SKAUTI AKIONYESHA UHODARI WA KUTAMBAA KATIKA KAMBA.
KAMBI ya skauti ya Afrika Mashariki ya Bahati yenye makao yake mkoani Morogoro imeanza mchujo wa kusaka skauti wenye vipaji na ujuzi maalum kutoka katika makundi manne yanayoundwa na shule za sekondari za manispaa ya Morogoro.
Mchujo huo unakusudia kupata kikosi cha skauti 32 watakao fuzu katika majaribio mbalimbali yatakayotolewa katika kambi hiyo kutoka kwa waalimu wa skauti wa ngazi za wilaya na mkoa.
Akizungumza na Mwananchi jana mjini hapa, kamishina wa skauti kanda ya Mashariki, Justine Mateza alisema kuwa tayari vikundi hivyo vinne vyenye jumla ya skauti 58 zimeripoti kambini hapo tayari kwa mchujo huo.
Alisema kuwa katika mchuo huo skauti hao watajaribiwa katika kujibu maswali yatakayoulizwa na wakufunzi wa skauti juu ya mambo ambayo wamejifunza ikiwemo stadi za skauti, mazingira na somo la afya.
Pia watapewa majaribio ya kukabiliana na majanga mbalimbali, kuishi katika mazingira ya asili na namana ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Mateza alisema kuwa lengo la kambi hiyo ni kutaka kupata kikosi cha skauti watakaowakilisha wilaya ya Morogoro katika mambo mbalimbali yanayowahusu skauti ndani ya wilaya, mkoa, taifa na hata nje ya nchi.
Kamishina huyo alitaja shule zilizoshiriki katika mchujo huo kuwa ni Mgulasi, Kigurunyembe, Kihonda na Uluguru ambazo kwa pamoja zimetoa vijana wa skauti 58.
Alisema kuwa baada ya kuteua skauti 32 kutoka katika wilaya hiyo pia kutakuwa na mchujo mwingine wa ngazi ya kiwilaya ambapo wilaya zingine Kilosa, Kilombero, Ulanga, Mvomero na Morogoro Vijijini zitashindanishwa ili kuunda timu ya mkoa.
0 comments:
Post a Comment