Sumbawanga. Mtendaji wa Kata ya Mwandui iliyopo katika mwambao wa Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, Benedict Chapewa ameuawa kwa kupigwa risasi wakati akinywa pombe kwenye baa anayoimiliki. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema jana kwamba watu wasiojulikana walimvamia mtendaji huyo usiku wa kuamkia jana katika baada hiyo na kutekeleza mauaji hayo.
Kamanda Kyando alisema, Chapewa alivamiwa na kundi hilo kijijini hapo na kushambuliwa kwa risasi na kwamba wauaji hao walitumia bunduki aina ya gobore.
“Watu hao walimmiminia risasi kisha kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake,” alisema.
Kamanda huyo alisema baada ya wauaji kutekeleza lengo lao waliondoka kuelekea kusikojulikana na hawakuchukua kitu chochote kutoka kwa mtendaji huyo au katika baa.
Kamanda Kyando alisema uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo unaendelea na kazi ya kuwasaka watuhumiwa imeanza ili wakamatwe na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.
Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kufanya mauaji dhidi ya wenzao. “Vyombo vya dola vitahakikisha vinawachukulia hatua za kisheria wale wote wanaojichukulia sheria mkononi,” alisema.Mwananchi

0 comments:
Post a Comment