BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CHANGAMOTO ZA RUFAA KWA WAJAWAZITO VYADAIWA CHANZO CHA VIFO VYA MAMA NA MTOTO MOROGORO

Mganga Mfawidhi Zahanati ya Mngazi, Dk Fredrick Mbalai akizungumza jambo na mwandishi wa habari, Christina Haule katika kijiji cha Mngazi halmashauri ya wilaya ya Morogoro.Picha na Juma Mtanda.

Na Juma Mtanda, Morogoro.
Wakati serikali ikiweka mikakati ya kupambana na vifo vinavyotokana na uzazi nchini, baadhi ya vifo vidaiwa kuchangiwa na miundombinu mibovu inayopelekea akinamama wajawazito hasa wakati wa kujifungua kupoteza maisha kwa watoto au mzazi hasa maeneo ya vijijini ambako kumekuwa na kila aina ya changamoto tofauti na mijini.

Takwimu za ongezeko la vifo vya uzazi kwa kipindi cha mwaka 2012-2013 ni vifo 432 huku mwaka 2016-2017 vikitokea vifo 556 ikiwa ni sawa na akinamama 900 wanaopoteza maisha kila mwezi wakati wa kujifungua hapa nchini.

Hivi karibuni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa anapokea mashine ya kisasa ya kutoa dawa ya usingizi wakati wa upasuaji alibainisha hali hiyo na kueleza kuwa serikali imeweka malengo ya kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka 109 hadi 279 ifikapo mwezi Juni mwaka mwaka huu.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mngazi halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Shabaan Kimwaga anaeleza kuwa kumekuwa na vifo vinavyotokana na uzazi hasa kwa wajawazzito wanaopewa rufaa kwenda kujifungua kituo cha afya Duthumi.

Kimwaga anaeleza kuwa vifo hivyo vya akinamama wajawazito au watoto kufa baada ya kujifungua vinasabishwa na mama mjamzito kupandishwa kwenye pikipiki, miundombinu mibovu ya barabara na kukosekana kwa magari ya kubebea wagonjwa.

“Vifo vinavyotokana na uzazi kijiji cha Mngazi au kata hii ya Mngazi vimekuwa vikitokea kwa nyakati tofauti kwa akinamama wajawazito au mtoto vinatokana na kupanda pikipiki na wamekuwa wakitembea umbali mrefu baada ya kupewa rufaa kutoka Zahanati ya Mngazi kwenda kituo cha Duthumi lakini wanapofika huko baadhi wamekuwa wakipoteza maisha aidha iwe mtoto au mama.”alieleza Kimwaga.

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Mtandao wa kijinsia Tanzania (TGNP) imeendesha kampeni ya uraghbishi katika mikoa mbalimbali nchini ikilenga kuibua changamoto, kutambua na kuchambua changamoto za kijinsia na namna zinavyoathiri uwezo wa wanawake walio pembezoni kumiliki rasilimali na inavyominya haki yao ya kiuchumi.

Halmashauri ya wilaya ya Morogoro ni miongoni mwa baadhi za wilaya zenye changamoto kubwa kwa huduma bora za afya ikiwemo mama mjamzito na kupelekea baadhi ya wanawake kukosa watoto na wengine kufariki dunia wakati wa uzazi.

Februari 14 mwaka 2015 nilishika ujauzito na wakati wa kujifungua nilienda Zahanati ya Mngazi halmashauri ya wilaya ya Morogoro Vijijini lakini ilishindikana kujifungua kutokana na mganga kunieleza kuwa nina mtoto mkubwa na wao hawana vifaa hivyo siwezi kujifungua katika Zahanati hiyo na kupewa rufaa kwenda kituo cha afya Duthumi.alianza kueleza Albina Maonya (23) mkazi wa Sesenga kata ya Mngazi.

Wanawake wakazi wa kijiji cha Sesenga kata ya Mngazi halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Albina Maonya kulia na Anastazia Simon moja wa wanawake waliokumbwa na mikasa hiyo.Picha na Juma Mtanda.

ALBINA ANASIMULIA.
Albina alieleza kuwa baada ya kufika Duthumi aliweza kujifungua kwa msaada wa mganga lakini kichanga chake kilipoteza maisha kutokana na misukosuko mbalimbali.

“Nilijifungua mtoto lakini alikufa muda mfupi baada ya kujifungua na nilielezwa sababu za kifo chake kuwa alichoka, nilisikitika na kupatwa na uchungu mkubwa kumkosa mtoto lakini nilimshukuru mwenyezi mungu na kurudi nyumbani na mikono mitupu.” alisema Albina.

Albina alieleza kuwa mtoto huyo huenda asingekufa endapo angesafirishwa kwa gari maalumu la kubebea wagonjwa kutoka zahanati ya Mngazi kwenda Duthumi na kutaja usafiri wa pikipiki ndio umechangia kifo cha mtoto wake.

“Hebu fikiria mama mjamzito anayetarajia kujifungua muda wowote alafu anapewa rufaa kwenda kituo kingine cha afya tena anatembea kwa umbali wa zaidi ya kilometa 25 alafu anapanda usafiri wa pikipiki nini kitatokea kwa mama mjamzito mwenyewe au mtoto mwenyewe aliye kwenye mlango wa uzazi?...alihoji Albina.

Ni jambo linalonikumbusha uchungu na huzuni kubwa kwangu na familia yangu.aliongeza Bina.

Albina alisema kuwa wakati yupo Zahanati ya Mngazi mtoto tayari alikuwa mlango wa uzazi na kupewa rufaa kwenda kituo cha afya Duthumi akisafiri na pikipiki kwa takribani dakika 45 mpaka saa moja.

Albina alieleza kuwa baada ya kujifungua kwa usaidizi wa mganga alizimia na kupata adha ya majibu mabovu kutoka kwa nesi aliyempokea Duthumi na kupata shida, karaha na maumivu makali muda wote akiwa kwenye usafiri wa pikipiki na mwili kuchoka.

“Mama mjamzito usafiri wa pikipiki si usafiri salama kwake lakini tunalazimika kuutumia kutokana na kutokuwepo magari ya kubeba wagonjwa pale dharura inapotokea lakini hasara zake zitaonekana muda si mrefu.”alisema Albina.

Endapo serikali itaondoa changamoto ya upatikanaji wa magari ya wagonjwa kwa uhakika, kupeleka vifaa kwa vingi katika Zahanati, vituo vya afya vijijini na kutengeneza miundombinu ya barabara…itasaidia akinamama wajawazito kujifungua salama na itaepusha vifo vinavyotokana na uzazi kwa mama na mtoto.

Suala la vifo vya mama wajawazito na watoto tayari limejitokeza kwa akinamama watano katika kata ya Mngazi pekee katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro Vijijini ikiwa wajawazito wawili kufariki dunia na watatu wakijifungua na kupoteza maisha.

Hali ya vifo hivyo ilielezwa wakati wa kuibua kero na changamoto ya afya na wanajamii katika uraghbishi wa siku 14 uliofanyika kwenye ofisi ya kata ya Mngazi mkoani Morogoro mwezi Machi mwaka 2018.

Mganga mfawidhi Zahanati ya kata ya Mngazi Morogoro Vijijini, Dk Fredrick Mbalai alisema kuwa akinamama wote wenye mimba za kwanza ndio wanaopewa rufaa kwenda kujifungulia kituo cha Duthumi, akinamama wenye umri chini ya miaka 20 na akinamama wote wenye mimba ya nne na kuendelea.

Dk Mbalai alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu za kadi za kliniki, akinamama wajawazito waliogundulika kuwa na mtoto ana mlalo mking’amo tumboni na akinamama wenye watoto wakubwa hawawezi kuruhusiwa kujifungua katika zahanati hivyo ni lazima wapewe rufaa kwenda kituo cha afya kwa usalama zaidi.

“Zahanati yetu ya Mngazi tumekuwa tukitoa rufaa kwa akinamama wajawazito kwenda kujifungua kituo cha afya Duthumi baada ya kugundua kuwa mama mjamzito ana mtoto mkubwa au ana mlalo mking’amo tumboni hao wote ni lazima wapewe rufaa.”alisema Dk Mbalai.

Dk Mbalai anasema kuwa taarifa za uwepo wa vifo vya mama mjamzito na watoto waliozaliwa muda mfupi baada ya kujifungua wakitokea Zahanati ya Mngazi baada ya kupewa rufaa kwenda Duthumi na yeye kama mganga mfawidhi bado hajapokea mrejesho wa taarifa ya kifo aidha kwa mtoto au mama mwenyewe kutoka kwenye kituo hicho cha afya.

“Suala la mama mjamzito kupoteza maisha ni suala zito na akinamama wote waliopewa rufaa kwenda kituo cha afya Duthumi kujifungua Zahanati ya Mngazi haijapata wala kupokea taarifa zozote za vifo vya akinamama wajawazito maana suala hilo mpaka wizara wanapaswa kujua.”alisema Dk Mbalai.

Dk Mbalai alisema kuwa Zahanati ya Mngazi inapokea wagonjwa 749 hadi wagonjwa 800 kwa mwezi na inahudumia vijiji vinne vinavyounda kata ya Mngazi na vijiji vya jirani.

“Suluhisho la kuwapunguzia adha ya akinamama wajawazito rufaa ya kwenda kituo cha afya Duthumi itakuwa pale itakapokamilika ujenzi wa kituo cha afya Mngazi na itasaidia kupunguza changamoto nyingi tofauti na hivi sasa.”alisema Dk Mbalai.

Said Athman Matumla mkazi wa Mngazi zanahati ya Mngazi ina wahudumu wachache na nilipoteza mjukumu wangu, Anti Mohamed kwa kufariki dunia kwa kifafa cha mimba baada ya kupewa rufaa kwenda hospitali ya mkoa wa Morogoro.

“Mjukuu wangu, Anti Mohamed amekufa akiwa amepatwa na kifafa cha mimba na kifo hicho kilimkuta ndani ya lori wakati tunamsafirisha kwenda Morogoro mjini kujifungua baada ya zahanati ya Mngazi kutupatia rufaa kutokana na mganga kuona hakuna njia ya kumsaidia ajifungulie pale.”alisema Matumla.

Matumla alisema kuwa anaamini mjukuu wake alipoteza maisha mwaka 2013 kutokana na kukosa huduma sahihi na miundombinu mibovu ya barabara imechangia na kukosekana kwa magari ya wagonja.

“Tangu lini wajawazito tena waliopewa rufaa wanaokwenda kituo cha afya au hospitali ya rufaa wakapanda lori au pikipiki wakitokea katika zahanati ?...alihoji Matumla.

Matumla aliongeza kwa kusema kuwa anavyofahamu yeye mjazito aliyepewa rufaa anapaswa kupanda gari la wagonjwa lenye kila aina vifaa vya huduma za dharura ili hali inapobadilika aweze kusaidiwa lakini wagonjwa hao wajawazito ni jambo la kawaida maeneo ya vijijini kupanda pikipiki, lori na baiskeli kutokana na kukosa huduma za magari ya wagonjwa na matokeo yake watapoteza maisha aidha mtoto au mama mwenyewe.

Baadhi ya manesi kwenye zahanati, vituo vya afya hata hospitali hawana lugha nzuri kwa akinamama wajawazito pindi wanapoenda kujifungua na mimi binafsi nimefikia maamuzi ya kutokwenda tena zahanati au kituo cha afya endapo nitapata ujauzito kujifungua huko maana nikikumbuka kero ya maneno ninaona bora nijifungulie nyumbani tu.alieleza Anastazia Simon (34).

Anastazia anasema kuwa Desemba 18 Mwaka 2017 alishikwa na uchungu wa kujifungua na alipofika zahanati ya Mngazi alipewa rufaa kwenda kituo cha afya Duthumi alipokelewa kwa kejeli na mmoja wa manesi siku hiyo na kudai kushindwa kumsaidia mpaka alipopita mganga na kumsaidia kujifungua kichanga ambaye dakika chake alikufa.

“Baada ya kujifungua mtoto muda mfupi tu alikufa na nilieleza na mganga kuwa mtoto alichoka sana lakini hebu fikiria mama mjamzito anapanda kwenye bodaboda na kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 14 tena kwenye barabara mbovu mama mjamzito na mtoto aliye kwenye mlango wa uzazi atashindwa kuchoka?..alihoji Anastazia.

Akizungumza wakati wa uraghbishi na kuibua changamoto na kero upande wa afya katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Zaituni Mgombwela (53) alisema kuwa vifo vya vinavyotokana na uzazi vinachangiwa na miundomini mibovu ya barabara.

“Kwa miaka tofauti baadhi ya akinamama wamepoteza maisha na wengine watoto wakati wakisafirishwa kwenda kujifungua kituo cha afya Duthumi baada ya kupewa rufaa kutoka kwenye zahanati mbalimbali.”alisema Zaituni.

Zaituni alisema kwenye uraghbishi huo uliofanyika ofisi ya kata Mngazi kwa siku 12 mwaka huu aliwataha akinamama waliopoteza maisha kutokana na tatizo la uzazi kuwa, Albina Adrian Maonya, Anastazia Chasambi wakazi wa Sesenga na Sikujua Mohamed mkazi wa Ngazi.

“Wajawazito wapo waliopoteza maisha wakiwa wajawazito akiwemo, Christina Pascal mkazi wa Mngazi B kitongoji Bane, Mwajuma Uttoh wa Vigolegole na wengine walipoteza watoto kutokana na adha ya miundombinu mibovu ya barabara kwa nyakati tofauti kutokana na changamoto za uzazi halmashauri ya wilaya ya Morogoro.”alisema Zainabu.

Kwa upande wa Kaimu mganga mkuu halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Dk Elizabeth Omingo amesema kuwa halmashauri hiyo, ina upungufu wa watumishi katika kada ya afya 618 na ina watumishi 327 tu ambao hawawezi kukidhi kuhudumia vituo 60 vya afya vya serikali.

Dk Elizabeth amesema kuwa bado halmashauri hiyo ina changamoto nyingi upande wa idara hiyo na mpaka sasa kuna vituo vingi vya afya vimekaa havijaanza kutumika kutokana na ukosefu wa watumishi.

“Ni kweli kuna changamoto nyingi upande wa idara ya afya katika halmashauri yetu na mpaka sasa bado tuna upungufu wa watumishi wa afya wengi na waliopo 327 hawawezi kukidhi kutoa huduma katika vituo 60 vya afya vya serikali.”alisema Dk Elizabeth.

Dk Elizabeth amesema kuwa zipo baadhi za changamoto zinaweza kuepukika kama akinamama wajawazito kuepukana na vifo vinavyotokana na uzazi akiwemo mama na mtoto.

“Kadi ya kliniki ndio ramani yetu kubwa na inampa mwanga mganga kujua mama mjamzito anaweza kujifungulia zahanati au kituo cha afya na kama ataona viashiria visivyofaa atamweleza mama mjamzito kwenda mapema kituo cha afya au hospitali ili aweze kujifungua salama huko kuliko kwenye zahanati.”alisema Dk Elizaeth.

Dk Elizaeth amesema kuwa suala la mama mjamzito kufariki duniani kutokana na uzazi ni jambo nyeti na linachukuliwa kwa uzito mkubwa na linapotokea ni lazima kujua chanzo cha kifo ili kupatia ufumbuzi ndio maana mganga mfawidhi katika zahanati au kituo cha afya anachukua hatua mapema kuepusha matatizo yanayoweza kutokea.

Dk Elizabeth amesema kuwa vifo vinavyotokana na uzazi kwa akinamama wanaopewa rufaa kutoka zahanati ya Mngazi kwenda kituo cha afya Duthum ni jambo la kufuatilia ili kujua ukweli wake.

Halmashauri ya wilaya ya Morogoro ina magari ya kubebea wagonjwa matatu huku baadhi za changamoto nyingine kwa baadhi ya zahanati au vituo vya afya, akinamama wajawazito wamekuwa wakidaiwa kwenda na maji wakati wa kujifungua.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: