BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WANAWAKE WANAVYOWEZA KULINDA MATITI YAO HUKU WAKIWATESA WATOTO 7.6 MILIONI KULINDA SHEPU


Hivi unajua kuwa maziwa ya mama ni muhimu kwa afya na makuzi ya mtoto katika miezi sita ya kwanza?

Ukweli ni kwamba kila mama anasimulizi yake ya namna anavyomnyonyesha au kutomnyonyesha mwanawe.

Wapo wanaokacha kuwanyonyesha watoto wao wakihofia kuharibu maumbile ya matiti yao lakini wengine wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya maradhi au kutingwa na kazi hasa za kujiongezea kipato.

Utafiti mpya wa Shirika la Afya Duniani (Unicef) unaonyesha takribani watoto 7.6 milioni duniani hawanyonyeshwi kila mwaka.

Utafiti huo unaonyesha idadi ya watoto wasio nyonyeshwa na mama zao ni kubwa zaidi katika mataifa yaliyoendelea ikilinganishwa na yale maskini.

Asilimia nne ya watoto kwenye nchi maskini hawanyonyeshwi kabisa maziwa ya mama wakati katika nchi zilizo endelea ni asilimia 22.

Viwango vya unyonyeshaji vilivyofanyiwa tathimini mwaka jana na Unicef kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika nchi 194 ilibaini asilimia 40 tu ya watoto walio chini ya miezi sita wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee.

Pia, ni nchi 23 pekee duniani ndizo zenye kiwango cha unyonyeshaji wa zaidi ya asimilia 60.

Ofisa Mawasiliano wa Unicef Tanzania, Usia Nkoma anasema wametoa utafiti huo na kutoa matokeo yake mwezi huu kuikumbusha dunia umuhimu wa kunyonyesha watoto.

“Kila mtoto hai anasherehekea siku ya mama duniani kwa hiyo ni jukumu la akina mama kutimiza wajibu wao wa msingi wa kuwanyonyesha watoto wao kwa sababu maziwa ya mama ndiyo msingi bora wa maisha yake,” anasema.

Nkoma anasema jamii inao wajibu mkubwa wa kuhakikisha mama anapata nafasi ya kumnyonyesha mtoto wake bila wasiwasi wowote.

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliwaonya watumishi wasio toa nafasi kwa akina mama wenye watoto kuwahi kutoka ofisini na kwenda kunyonyesha.

“Serikali ya awamu ya tano, katika kuhakikisha watoto wanakuwa na afya bora imeweka kanuni inayompa nafasi ya saa mbili mama mwenye mtoto wa chini ya miezi sita kumnyonyesha mwanawe,” anasema Ummy.

Simulizi za unyonyeshaji.
Katika jamii wapo kina mama wanaonyonyesha watoto wao kwa miezi sita, mwaka mmoja na wengine miwili.

Lakini pia wapo wasiopenda kabisa kunyonyesha kwa sababu mbalimbali.

“Nilikuwa nabanwa sana na kazi ikabidi nimuanzishie mtoto wangu maziwa ya kopo akiwa na miezi minne, ndiyo muda niliomuachisha,” anasema Anitha Linus (jina la pili sio sahihi).

Anitha anajipa moyo kuwa japo alimuachisha mwanawe katika umri huo alihakikisha anampatia maziwa hayo na mpaka sasa anamiaka miwili.

Adelina Elias anasema mwanawe wa mwezi mmoja hanyonyi baada ya kupata maradhi ya kuvimba matiti.

“Nilijitahidi kutibiwa lakini maumivu makali na uvimbe vimemfanya mwanangu asinyonye na sasa nampatia uji ambao unga wake umechujwa,” anasema Adelina. Anasema kama atatibiwa na kumaliza tatizo hilo, bado uwezekano wa kumnyonyesha tena hautakuwapo tena kwa sababu maziwa yatakuwa yameshakauka.

Wakati kina mama hao wakiyasema hayo, Ofisa Mawasiliano wa Unicef Nkoma anasema sio tu kumfanya mtoto akue ipasavyo, unyonyeshaji unamuwezesha kuwa na upeo mkubwa kiakili jambo ambalo pia ni sifa kwa mama.

Ukweli kuhusu unyonyeshaji

Muuguzi mkongwe wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Aphrosina Kaduma, anakiri kwamba maziwa ya mama ni kinga tosha dhidi ya mtoto.

“Kwa hiyo tunaposherehekea siku ya mama siku zote, ni budi kuwapongeza na kuwashukuru kina mama wanaotekeleza wajibu wao ikiwa ni pamoja na suala zima la unyonyeshaji, usimnyime mwanao haki yake ya msingi,” anasema Nkoma.

Naye Kaduma anasema kihalisia, mtoto mchanga anatabia ya kulala usingizi ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.

“Katika muda huo anapaswa kunyonyeshwa, kwa hiyo mama usione uvivu wala maumivu kumnyonyesha titi lako mtoto baada ya kuzaliwa,” anasema.

Anasema kihalisia mtoto hatakuwa na hamu ya kunyonya ndani ya muda huo hivyo ni jukumu la mama kumshawishi ili anyonye.

“Mama bora anaweza kumshawishi mtoto anyonye, unachotakiwa kufanya ni kumkamulia matone ya maziwa mdomoni na unaweza kutingisha mdomo wake kidogo kwa kutumia chuchu, kwa sababu hakuna kitu kinachomhakikishia mtoto afya njema kama kunyonya,” anasema.

Wataalamu wa afya wanasema maziwa ya mama ni bora kwa mtoto kuliko aina yoyote ile ya maziwa au mchanganyiko wowote wa vyakula vingine.

Mtandao wa Hesperian Health Guides unashauri kuwa ikiwa mama hatakuwa na uwezo wa kunyonyesha mtoto baada ya kujifungua, anapaswa kusaidiwa.

Mtandao huo katika makala yake kuhusu umuhimu wa maziwa ya mama unaandika ‘maziwa ya mwanzo ya mama ni sawa na kimiminika cha dhahabu’.

Kaduma anasema maziwa ya kwanza hunata na huonekana ya njano na ndiyo chakula sahihi katika tumbo la mtoto ambaye ndiye kwanza amezaliwa.

Wataalamu wa tiba lishe wanalizungumziaje hili?

Wataalamu wa lishe kutoka Jukwaa la Lishe Tanzania, wanasisitiza ni lazima mama amnyonyeshe mwanawe bila kumpa chakula chochote ndani ya miezi sita tangu azaliwe.

Mtaalamu wa Lishe na Mratibu wa Miradi wa Jukwaa la Lishe nchini (Panita), Jane Msagati anasema maziwa ya mama kwa siku za kwanza ni dawa muhimu kwa mtoto kuliko kitu chochote kile.


Anashauri mama kupata mlo kamili ili kuendelea kutengeneza maziwa ya mtoto yenye virutubisho vya kutosha kunyonya na kushiba vizuri sambamba na kujenga afya yake.

Faida za unyonyeshaji
Maziwa ya mama ni chakula bora kwa watoto wachanga na wale wakuao.

Muwakilishi Mkazi wa Unicef, Maniza Zaman anasema kiuhalisia unyonyeshaji unaweza kuokoa maisha ya mtoto na kuboresha afya yake.

Anasema unyonyeshaji pia unahusishwa na kufanya vizuri zaidi kwenye vipimo vya upeo wa akili kwa watoto na vijana. 


Kwa mujibu wa mtandao wa Manyanda Health, maziwa ya mama ni salama na husaidia kuwalinda watoto wachanga dhidi ya maradhi ya kawaida ya utoto yakiwamo ya kuhara na pneumonia ambayo ndiyo sababu moja wapo ya vifo vingi vya watoto wachanga duniani. 

Kwa upande wa wanawake, mtandao huo unaonyesha maziwa ya mama ni njia ya uzazi wa mpango na inasemekana kuwa husaidia kwa asilimia 98 kuzuia mimba kwenye miezi sita ya kwanza.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: