MAPIGANO MAKALI YAZUKA NCHINI SOMALIA.
Mapigano makali yamezuka katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, siku moja baada ya shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa(WFP) kupeleka kwa ndege ya msaada wake wa kwanza wa dharura kwa watu walioathiriwa na ukame.
Inaarifiwa takriban watu wanne wameuawa baada ya vikosi vya serikali vikisaidiwa na askari wa Muungano wa Afrika kuwashambulia wapiganaji wa harakati za kiislamu. Mwandishi wa BBC mjini Mogadishu Mohamed Dhore alisema mapigano hayo yametokea katika maeneo ya kaskazini na hayataathiri shughuli za kupeleka misaada.
Maelfu ya watu wamewasili katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali wakitafuta chakula.
Waandishi wa habari wanasema ikiwa vikosi vya serikali vitaweza kuyateka maeneo zaidi, basi mashirika ya misaada yataweza kuyafikia maeneo mengi zaidi yalikumbwa na njaa. Shehena hizi za WFP ndio sehemu ya kwanza ya kupeleka chakula tangu Umoja wa Mataifa uyanadi maeneo mawili ya kusini mwa Somalia kwamba yanakabiliwa na janga la njaa.
Kundi la Al-Shabab, lenye fungamano na al-Qaeda ambalo linadhibiti sehemu nyingi za Somalia, limelipiga marufuku shirika la WFP katika maeneo yake.
Hali ya ukame katika Pembe ya Afrika imesababisha janga la ukosefu wa chakula katika nchi za Kenya, Ethiopia, Djobouti na Somalia. Hali ya hewa katika bahari ya Pacific imesababisha ukosefu mkubwa wa mvua kwa misimu miwili mfululizo na hakuna matumaini ya kunyesha mpaka mwezi wa September.
Takriban watu millioni kumi wameathiriwa na ukame mbaya ambao haujapata kutokea katika kipindi cha miaka 60. Na hali imezidi kuwa mbaya kwa sababu ya mapigano yanayoendelea katika eneo hilo.
0 comments:
Post a Comment