Mkuu wa jeshi la majini Guinea Bissau akamatwa.
Serikali ya Guinea Bissau imemkamata kiongozi mmoja wa cheo cha juu nchini humo kwa jaribio la kutaka kupindua nchi.
Mkuu wa majeshi nchini Guinea Bissau, Jenerali Antonio Indjai, anasema mkuu wa jeshi la majini la nchi hiyo amekamatwa kwa njama za kujaribu kuipindua serikali.
Jenerali Indjai anasema Admirali mkuu, Bubo Na Tchuto alijaribu kufanya mapinduzi ya kijeshi mapema Jumatatu wakati wanajeshi waliposhambulia makao makuu ya jeshi la taifa katika mji mkuu wa Bissau.
Indjai na Na Tchuto ni wakuu wa jeshi wanaojulikana wakitofautiana mara kwa mara katika taifa hilo la Afrika magharibi, linalofahamika kutokana na kufanyika kwa majaribio kadhaa ya mapinduzi na kukosekana kwa hali ya utulivu nchini humo.
Mashahidi mjini Bissau wanasema vikosi mbali mbali vya jeshi vilipambana katika mji mkuu na kumlazimisha Waziri Mkuu, Carlos Gomes kukimbilia kwa muda katika ubalozi wa Angola uliopo karibu na nyumbani kwake.
Bubo Na Tchuto, mkuu wa jeshi la majini nchini Guinea Bissau.
Balozi wa Guinea Bissau nchini Angola, Isac Monteiro alithibitisha dai hilo alipozungumza na Sauti ya Amerika hiyo Jumatatu, akisema kuna wakati mmoja walinzi wa ubalozi wa Angola waliwafyatulia risasi wanajeshi wa Guniea Bisaau, waliojaribu kumchukua mateka Waziri Mkuu huyo.
Jenerali Indjai anadai kwamba jeshi limechukua udhibiti wa makao makuu ya jeshi na kwamba hivi sasa wanadhibiti hali ya mambo. Wakazi wanaripoti kuwepo kwa ulinzi mkali wa kijeshi katika barabara za mji mkuu.
Wakati huo huo, Rais Malam Bacai Sanha, bado yupo nje ya nchi kwa wiki kadhaa, baada ya kuitembelea Paris, Ufaransa ambako alikuwa anatibiwa maradhi ambayo hayakutajwa.
Rais Sanha alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo mwaka 2009, miezi minne baada ya kuuliwa kwa Rais Joao Bernardo Vieira. Guinea Bissau ilikuwa koloni la zamani la Ureno.
0 comments:
Post a Comment