BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ULAJI WA CHIPS, SODA KWA AKINAMAMA WAJAWAZITO CHANZO CHA KUZAA WATOTO LEGELEGE


Kitendo cha baadhi ya wajawazito kuwadanganya waume zao kwamba wametakiwa na madaktari kutumia chips na soda wakati wa ujauzito ni sababu inayoelezwa kuzaa watoto wenye afya dhaifu.

Madai hayo yametolewa na baadhi ya wanaume walipozungumzia ukosefu wa lishe ya kutosha wakati wa kulea mimba kwa wanawake.

Wanaume waliohojiwa juu ya hali ya malezi ya wakati wa ujauzito walisema ulaji wa aina hiyo huchangia kuzaliwa watoto wenye udumavu wakiwamo wenye upungufu wa damu na afya dhaifu kutokana na mama zao kukosa lishe bora.

Mlolwa Madebe kutoka Kata ya Kilago alisema wengi wa wajawazito kwenye maeneo ya vijijini wanapenda vitu vizuri wakati wa ujauzito.

Alisema wajawazito hao wakishaanza kwenda kliniki wakitoka huko huwadanganya waume zao kwamba wameambiwa na madaktari wawe wanakula chips na kunywa soda, vyakula ambavyo havileti lishe bora kwa mtoto aliye tumboni.

Madebe alisema hali hiyo imeshika kasi kwenye maeneo ya vijijini ambako katika miaka ya karibuni wanawake wengi hawazingatii kula vyakula vyenye lishe bora wakati wa ujauzito.

Hata hivyo, kaimu mganga mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, John Mfutakamba aliwataka akina baba kuambatana na wake zao kwenda kliniki na kupewa maelekezo ya utunzaji mimba kwa pamoja hali ambayo itaondoa udanganyifu wanaoambiwa na wake zao.

Katika hatua nyingine mkazi wa Kilago, Magdalena Charles alisema tatizo la watoto kuwa na udumavu linachangiwa na wazazi kuwatelekeza ambapo malezi hufanywa na mabibi ambapo wengi hawana uwezo wa kiuchumi kuwatunza, hali ambayo inachangia ukosefu wa lishe bora na watoto hudumaa.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika kwa ushirikiano wa Serikali na shirika lisilo la kiserikali la World Vision mwaka 2015/2016, ulibaini hali ya udumavu mkoani Shinyanga ni watoto 28 kati ya 100 uliosababishwa na upungufu wa damu kwa wazazi wakati wa ujauzito.

Meneja mradi wa uboreshaji huduma za lishe kwa mama na mtoto wa Shirika la Enrich mkoani Shinyanga, Mwivano Malimbwi alisema tayari wametoa vifaa vya vipimo vya kugundua matatizo hayo vyenye thamani ya Sh113 milioni.

Mradi huo unaoratibiwa na World Vision katika halmashauri za Kahama Mji, Kishapu na Shinyanga Vijijini. 


Mwivano alisema utafiti ulibaini watoto 71 kati ya 100 wana upungufu wa damu na pia wajawazito 59 kati ya 100 wana upungufu huo.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: