BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HUKUMU YA SUGU KUSOMWA LEO AKIDAIWA KUTUMIA LUGHA YA FEDHEHA DHIDI YA RAIS MAGUFULI MBEYA


Hatima ya mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ anayeshtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli itajulikana leo.

Sugu na katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ambayo leo itatoa hukumu.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30 mwaka jana, Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite anatarajiwa kutoa hukumu baada ya upande wa mashtaka na utetezi kukamilisha ushahidi tangu Februari 9.

Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.

Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka maneno wanayoshtakiwa kuyatoa.

Awali, washtakiwa hao walitetewa na mawakili; Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu lakini walijitoa.

Kwa mara ya kwanza, Sugu na Masonga walifikishwa mahakamani Januari 16 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyeeleza upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na usikilizaji.

Mawakili wengine wa Serikali walioendesha kesi hiyo ni Ofmed Mtenga na Baraka Mgaya.

Wakili Yongo aliiomba Mahakama kuwapa muda ili aweze kukaa na wateja wake kujadiliana kuhusu mashtaka hayo. Hakimu Mteite alikubali ombi hilo.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Pande uliiomba Mahakama kuzuia dhamana kwa washtakiwa akitoa sababu kwamba ni kwa ajili ya usalama wao.

Wakili Yongo alipinga ombi hilo akisema dhamana ni haki ya kikatiba ya washtakiwa.

Hata hivyo, Hakimu Mteite alikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka na kuzuia dhamana, hivyo Sugu na Masonga walikaa mahabusu katika Gereza Kuu la Ruanda kwa siku 24 kabla ya kuachiwa kwa dhamana Februari 9, kwa sharti la kusaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Yaliyojiri mahakamani

Kabla ya kuanza kutoa ushahidi, Sugu na Masonga wakiongozwa na mawakili wao Mwabukusi, Mwasipu na Yongo walimkataa Hakimu Mteite kuendelea kusikiliza kesi wakidai ana upendeleo, hawana imani naye.

Walimtaka ajiondoe na Mahakama impangie hakimu mwingine atakayeendesha kesi bila upendeleo.

Hakimu Mteite aligoma kujiondoa katika kesi hiyo akisema sababu zilizotolewa na washtakiwa hazina mashiko kisheria kwa kuwa suala la hakimu kujitoa katika kesi lipo kisheria na kwa sababu za msingi.

Aliamuru kesi kuendelea kwa Sugu na Masonga kuanza kutoa ushahidi.

Baada ya Hakimu Mteite kugoma kujitoa katika shauri hilo, mawakili wa utetezi Mwabukusi, Mwasipu na Yongo walitangaza kujiondoa kuwawakilisha washtakiwa.

Mawakili hao walitangaza kujiondoa wakisema hawaoni sababu ya kuwawakilisha wateja wao hao wakati tayari wamepishana na Mahakama.

Wakili Mwabukusi alisema, “Wakili ukiona huoni nuru au taratibu zinazoendelea ndani ya mahakama huna weledi nazo kuweza kumwakilisha mteja wako kikamilifu, wajibu wako ni kujitoa. Hivyo mimi na msaidizi wangu wakili Yongo tumejitoa rasmi kuwawakilisha wateja wetu.”

Wakili Mwasipu alisema kwa kuwa wateja wake tayari wameonekana kupishana na mahakama, haoni sababu ya kuendelea kuwawakilisha katika kesi hiyo.

Kutokana na hilo, Sugu na Masonga waliiomba mahakama kuwapata siku 14 ili watafute mawakili wengine. Ombi hilo lilikubaliwa na mahakama.

Februari 8, Sugu na Masonga walianza kutoa ushahidi wakiwa na wakili mpya, Peter Kibatala.

Wakili huyo aliwaongoza mashahidi sita kutoa ushahidi akiwamo Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mbeya, Modestus Chambu. 


Wakati kesi hiyo ikiendeshwa kwa mara kadhaa askari walikuwa wakiimarisha ulizi na kuna wakati wafuasi wa Chadema waliofika mahakamani walizuiwa kuingia ndani.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: