BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JWTZ yalinda kambi za waathirika wa mafuriko Dar

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limechukua jukumu la kusimamia shughuli zote za utoaji huduma kwa waathirika wa mafuriko ikiwa ni siku chache baada ya kuibuka kwa matukio ya uhalifu katika kambi wanakohifadhiwa.

Kabla ya JWTZ kuanza kazi hiyo, kuliripotiwa upotevu wa vitu mbalimbali kama vile magodoro 50 na vyakula vya msaada ambavyo yalipangwa kugawanywa katika kambi mbalimbali.

Jana katika vituo vitatu vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Changanyikeni na Hananasifu, Kinondoni na kuwakuta wanajeshi wakisimamia shughuli zote katika vituo hivyo, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick alisema si ajabu kwa jeshi hilo la wananchi kuingilia kazi hiyo akisema uamuzi huo unatokana na Polisi kuwa na jukumu jingine muhimu la kuhakikisha usalama unakuwepo katika Sikukuu ya Krismasi.

Alisema JWTZ limeombwa kufanya shughuli hizo baada ya watu wengi kujitokeza katika kambi ziliotengwa kwa ajili ya waliopata maafa na kuiba vitu mbalimbali vikiwemo misaada wanayopewa.

Hatua hiyo ya kutumia JWTZ pia imekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kutaka jeshi hilo liingilie kati kulinda kambi hizo kutokana na matukio hayo ya wizi.

Mbowe akiwa katika ziara Dar es Salaam ambayo chama chake kilitoa msaada wa Sh25milioni kwa waathirika, alitaka matumizi ya JWTZ kukabiliana na hali hiyo.

Jana wanajeshi walikuwa katika kambi hizo wakiwa na vitendea kazi mbalimbali yakiwemo magari ya kijeshi wakiwahudumia wananchi.

Usambaziji chakula
Katika hatua nyingine, kumeibuka mvutano mpya uhusu utoaji wa tenda ya kusambaza chakula baada ya waathirika kutaka kupewa vyakula ili wapike wenyewe.

Waathirika takriban 600 wanaoishi katika Kambi ya Benjamin Mkapa jana walikuja juu kutaka wapewe vyakula wapike wenyewe baada ya kupewa mikate 20 tu.

Baadhi ya waathirika hao walisema upatikanaji wa chakula katika kambi hiyo umekuwa mgumu baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba Serikali imetoa tenda ya usambazaji wa chakula.Mmoja wa madiwani ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema baadhi ya viongozi wanayatumia maafa hao kujinufaisha.“Kuna mtu amepewa zabuni ya kusambaza chakula.

Sahani moja ni Sh4,800 na jana tumepokea sahani 78 katika Kituo cha Rutihinda ambako kuna waathirika zaidi ya 300,” alisema.

“Kuna kiongozi (jina tunalo) amepewa tenda ya kusambaza chakula katika kambi zote zilizotengwa kwa kuuza kila sahani Sh4,800 huku chakula kinachotolewa kikikadiriwa kuwa cha Sh1,200,” alisema na kuongeza:

“Hali hiyo imesababisha sisi katika Kituo cha Sekondari ya Benjamin Mkapa kupata mikate 20 tangu jana kwa kuwahudumia wananchi 600.

Wananchi wanafika mahali wanakimbia mchana na kurudi usiku wakiwa na chakula kwa ajili ya watoto wao.”

Hata hivyo, waathirika waliopo katika kambi hiyo ya Benjamin Mkapa wamesema wapishi waliopewa tenda ya kupika chakula hapo wamebadili mwelekeo tangu JWTZ lilipoanza kazi ya usimamizi kwani badala ya kupikia hapohapo wamekuwa wakipikia mbali na kukifikisha hapo kwa magari.

Mmoja wa waathirika hao, Juma Abdallah alidai kwamba badala yake, wapishi hao wamekimbilia Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko ambako kuna kambi nyingine yenye waathirika 415.

Alipoulizwa kuhusu upatikanaji wa huduma hiyo muhimu ya chakula, Sadick alisema hilo si jukumu lake.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na baadhi ya watu wasiohusika kujitokeza wakati wa kula na kisha kuondoka jambo linalosababisha chakula kilichopangwa kushindwa kuwatosha wahusika.

Vifo na athari nyingine vyaongezeka idadi ya vifo kwa wathirika wa maafa ya mafuriko hayo imeongezeka na kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, idadi hiyo imefikia watu 40.

Alisema idadi hiyo imeongezeka baada ya kupatikana maiti za watu wengine wawili ambazo zimehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mvua hizo zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo, kuanzia Desemba 20, mwaka huu zimesababisha wakazi zaidi ya 5,000 wa eneo la Mongo la Ndege, Kata ya Ukonga, Dar es Salaam kukosa mawasiliano baada ya kubomoka kwa madaraja manne.

Madaraja hayo yaliyopo katikati ya Kinyerezi na Gongo la Mboto yalibomoka siku ya kwanza mvua hizo zilipoanza kunyesha.

Mwenyekiti wa Kamati inayoshughulikia ujenzi wa barabara na madaraja hayo, Benjamin Kilamato alisema jana kwamba mafuriko hayo yamesababisha kukatika kwa mawasiliamo kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo ya Kinyerezi, Ukonga, Uronguni na Gongo la Mboto.

“Leo (jana), ni siku ya tano tangu kutokea kwa mafuriko yaliyosababisha kuharibika kwa miundombinu. Huduma muhimu hazipatikana kwa wakati na hata pale zinapopatikana huwa ni kwa gharama ya juu,” alisema Kilamato.

Kilamato alisema kutokana na barabara kukatika wameamua kuchangishana fedha za ukarabati ili kuwezesha magari kuendelea kupita na kusambaza huduma muhimu.

“Kwa sasa bidhaa mbalimbali za majumbani zimepanda bei. Kwa mfano, maji ambayo tulikuwa tunanunua lita 3,000 kwa Sh21,000 sasa tunanunua kwa Sh40,000 yaani ni mateso matupu,” alisema Kilamato.

Kilamato alisema tangu tukio hilo lilipotokea, hakuna kiongozi yeyote aliyefika kuwapa pole wala kutoa mawazo ya nini kifanyike.

“Hapa hajafika mtu yoyote, si mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mongo la Ndege, Diwani Elizabeth Mbano wala Mbunge wa Ukonga, Eugene Mwaiposa,” alisema Kilamato.Ndiyo maana alisema wameamua kujichangisha fedha ili kufanya ukarabati huo wenyewe.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: