Kaimu katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu watu waliokamatwa katika vurugu zilizotokea Februari 16 katika eneo la Kinondoni Mkwajuni. Picha na Omar Fungo. Iringa/Dar. Chadema ipo katika hatihati ya kuipoteza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutokana na wimbi la madiwani wake kujiuzulu.
Hiyo ni baada ya jana, Diwani wa Gangilonga, Dadi Igogo kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo na kufanya idadi ya madiwani wa Chadema katika halmashauri hiyo waliojiuzulu kufikia saba.
Kabla ya kujiuzulu udiwani, Igogo alijiuzulu nafasi ya naibu meya wa manispaa hiyo.
Hata hivyo, tofauti na madiwani wengi ambao wamekuwa wakijiuzulu kutoka upinzani, Igogo hakutangaza kujivua uanachama wa Chadema.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa manispaa hiyo, Omary Mkangama alisema baraza la madiwani la halmashauri linaundwa na wajumbe 28.
Kati ya hao, 18 ni madiwani wa kuchaguliwa, sita viti maalumu na wanne ni wabunge. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Chadema ilishinda kata 14 na CCM nne.
Kutokana na ushindi huo, Chadema ilipata madiwani watano wa viti maalumu, CCM ikiwa na mmoja hivyo kuiwezesha Chadema kuwa na madiwani 19 na CCM kuwa na madiwani watano na idadi hiyo ilifikia 28 kutokana na kila chama kuwa na wabunge wawili katika baraza hilo.
Tangu madiwani walipoanza kujiuzulu mwishoni mwa mwaka jana ambao idadi yao imefikia saba, Chadema imebakiwa nao saba wa kuchaguliwa kwenye kata huku wa CCM wakiongezeka kutoka wanne na kufikia sita baada ya uchaguzi mdogo na iwapo itashinda katika kata zilizo wazi, idadi ya hiyo itafikia kumi na moja.
Hilo likitokea, CCM pia itaongeza idadi ya madiwani wa viti maalumu.
Akizungumzia hilo, mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Said Lubeya alisema kuachia ngazi kwa madiwani ni afya kwenye chama chao kwa kuwa inaonyesha namna ambavyo viongozi hao hawaridhishwi na uwepo wao ndani ya Chadema.
Mwenyekiti wa Bavicha Manispaa ya Iringa, Lawrence Marto alisema kwa sasa hawana cha kufanya na wameamua kuwaacha wanaoondoka wafanye hivyo ili chama hicho kipate nafasi ya kujisuka upya.
Alisema walishakaa kuzungumza na madiwani hao wakaahidi hawataondoka lakini akashangaa kuona bado wimbi la kujiuzulu linaendelea.Mwananchi

0 comments:
Post a Comment