Basi la Super Champion T851 APW likiwa limepinduka baada ya kuacha njia katika eneo la kijiji cha Mkambarani barabara kuu Dar es Salaam-Morogoro ambapo abiria wanne walijeruhiwa na abiria 60 kukwama kwa muda wa masaa 2;30 kabla ya kuondoka katika eneo hilo kuendelea na safari wakati wakisarifi kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma mkoani hapa.
ABIRIA 60 na majeruhi wanne wa basi la Super Champion T 851 APW wamenusurika kufa baada ya basi hilo lililokuwa likitoka jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Dodoma kuacha njia na kupinduka katika kijiji Mkambarani barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro mkoani hapa.
Majeruhi hao wanne walioumia katika ajali hiyo ni Grace Ndalo, Jonathan Hanji mkazi wa Dodoma, Jolam Jonas mkazi wa Mbagala jijiji Dar es Salaam na Ibrahim Keya.
Wakizungumza na gazeti hili eneo la tukio abiria walionusuri kifo katika ajali hiyo walisema kuwa basi hilo liliacha njia na kupinduka baada ya dereva wa basi hilo akijaribu kulipita gari lingine na katika kukwepa kugongana uso kwa uso na gari lililokuwa likitokea mbele yao aliingia kwenye mtaro na kupinduka.
Ibrahim Keya alisema kuwa ajali ingekuwa mbaya sana endapo dereva wa basi la lao la Super Champion angegongana uso kwa uso na gari hilo na kulazimika kuliingiza basi katika mtaro kabla ya kupinduka.
Keya alisema kuwa baada ya kutokea kwa ajili hiyo dereva wa basi hilo alitoweka katika eneo la tukio na kukwama katika eneo hilo kwa muda wa masaa 2:30 bila ya kupatiwa huduma ya kwanza na wahusika baada ya kutokea kwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa 5:15 asubuhi.
“hapa tumepata ajili majira ya saa 5:15 asubuhi hivi lakini mpaka majira hayo (saa 7 mchana ) bado hatujapatiwa msaada wo wote ule wa kukimbizwa hospitalini hivyo hatuelewi tufanye nini kama mimi nimeumia goti na hawa abiria wenzangu watatu” alisema Keya.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Morogoro Ibrahim Mwamakula alisema kuwa basi la Super Champion T 851 APW limeacha njia na kupinduka majira ya saa 5:15 asubuhi katika eneo la Mkambarani barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro mkoani hapa.
Mwamakula akizungumzia juu ya hali ya mareruhi katika ajali hiyo alisema kuwa hana idadi kamili ya majeruhi wa ajali hiyo kutokana na askari waliokuwepo katika eneo la tukio kuwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kukamilisha taratibu za matibabu kwa majeruhi hao.
0 comments:
Post a Comment