Mbeya. Nje ya Gereza Kuu la Ruanda, kuna umati mkubwa wa watu.
Viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe
wanasubiri kwa hamu kubwa.
Fununu za kuachiwa kwa mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ zimeenea kila mahali. Polisi
wamejipanga maeneo yote ya gerezani kulinda usalama.
Viongozi wa
Chadema wanaonekana wakizungumza kwa simu, wengine wakiwa katika
vikundi vikundi wakijitahidi kuvuta muda kusubiri jambo moja tu,
kuachiwa kwa Sugu.
Hata hivyo, umati huo pamoja na Mbowe
wanapigwa chenga ya mwili wanapoambiwa kuwa Sugu na mwenzake Katibu wa
Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga wameshaondoka gerezani hapo
tangu saa moja na nusu asubuhi na tayari wamefika nyumbani.
Hizo
zote ni mbwembwe, lakini ukweli unabaki kuwa Mei 10, mwaka huu, itabaki
kuwa kumbukumbu Sugu aliyeachiwa huru kutoka gerezani alikokuwa
akitumikia kifungo cha miezi mitano alichohukumiwa baada ya kukutwa na
kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Sugu
alitolewa gerezani kwa msamaha wa Rais alioutoa Aprili 26, mwaka huu
baada ya kukidhi vigezo vya msamaha huo sawa na wafungwa wengine zaidi
ya 3,000 waliopunguziwa robo ya vifungo vyao.
Mpaka wakati
anatolewa gerezani, Sugu alikuwa tayari ameishi siku 73 katika Gereza
Kuu la Ruanda ambako alifungwa tangu Februari 26.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Sugu anasema maisha aliyoishi ndani ya gereza hilo si mazuri hata kidogo.
Sugu
anasema gereza hilo lilijengwa tangu enzi za ukoloni likiwa na uwezo wa
kuhudumia wafungwa kati ya 400 na 450 kwa wakati mmoja.
Sugu
ambaye pia ni msanii wa muziki anasema kwa sasa gereza hilo lina
wafungwa na mahabusu zaidi ya 1,400 ambao wanahudumiwa na gereza hilo
kwa wakati mmoja.
Anasema kutokana na idadi kubwa ya wafungwa na
mahabusu waliopo ndani ya gereza hilo, maisha ya wafungwa na askari wa
gereza hilo ni magumu kuliko watu wengi wanavyofikiria wakiwa nje ya
gereza.
Azungumzia malazi
Sugu anasema katika gereza
hilo, kila chumba kimekusudiwa kulala wafungwa kati ya 21 hadi 26,
lakini chumba hicho hicho kwa sasa wanalala wafungwa kati ya 80 hadi 100
hali ambayo inasababisha walale wakiwa wamerundikana kiasi kwamba
hakuna hata njia ya kupita wakati mfungwa anapohitaji kwenda chooni
kujisaidia.
Anasema gereza hilo pia lina uhaba mkubwa wa
magodoro, hali ambayo inasababisha godoro moja dogo lenye upana wa futi
mbili na nusu kulaliwa na watu wanne.
“Katika godoro la futi
mbili na nusu tulikuwa tunalala watu wanne, tulikuwa tunalazimika kulala
mtindo wa mchongoma yaani wawili wanalala wakiwa wameelekeza vichwa
upande mmoja na wengine wawili wanaelekeza vichwa upande mwingine.
Mtindo
huu wa kulala baadhi ya watu wanauita ‘mzungu wanne’ na mimi kwa
kipindi chote cha miezi mitatu nilichokaa gerezani nilikuwa nalala
mzungu wanne kama wengine,” anasimulia Sugu.
Anasema kutokana na
hali duni ya malazi ya wafungwa ni rahisi kuambukizana maradhi hasa
yanayoambukiza kupitia mfumo wa hewa kama kikohozi na kifua kikuu.
Chakula cha ubabe
Sugu
anasema hali ya chakula kwa wafungwa ndani ya gereza hilo pia si nzuri,
kwani wafungwa wanakula mlo mmoja tu kwa siku licha ya Serikali kusema
inawatengea fedha za kutosha watu walio gerezani.
Anasema
kulingana na tabia za gerezani, watu wengi hawawezi kula na kushiba
kwani chakula kinagawiwa na kuliwa kwa ubabe mwingi ambapo wenye nguvu
au madaraka ndani ya gereza ndio wenye uhakika wa kula chakula na
kushiba.
“Wafungwa waliopewa cheo cha unyampala ndio wanaoweza
kupata chakula cha kutosheleza matumbo yao, wengine huishia kula kwa
kunyang’anyana na mwenye nguvu ndiye anayekula, kwa kifupi mle ndani
utemi tu bila utemi mzee hupati chakula,” anasema Sugu.
Mavazi kwa wafungwa
Kwa
mujibu wa Sugu, hali ya mavazi kwa wafungwa gerezani hapo si ya
kuridhisha kwani licha ya Serikali kuamua wafungwa wote wavae sare zenye
rangi ya njano, upatikanaji wake umekuwa ni mgumu hivyo kushindwa
kukidhi mahitaji ya wafungwa.
Sugu anasema katika kundi la
wafungwa wanaokadiriwa 800 ni wafungwa kama 200 tu ambao wanapata mavazi
rasmi ya wafungwa kwa maana ya sare za rangi ya njano na wanaosalia
takribani 600 wanalazimika kuvaa nguo zao za nyumbani.
Anasema
ikitokea nguo za mfungwa zimechakaa, atalazimika kuzitumia hizo hizo na
kuteseka kwa baridi kali hadi mwisho wa kifungo chake au labda itokee
mfungwa mwenye mavazi rasmi amemaliza kifungo na kuvua nguo zake ndipo
mwingine hupewa.
Akataa sare zilizotumika
Sugu
anasema wakati yeye na mwenzake Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa,
Emmanuel Masonga wanaingia gerezani hapo walikaa takribani wiki moja
bila kuwa na sare, lakini aliambiwa kwamba kuna agizo kutoka ‘juu’
kwamba lazima wavae sare.
“Nilishangaa pale nilipopata taarifa
kwamba kuna agizo kutoka juu likidai Sugu lazima avae sare. Lakini
ukiangalia mle ndani kuna wafungwa wana zaidi ya miaka 10 hawana sare
kwa sababu Serikali haijawashonea.
“Kwa sababu ya Sugu na
Masonga tu zilitafutwa sare za zamani ambazo zilitumika wakatuletea ili
tuvae….. tulizikataa na walipoona vile mzee unaambiwa walihaha
kututafutia nyingine… wakatushonea mpya.
“Na nilishangaa kusikia
hilo ni agizo toka juu… maana sikuona ajabu mfungwa Sugu kuvaa sare.
Eti walitaka kumfedhehesha Sugu kisaikolojia. Kwangu niliona poa tu
kwanza walinipunguzia kuvaa nguo za nyumbani na kuanza kufuafua mara kwa
mara,” anasema Sugu.
Usikose kusoma mfululizo wa maisha ya Sugu gerezani kesho katika gazeti la Mwananchi.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
siasa /
slider
/ SUGU AELEZA NAMNA ALIVYOKUWA AKILALA MZUNGU WA NNE GEREZA KUU LA RUANDA MBEYA
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment