BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAMA MZAZI WA MBUNGE WA MBEYA MJINI "SUGU" AMZUIA MWANAYE ASIENDE BUNGENI DODOMA


Dar es Salaam. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) Joseph Mbilinyi  maarufu Sugu ambaye tangu jana yupo uraiani baada ya kutoka gerezani kwa msamaha wa Rais John Magufuli, amesema ataanza kushiriki vikao vya Bunge la bajeti mjini Dodoma baada ya kujua maendeleo ya afya ya mama yake mzazi.
“Nasubiri ripoti ya daktari kuhusu hali ya mama ndipo niweze kwenda bungeni.  Ripoti hiyo huenda ikatolewa Jumapili (keshokutwa),” amesema Sugu ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha miezi mitano jela pamoja na na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga
Bunge la bajeti lilianza Aprili 3, 2018 na linatarajiwa kumalizika Juni 30, 
Sugu na Masonga walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela Februari 26 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara walioufanya Desemba 30 mwaka jana eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.
Wawili hao wameshatumikia adhabu hiyo kwa siku 73 ikiwa ni zaidi ya robo ya kifungo chao.

Sugu alivyotolewa jela ‘kininja’ Gereza Kuu la Ruanda.

Ilikuwa kama sinema namna mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na katibu wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga walivyotolewa gerezani ‘kininja’.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyewaongoza viongozi wa chama hicho katika Gereza Kuu la Ruanda jijini Mbeya kuwapokea, waliachwa njia panda jana asubuhi.

Viongozi hao kwa nyakati tofauti kuanzia jana saa 12:10 asubuhi walifika na kuingia katika lango kuu la gereza hilo, na ilipofika saa 12:30 wafuasi wa Chadema waliendelea kumiminika.

Askari Magereza waliokuwa nje ya gereza walilazimika kuwatoa nje ya jambo lililozua msuguano. Hata hivyo, viongozi hao wakiongozwa na Mbowe walitii amri hiyo hivyo kuegesha magari yao nje ya lango.

Mbowe alibaki ndani ya gari akiwa na mke wa Sugu, Happines Masonga.

Saa 12:45 asubuhi, magari mawili ya polisi yalifika eneo la gereza yakiwa na askari wenye sare na waliovaa kiraia, baadhi wakiwa na silaha za moto ili kuimarisha ulinzi.

Magari ya jeshi hilo yaliongezeka na kufikia matano huku lile la maji ya kuwasha likiranda eneo hilo.

Wakati magari ya polisi yakiingia na kutoka gerezani, gari la mkuu wa magereza Mkoa wa Mbeya liliingia ndani na kuegeshwa jirani na mlango mkuu wa gereza na wakati wote huo, nje ya lango kuu, askari walikuwa wakiendelea kuwaondoa watu na magari yaliyokuwa yameegeshwa.

Wakati hilo likifanyika, gari la mkuu wa Magereza na lingine aina ya Pick-up la gereza hilo yalitoka kwa mwendo wa kasi pasipo yeyote kujua kuwa Sugu na Masonga walikuwamo ndani ya gari la mkuu huyo wa Magereza.

Ilipotimu saa 1:40 asubuhi, Sugu alimpigia simu mkewe akimweleza kuwa wapo eneo la Mama John wakielekea nyumbani na kwamba, wapo kwenye gari la mkuu wa gereza.

Kabla ya simu hiyo, Mbowe alizungumza na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO) ambaye alimweleza kwamba Sugu na Masonga wameshapelekwa nyumbani.

Mbowe alipokuwa akiwaeleza wafuasi wa Chadema kuhusu hilo, mkewe Sugu akamwambia Mbowe kwamba amepigiwa simu na mumewe kwa kutumia simu ya askari akimweleza wapo njiani wanaelekea nyumbani.

Wakati wafuasi hao wakiwa wamepigwa butwaa, askari waliokuwa wametanda eneo hilo waliingia kwenye magari na kuondoka.

Mke wa Sugu na wa Masonga, Grace Malya ndio waliokuwa wa kwanza kufika nyumbani kwa Sugu ambako walikuta wawili hao wakifunguliwa geti na mlinzi wakiwa wamebeba nguo zao kwenye mifuko ya rambo, huku gari lililowapeleka likiwa limeondoka.

Baadaye Mbowe na viongozi wengine wa Chadema walifika nyumbani kwa Sugu na kuanzia hapo shangwe zilitawala eneo hilo.

Sugu aliwaeleza kuwa gari la mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya likiwa na askari ndilo liliwapeleka nyumbani.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Paul Kijida akizungumza na waandishi wa habari alisema kilichofanyika ni utaratibu tu kwa kuwa mfungwa anapomaliza kifungo, magereza ndio wenye wajibu wa kumrudisha nyumbani kwao kwa kumpatia nauli, lakini kwa Sugu na Masonga waliona ni jirani ndiyo maana akaamua kuwapeleka kwa gari lake.

Baadaye msafara wa kina Sugu ulikwenda ofisi za kanda za Chadema zilizopo Kadeghe kuonana na wafuasi wa chama hicho waliokuwa wamekusanyika.Mwananchi

Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: