WANANCHI DAKAWA WAOMBA JESHI LA POLISI KUCHUNGUZA KUTOWEKA KWA KIJANA ALIYEKUWA AKICHUNGA MIFUGO HIFADHINI SELOUS.
Miongoni mwa vijana watatu wa jamii ya wafugaji wa wamang'ati katika eneo la Kikwatu tarafa ya Kisaki Morogoro Vijijini, Alex Kipara (19) aliyenusurika katika tukio la kijana, Qambadiyai Kipara (18) aliyetoweka kwa kunadhaniwa kuwa huenda ameuawa na askari wa hifadhi ya taifa ya wanyama pori ya Selous katika tukio linalodaiwa kupigwa risasi na kuuawa ng’ombe 15 na wengine 11 kujeruhiwa wakati vijana hao wakichunga mifugo kwenye hifadhi hiyo ambalo lilitokea oktoba 10 mwaka huu eneo la Matambwe mkoani hapa.
HABARI KAMILI.
WANANCHI wa kijiji cha Dakawa, wilaya ya Morogogoro wamelitaka jeshi la polisi mkoa wa Morogoro kufanya uchunguzi wa kina juu ya madai ya kutoweka kwa kijana mmoja, Qambadiyai Kipara (18) aliyekuwa akichunga mifugo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Selous.
Kutoweka kwa kijana huyo ambako kunadhaniwa na wananchi hao kuwa huenda ameuawa na askari wa wanyama pori kumekwenda sambamba na kupigwa risasi na kuuawa kwa ng’ombe 15 na wengine 11 kujeruhiwa huku ng’ombe wengine zaidi ya 45 wakidaiwa kupotea ndani ya hifadhi hiyo katika eneo la Matambwe tarafa ya Kisaki wilaya ya Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wananchi hao, tukio hilo limedaiwa kuchochewa na askari wa wanyama pori wa hifadhi hiyo ambao wanadaiwa kuwashambulia ng’ombe hao kwa kuwapiga risasi kutokana na kuingia ndani ya hifadhi hiyo kinyume cha sheria.
Akingumza na Mwandishi wa wa Blogu hii katika mahojiano maalum kijijini hapo kiongozi wa wafugaji wa jamii hiyo, Steven Kaoga alisema wafugaji wanaliomba jeshi la polisi mkoa wa Morogoro kufanya uchunguzi ili kubaini madai ya kifo cha Qambadiyai Kipara na upotevu wa ng’ombe hao.
Kiongozi huyo alidai kuwa wananchi wa kijiji hicho wanahofu kuwa huenda kijana Kipara ameuawa wakati wa sakata hilo lililotokea Oktoba 10, mwaka huu majira ya saa 10.00 jioni ambapo vijana wengine wawili Alex Kipara (19) na Kidabahewi Kipara (17) waliokuwa wakichunga pamoja na kijana huyo walifanikiwa kukimbia.
Kaoga alisema kuwa siku ya tukio vijana hao watatu walienda kuchunga mifugo eneo la Matambwe na kuingia ndani ya hifadhi hiyo na ilipofika majira ya saa 10.00 jioni vijana hao waliwaona watu wengi wakiwa na silaha na mmoja wao alitoa amri ya kuwataka wasimame jambo ambalo hawakuweza kulitekeleza na kuamua kukimbia na kuacha ng’ombe hao.
Alisema baada ya kukimbia vijana wawili kati yao walifanikiwa kufika nyumbani kwao eneo la Kikwatu majira ya saa 2 usiku huku mwenzao akishindwa kurejea mpaka leo jambo ambalo linatia mashaka na kuamini kuwa kijana huyo huenda ameuwawa katika tukio hilo.
Kaoga aliendelea kusema kuwa baada ya vijana hao wakikimbia ili kujiokoa milio ya risasi ilikuwa ikisikika huku ng’ombe nao wakitoa milio ya maumivu jambo ambalo liliashiria kupigwa risasi.
“Sisi kama viongozi wa jamii hii ya wamang’ati baada ya kupata taarifa Oktoba 11 asubuhi juu ya tukio hilo nasi tulitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji cha Dakawa na kupatiwa kibali cha kuingia ndani ya hifadhi kwa siku mbili Oktoba 14 na 15 kwa lengo la kumsaka Qambadiyai Kipara ambapo tulimsaka kwa masaa matano bila mafanikio yoyote katika siku hizo mbili,” alisema Kaoga.
Katika safari hiyo ya kumsaka Qambadiyai na mifugo hawakuweza kumpata isipokuwa walishuhudia mizoga ya ng’ombe na wengine wakiwa wanashindwa kutembea kutokana na kuwa na majeraha ya risasi maeneo ya miguuni.
Naye mmoja wa vijana aliyefanikiwa kuokoka katika tukio hilo, Alex Kipara akielezea juu ya tukio hilo lilivyotokea alisema waliowaona watu wengi wakiwa na silaha lakini kabla ya kuwafikia walitoa amri ya kuwataka kusimama jambo ambalo hawakuweza kulitii na kudai kuwa walifyatua risasi nyingi huku zikiwalenga na zingine waliwapiga ng’ombe lakini yeye na Kidabahewi Kipara walifanikiwa kuondoka eneo hilo salama.
Kipara alisema mwenzao hakuweza kurudi kwenye nyumbani na hiyo ilitokana na kila mtu kwa wakati huo alikuwa anaokoa maisha yake kwani hata wao walifika kwenye nyumba kila mtu na wakati wake kutokana na kupotea wakati wa tukio hilo lilipotokea.
Mama mdogo wa vijana hao, Meruna Gillexsa (40) alisema siku ya tukio alishangaa kuona vijana wake wakichelewa kurudi na majira ya 12 jioni.
jioni aliona kundi la ng’ombe wakirudi pekee yao huku baadhi yao wakiwa na majeraha na wengine wakiwa wametapakaa damu jambo ambalo lilimstua na asijue la kufanya kwa wakati huo.
Gillexsa alisema baada ya kuona hali hiyo majira ya saa 2 usiku vijana hao walianza kurejea moja baada ya mwingine na asubuhi ya Oktoba 11 kundi la wafugaji wakiongozwa na vijana hao waliamua kuelekea eneo la tukio kwa lengo la kumsaka Qambadiyai Kipara na kujua chanzo cha mifugo kujeruhiwa lakini wakati wakikaribia eneo la tukio waliona watu wakiwa na silaha na walisitisha zoezi hilo na kurudi nyumbani kwa kuhofia usalama wao.
“Watoto wangu walikuwa na zaidi ya ng’ombe 200 katika tukio hili nimepoteza mwanagu na ng’ombe 50 kutokana na kuingia kwenye hifadhi ya Selous ninachoamini ni kuwa Qambadiyai ameuwawa na kama amekamatwa tungepata taarifa zake katika vyombo vya dola lakini hilo hakuna kwani tangu apate leo tayari amefikisha siku20”, Gillexsa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Adolfina Chialo alipohojiwa alisema kuwa jeshi la polisi halina taarifa kuhusiana na tukio hilo na kuahidi kulifanyia kazi ili kubaini ukweli na kilichotokea katika tukio hilo.
Hata hivyo Kamanda Chialo alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema katika kituo cha polisi kilicho jirani kuhusiana na matukio yoyote ya kiuhalifu na yenye shaka ili yaweze kufanyiwa kazi mara moja badala ya kuchelewa kwani upelelezi unaweza kuvurugika.
0 comments:
Post a Comment