WADAU WA KILIMO CHA SUKARI TUNAFUATILIA WARSHA.
SERIKALI YAANZA KUWEKA MIKAKATI YA KUPUNGUZA UPUNGUFU WA SUKARI KWA KUANZISHA VIWANDA VIDOGO VYA KUSINDIKA SUKARI KUANZIA MWAKA 2012.
SERIKALI imeanza kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza tatizo la upungufu wa sukari kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika sukari na kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo.Mkakati huo ni maalum kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa tani 100,000 za sukari zinazohitajika kwa mwaka na kukidhi matumizi ya ndani, mpango ambao utaanza mwaka 2012/2014 hapa nchini.
Hayi yalielezwa na Mkurugenzi wa Sheria na Udhibiti wa Bodi ya Sukari nchini, Henry Semwaza alipokuwa akizungumza kwenye warsha kuhusu mikakati ya wakulima wa miwa, maendeleo ya nishati, mimea mbadala na upungunzaji wa umasikini mjini Morogoro.
Semwaza alisema kwa sasa serikali imeanza kuweka mikakati ya kupunguza tatizo la upungufu wa sukari kwa kuanzisha vindanda vidogovidogo vya kusindika sukari kuanzia mwaka 2012/2013.
Semwaza alieleza kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha tani 300,000 kwa mwaka na upungufu ni tani 100,000 za sukari ambapo mahitaji halisi ni kiasi cha tani 500,000 kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya ndani hivyo mpango huo utasaidia kupunguza ukosefu wa sukari hapa nchini.
“Serikali imeanza kuweka mikakati madhubuti ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo na mashamba mapya kuanzia mwaka 2012 ambapo ukamilikaji wa viwanda hivyo na mashamba yatapunguza au kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa sukari kutokana na mikakati hiyo kukamilika,” alisema Semwaza.
Aidha alisema kuwa ukiachilia mbali mpango huo wa kuanzishwa viwanda hivyo, serikali ipo mbioni kuanzisha mashamba mapya ya kilimo cha miwa katika kijiji cha Ruipa kilichopo tarafa ya Mngeta Wilaya ya Kilombero mkoani hapa ambapo tayari mchakato wa mpango huo umeanza.
Alisema kuwa katika mashamba hayo mapya kuna zaidi ya hekta 15,000 za ardhi ambazo mchakato wa maandalizi yake tayari umeanza kufanywa kunzia ngazi ya kijiji na Wilaya ili kuweza kupata ardhi hiyo.
Naye Mwenyekiti wa chama cha wakulima wa zao la miwa Tanzania (TSGA) Dk George Mlingwa alisema kuwa kwa sasa Tanzania inaweza kutumia zao la miwa kuzalisha nishati mbadala ikiwemo mafuta ya petroli na dizeli kwa ajili ya kutumika katika magari licha ya matumizi machache ya zao la miwa yanayotumika hivi sasa.
Alitaja kuwa matumizi hayo yanatokana na zao la miwa kuwa sukari, juisi, molasesi ya miwa, juisi ya Sugar beet na molasisi ya sugar beet hivyo matumizi hayo yanaweza kuongeza kwa uzalishaji wa nishati hiyo itokanayo na zao hilo la miwa.
Mlingwa alisema kuwa kwa sasa nchi zilizoendelea tayari wameanza kutumia nishati hiyo pamoja na Brazil, Marekani, China, Canada, Thailand ambazo nchi hizo huzalisha lita zaidi ya lita 10 bilioni ambapo Brazil akiwa mzalishaji mkubwa akifuatia na Marekani inayozalisha lita tano milioni kwa mwaka.
Dk Mlingwa alisema kuwa magari ambayo tayari yanatumia nishati hiyo ni gari aina ya Flexi Fuel (FFV) ambalo hutumia nishati hiyo na mafuta ya petroli na dizeli ya kawaida ambapo asilimia 80 ya magari mengi nchini Brazil yanatumia nishati hiyo.
Aliongeza kuwa ili kuleta msisimko wa uzalishaji wa nishati hiyo inatokana na mimea kwa Tanzania, kunahitajika sera kuhusu uzalishaji hususani ardhi kuwepo na sheria inayohusu uchakachuaji bei kwani serikali tayari imeshatoa mwongozo kuhusu nishati mimea.
Licha ya zao la miwa kutoa nishati hiyo yapo mazao mengine ambayo yanaweza kutumika katika kutengeza mafuta ya mimea sambamba na zao la jatropha, michikichi na mtama ambapo makampuni mengi ya nje yako tayari kuwekeza hapa nchini.
0 comments:
Post a Comment