BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

GBAGBO CHINI YA ULINZI.

Majeshi ya Ouattara yakipiga doria Abidjan

Aliyekuwa rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo baada ya kukamatwa akiwa chini ya ulinzi.



RAIS aliyekuwa aking’ang’ania madarakani nchini Ivory Coast, Laurent Gbagbo amekamatwa na kukabidhiwa kwa wafuasi wa mshindi wa urais anayetambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa, Alassane Ouattara.

Taarifa zilieleza jana kwamba Gbagbo aliyekuwa amejificha katika handaki baada ya kuzingirwa tangu wiki iliyopita, alikamatwa jana na kikosi maalumu cha majeshi ya Ufaransa.

Msemaji wa Gbagbo, Toussaint Alain pia aliliambia Shirika la Habari la Reuters kutoka Paris kuwa: "Amekamatwa na majeshi maalumu ya Ufaransa nyumbani kwake na amekabidhiwa kwa wapinzani."

Baada ya kukamatwa, alipelekwa kwenye Hoteli ya Golf, yalipo makazi ya Ouattara ambako ndiko anakoendeshea Serikali yake chini ya ulinzi wa askari wa Umoja wa Mataifa (UN) kutia saini waraka maalumu unamlazimu kukabidhi madaraka kwa Ouattara.

Gbagbo amekamatwa baada ya mashambulizi makali ya makombora yaliyofanywa na vikosi vya Ufaransa kwa kushirikiana na vikosi vya kulinda amani vya UN.

Baada ya mashambulizi hayo, magari zaidi ya 30 ya kijeshi yaliingia katika eneo la makazi alimokuwa amejificha katikati mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Abidjan na kuwadhibiti walinzi wake.

“Ndiyo, wamemkamata,” msemaji wa Ouattara, Affoussy Bamba alithibitisha akinukuliwa na Reuters.

Awali, mshauri wa Gbagbo aliyepo mjini Paris, aliiambia Reuters kwamba Gbagbo alikamatwa baada ya vifaru kushambulia makazi alikokuwa amejificha na kuyavunja kwa kutumia makombora.

Inaripotiwa kuwa askari hao walimkamata baada ya vifaru vya Ufaransa kuingia katika makazi yake kwenye na pia mashambulizi ya helikopta za Ufaransa na Umoja wa Mataifa.

Gbagbo alikataa kukabidhi madaraka kwa Ouattara, anayetambuliwa kimataifa kuwa mshindi wa urais nchini humo, katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Novemba 28, mwaka jana.

Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa yanayashutumu majeshi ya Gbagbo kuhatarisha maisha ya raia.

Mmoja wa wapiganaji wanaomuunga mkono Ouattara, Issard Soumharo aliyekuwepo kwenye eneo la mapambano alisema mashambulizi hayo yaliyomtoa Gbagbo kwenye handaki yalianza kwa mashambulio ya ndege na helikopta za kijeshi tangu saa 9.30 alfajiri ya kuamkia jana.

“Tulishambulia na kujaribu kuharibu upande mmoja wa handaki. Alilokuwepo ndani pamoja na mkewe na mwanaye. Hakujeruhiwa ila alionekana kuwa mchovu sana na shavu lake moja lilivimba baada ya kupigwa kibao na mmoja wa askari,” alieleza.

Katika picha za televisheni zilizochukuliwa wakati akikamatwa, alionekana akiwa ndani ya handaki hilo huku akiwa amevaa fulana ya ndani yenye rangi nyeupe, kisha kuvaa shati lenye maua.

Gbagbo ambaye katika uchaguzi huo uliopita alipata asilimia 46 alishatawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 10, kisha kuongeza miaka mitano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Hata baada ya Tume ya Uchaguzi na waangalizi wa kimataifa kutangaza kwamba ameshindwa katika uchaguzi huo alikataa kuondoka madarakani.

Gbagbo ambaye aliwahi kuwa Profesa wa historia alikataa katakata kukabidhi madaraka kwa Ouattara, hivyo wawili hao kulazimika kuongoza serikali mbili ndani ya Ivory Coast.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: