidha, niwapongeze ninyi Wanahabari kwa ushirikiano mliotoa kwa kuzitangaza shughuli za BARAZA katika Kipindi chote cha Utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango Mkakati Awamu hii ya pili.
Nawaomba wote kwa pamoja tuendelee kushirikiana vile vile katika Kipindi cha utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mpango mkakati wa BARAZA letu.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
ZUIA AJALI, TII SHERIA OKOA MAISHA.
AJALI ZA BARABARANI ZINAZUILIKA, ZINGATIA SHERIA.
MHE. ENG. HAMAD MASAUNI (MB)
MWENYEKITI,
BARAZA LA TAIFA LA USALAMA BARABARANI (T)

0 comments:
Post a Comment