KABILA ATOA AHADI YA KULIUNGANISHA TAIFA LA CONGO
Rais Joseph Kabila akiwa amesimama kutoa heshima kwa gwaride la jeshi wakati wa sherehe za kuapishwa kwake kwa mhula wa pili mjini Kinshasa, Disemba 20 2011.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo aliyeapishwa Jumanne kuanza mhula wa pili wa miaka mitano, ameahidi kuunganisha nchi yake licha ya kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi kudai yeye ni kiongozi halali wa nchi hiyo.
Bwana Kabila aliapishwa Jumanne mjini Kinshasa kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi uliopita ambapo wafuatiliaji wa kimataifa wanasema ulikuwa na kasoro nyingi wakati wa upigaji kura pamoja na hesabu za kura hizo.
Vikosi vya usalama viliwekwa katika pembe zote za mji mkuu kuhakikisha usalama kutokana na upinzani kuendelea kupinga matokeo ya uchaguzi na kutishia kuanda maandamano kudai uchaguzi mpya.
Rais Robert Mugabe ndiye kiongozi pekee wa kigeni aliyehudhuria sherehe hizo zilizofanyika katika uwanja mkuu wa michezo mjini Kinshasa.
Maafisa wa Marekani pia wamesema uchaguzi huo ulikuwa na “kasoro nyingi”.
Bwana Kabila anasisitiza kuwa hakuna shaka kuhusu kuchaguliwa tena kwake, na maafisa wa uchaguzi nchini humo wanasema ameshinda uchaguzi huo kiurahisi.
Lakini mpinzani wake mkuu Tshisekedi anayakataa matokeo akisema ni ya wizi na alijitangaza mwenyewe kuwa ni Rais akisema ataapishwa Ijumaa.
Bwana Kabila anamshauri Tshisekedi kutumia mfumo halali wa kisheria nchini humo kuweza kupinga matokeo hayo.
Uchaguzi huo wa urais na wabunge ulikuwa uchaguzi wa pili huru nchini Congo tangu nchi hiyo ilipojitenga miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilimalizika mwaka 2003.
Bwana Kabila alikuwa Rais kwa mara ya kwanza baada ya kuuwawa kwa baba yake mwaka 2001, na baadae alishinda kuwepo madarakani kufuatia kura iliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2006.
0 comments:
Post a Comment