ZITTO AHOJI UHALALI WA MKUCHIKA KUKAIMU UWAZIRI MKUU
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amehoji ni kwanini Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi, George Mkuchika akaimu nafasi ya Waziri Mkuu bungeni wakati kanuni za bunge haziruhusu.
Amesema kwa mujibu wa kanuni za bunge, mwenye sifa ya kukaimu nafasi hiyo ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi ambaye ndiye ana muda mrefu bungeni.
“Uwepo wa Mkuchika katika nafasi hiyo umechangiwa na nafasi yake ya udhamini katika Klabu ya Yanga kwa kuwa viongozi wa Yanga wanapenda sana madaraka,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Zitto alitaka Waziri Mkuchika aachie nafasi hiyo kwa kuwa uwepo wake katika nafasi hiyo anakiuka kanuni za bunge.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema Mkuchika alikaimishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati Dk. Mwinyi akiwa na shughuli nyingine nje ya bunge.
“Kutokana na hali hiyo, Mkuchika ataendelea kushika nafasi hiyo hadi Waziri Mkuu atakapofanya mabadiliko mengine,” amesema Jenista.Mtanzania
0 comments:
Post a Comment