OSAMA BIN LADEN AUWA.
KIONGOZI Mkuu wa Mtandao wa Kigaidi wa al-Qaeda, Osama Bin Laden ambaye amekuwa akisakwa kwa miaka 10 na majeshi ya Marekani na washirika wake, ameuawa katika shambulizi lililochukua dakika 45.Tayari Osama ameshazikwa kwa taratibu zote za dini yake ya Kiislamu karibu na bahari katika eneo ambalo, hata hivyo, halijawekwa wazi.
Shambulizi hilo lilianza baada ya tangazo la muda mfupi la hali ya hatari lililotolewa na askari wa Marekani kabla ya kuanza kuvamia jengo hilo na kuua watu kadhaa kabla ya kumfikia Osama na kumpiga risasi ya kichwa na kufa papo hapo.
Tukio hilo lilitokea usiku wa manane kuamkia jana muda ambao kwa saa za Pakistani ilikuwa ni karibu na alfajiri.
Aliuawa kwenye jengo lililokuwa na ulinzi mkali lijulikanalo kama Abbottabad, Kaskazini-Magharibi mwa Pakistani.
Walioshuhudia tukio hilo walisema shambulizi la kumwua Osama lilianza saa 6:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwa helikopta tatu kuonekana zikiruka katika anga la eneo hilo na kusababisha taharuki kwa wenyeji.
Wakati taharuki hiyo ikiendelea, moja ya helikopta hizo ilitua na mara wakatoka watu wenye vipaza sauti na kuanza kutangaza hali ya hatari kwa wakazi wa eneo hilo.
Katika matangazo hayo, mashushushu hao wa Marekani, walisikika wakiwataka wakazi wa eneo hilo kuzima taa na kutulia kwenye makazi yao.
Muda mfupi baada ya tangazo hilo, ilisikika milio ya risasi iliyoandamana na vishindo vya silaha nzito.
Helikopta hizo zilionekana zikilenga maeneo yanayolizunguka jengo alimokuwa akiishi Osama lenye ghorofa tatu.
Katika shambulizi hilo, inaelezwa kuwa helikopta moja iliangushwa na mabaki yake yalishuhudiwa na wenyeji asubuhi yake.
Haikufahamika mara moja kama ilitunguliwa na walinzi wa Osama au ni makosa ya kikosi hicho cha Marekani na hakuna taarifa yoyote kuhusu kujeruhiwa au kuuawa kwa waliokuwamo.Hata hivyo, Rais Barak Obama alisema hakuna askari wa Marekani aliyekufa katika shambulizi hilo alilolielezea kuwa la mafanikio na kutekeleza haki.
Taarifa zinaeleza kwamba shambulizi hilo lilikuwa linasimamiwa na meli ya kijeshi iliyokuwa eneo la Tarbela Ghazi na kituo kidogo ambacho kiliwekwa kwa dharura kwenye eneo hilo la Abbottabad.Baada ya kufanya mauaji hayo, kikosi hicho maalumu cha wanajeshi wa Marekani kilitoka nje ya jengo hilo kikiwa na maiti ya Osama.
Kikundi hicho pia kiliwaua anayesadikiwa kuwa mke wa Osama pamoja na mtoto wao. Wengine ni mwanamume mmoja ambaye alikutwa ndani ya nyumba ya Osama pamoja na mhudumu mmoja.
Mara baada ya shambulizi hilo, wenyeji wa eneo hilo walidai kuwa walipochungulia kwenye jengo hilo waliona moshi ukifuka.
Jengo alimoishi
Kinyume na watu wengi walivyokuwa wanafikiri kuwa Osama alikuwa anaishi kwenye mahandaki eneo la milimani kwenye mpaka wa Afghanistani na Pakistani ili kukwepa mashambulizi ya Wamarekani, alikuwa akiishi kwenye eneo la kijeshi ambalo lilikuwa na ulinzi wa saa 24 na kila aliyeingia alipekuliwa.Jengo hilo la kifahari la ghorofa tatu, liko umbali wa futi 2,400 kutoka kwenye Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Pakistani. Kituo hicho cha kijeshi kilielezewa kuwa kina hadhi sawa na Chuo cha Kiintelijensia cha Uingereza kijulikanacho kama Sundhurst.
[Nyumba aliyokuwa akiishi Kiongozi wa kundi la Al-Qaeda, Osama Bin Laden na mauti yakamkuta akiwemo humo baada ya kushambuliwa na wanajeshi wa Marekani, usiku wa kuamkia jana mjini Abbottabad, nchini Pakistan. Picha na AFP]
Nyumba aliyokuwa akiishi Kiongozi wa kundi la Al-Qaeda, Osama Bin Laden na mauti yakamkuta akiwemo humo baada ya kushambuliwa na wanajeshi wa Marekani, usiku wa kuamkia jana mjini Abbottabad, nchini Pakistan. Picha na AFP
Eneo hilo linazungukwa na makazi ya watu ingawa wengi walidai hawakujua anayeishi ndani ya jengo hilo.
Umbali wa mahali hapo hadi kufika Mji Mkuu wa Pakistani, Islamabad ni mwendo wa saa moja kwa gari.
Cha kushangaza ni kwamba Osama alikuwa anaishi katika eneo salama ambalo lilikuwa lina ulinzi wa hali ya juu na lilikuwa likilindwa kwa saa 24.
"Ni eneo ambalo linaonekana kuwa na ulinzi wakati wote kutokana na shughuli za kijeshi zinazofanyika na isitoshe kuna kituo cha upekuzi," linaeleza Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliiambia BBC kwamba jengo hilo lilijengwa yapata miaka 10 iliyopita na mwanamume mmoja wa kabila la Kipashtun na hawakujua nani anayeishi humo.
Lakini Shirika jingine la Habari la AP, lilimkariri mmoja wa mashushushu wa Kimarekani akisema jengo hilo lilikuwa limejengwa kwa lengo la kulinda viongozi wa juu wa mtandao wa kigaidi.
Jengo hilo lilikuwa limezungushiwa ukuta unaokadiriwa kuwa na urefu kati ya futi 10 hadi 18 na juu yake kulikuwa na nyaya maalumu za ulinzi kiasi kwamba si rahisi kwa mtu yeyote kuona ndani wala kujua kilichokuwa kinaendelea humo.
Ukuta huo una milango miwili ya kuingilia yenye ulinzi lakini hakuna njia za simu wala mtandao wa mawasiliano ya kompyuta (intaneti), linaeleza AP.
Kikosi maalumu kilichomuua Osama
Imeelezwa kwamba mauaji ya kiongozi huyo wa al-Qaeda ambaye amekuwa akitafutwa kwa muongo mmoja yalifanywa na kikosi maalumu cha askari wa Marekani chenye sifa za kipekee.
Kikosi hicho kinajulikana kama Navy SEAL ambacho kinajumuisha wataalamu waliofunzwa vyema katika masuala ya oparesheni za kivita, wenye uwezo wa kupigana ardhini, angani na baharini. Neno SEAL ni kifupi cha maneno (Sea, Air and Land- yaani Baharini, Angani na Ardhini).
Uwezo mkubwa wa askari wa kikosi hicho kufanya kazi chini ya maji ni sehemu muhimu inayokifanya kiwe tofauti na vikosi vingine duniani
Askari wa kikosi hicho wanaaminika kuwa walifunzwa vizuri na kupata ujuzi katika mbinu mbalimbali za kivita kwa miaka mingi, hivyo kuimarisha uwezo wa kikosi hicho na kukifanya kuwa cha kipekee.
Kikosi hicho kilianzishwa wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia (WWII), mwaka 1942 baada ya Jeshi la Marekani kubaini umuhimu wa kuwa na askari wanaoweza kupigana katika mazingira yote kwa pamoja.
Kila kikosi katika mfumo huo kinajumuisha askari 20 wataalamu wa sanaa ya vita na kimekuwa kikitumika katika matukio mbalimbali, yakiwamo mapambano ya moja kwa moja au operesheni maalumu, ulinzi wa ndani wa mataifa ya nje, kuokoa mateka, kupambana na ugaidi na mipango mingine.
Sifa mojawapo ya wanajeshi wa kikosi cha SEAL ni lazima wawe wanaume wanaotoka katika ama Jeshi la Majini la Marekani au Kikosi Maalumu cha Ulinzi wa Baharini.
Taarifa zilizopatikana jana zilieleza kwamba kikosi hicho ndicho kilichofanikisha shambulizi hilo maalumu la kumwua Osama bin Laden juzi katika eneo la Abbottabad, Pakistani, kilometa 110 kutoka Mji Mkuu wa nchi hiyo, Islamabad.Hata hivyo, akitangaza kuhusu kuuawa kwa Bin Laden, Rais Barack Obama hakutaja moja kwa moja kuhusika kwa kikosi hicho cha SEAL lakini alitumia neno “kikosi kidogo” cha Wamarekani ndicho kilichochukua jukumu la kummaliza Bin Laden.Kikosi hicho kimewahi kuendesha mashambulizi huko Vietnam, Panama, Vita ya Iran na Iraq, Iraq, Afghanistani.
0 comments:
Post a Comment