BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MADAWA YA KULEVYA YAWATIBULIA AJIRA MABAHARIA 800 KUTOKA ZANZIBAR

Mabaharia wakiwa na viongozi wao wa kampuni ya Mabaharia ya danaos visiwani Zanzibar mara baada ya kumaliza mafunzo ya kupinga vitendo vya mabaharia kujihusisha na usafirisha na matumizi ya dawa za kulevya, mafunzo hayo yalifanyika juzi katika Chuo cha Mabaharia Chukwaji Mjini Unguja, Picha na Haji Mtumwa.


Zanzibar. Zaidi ya mabaharia 800 kutoka Zanzibar waliokuwa wakifanya kazi katika meli mbalimbali nje ya Tanzania, wamesimamishwa wakihusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya katika meli hizo.

Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na mkurugenzi wa kampuni ya ubaharia ya Danaos, Ali Mzee Yussuf.

Yussuf aliyasema hayo wakati wa mafunzo maalumu yaliyowashirikisha mabaharia mbalimbali visiwani hapa yenye lengo la kupiga vita matumizi na kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Alisema awali mabaharia kutoka katika kampuni hiyo walikuwa zaidi ya 1,000 lakini kwa sasa wamebaki 200 baada ya wengi wao kukamatwa kwa madai ya matumizi na kusafirisha dawa za kulevya.

“Hali hii imekuja baada ya wamiliki wa kampuni za meli husika kuona kuwa mabaharia wetu mara kwa mara hukamatwa kwa kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya, hivyo wakaona ni bora kupunguza idadi kutoka kwetu ili kuzinusuru meli zao kuingia katika matata ya usafirishaji dawa hizo,” alisema Yussuf.

Alisema ni ukweli usiopingika kuwa kuna baadhi ya mabaharia kutoka kampuni yao wamekuwa wakikamatwa na dawa za kulevya kutokana na tamaa zao binafsi, lakini kampuni haihusiki.

Mkurugenzi huyo alisema kutokana na hali hiyo wamedhamiria kutoa mafunzo kwa baadhi ya mabaharia wa Zanzibar, ili kuwaonyesha hasara watakazozipata wakikamatwa na dawa hizo.

“Kwa sasa kupitia chuo chetu cha ubaharia Zanzibar, tumeweka utaratibu maalumu kwa mabaharia wote kutoka hapa lazima wapatiwe elimu ya athari za dawa za kulevya. Mbali na hilo tutafanya uchunguzi maalumu juu yake ili kuona tabia zake kama zinafaa kuwa naye au la, lengo ni kuona kampuni yetu inazidi kupata sifa duniani,” alisema Yussuf.

Naye ofisa wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA), Khamis Mohamed Ali alisema kitendo cha mabaharia kujihusisha na usafirishaji dawa za kulevya katika meli hakikubaliki kwa mujibu wa taratibu za kazi.

Ali alisema kitendo hicho kinaitia aibu kubwa nchi kwa kuonekana inajihusisha na vitendo hatari vya dawa za kulevya.

Alisema wao kama Serikali mara nyingi wamekuwa wakifanya kazi na kampuni hiyo lengo ni kuona wanatekeleza majukumu yao vizuri, ila ni jambo la kushangaza baadhi yao wamekuwa wakijihusiha na usafirishaji wa dawa za kulevya.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: