Mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini, Innocent Kalogeries akichangia moja ya hoja 13 zilizosababisha Halmashauri ya Morogoro Vijijini kupata hati chavu baada ya ofisi ya mkaguzi wa mahesabu za serikali (CAG) kubaini upotevu wa zaidi ya sh130Mil za fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo wakati wa kikao cha baraza la madiwani katika halamshauri hiyo mkoani hapa.
Na Venance George, Morogoro.
OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mkoani Morogoro imeanza kukagua hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kufutia kuwepo kwa tuhuma za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha, huku Halmashauri hiyo ikichukua hatua za haraka za kuwafukuza na kuwasimamisha kazi baadhi ya watendaji wake kwa tuhuma hizo.
Taarifa za kukagua fedha za Halmashauri hiyo imetolewa na mwenyekiti wa Baraza la Halmshauri hiyo, Kibena Kingu, wakati wa kikao cha kawaida cha baraza hilo kilichofanyika jana mjini Morogoro.
Katika kikao hicho, wajumbe wa baraza hilo waliazimia kumfukuza kazi, Mhandisi wake, Stephen Mhauka, kuwasimamisha kazi watendaji wake tisa huku ikiwapa onyo wengine 12 kutokana na makosa mbalimbali yakiutendaji ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za Halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo akitoa maamuzi hayo alisema baraza limefikia hatua hiyo baada ya Halmashauri hiyo kupata hati chafu katika hesabu zake za mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Kingu alisema kuwa Mhandisi Mhauka amefukuzwa kazi kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mradi wa Joint Rehabilitation Fund (JRF) zilizopangwa kukarabati vituo na zahanati mbalimbali katika Halmashauri hiyo.
Alisema kuwa hatua ya kumfukuza kazi imekuja baada ya awali baraza hilo kuchukua hatua za kumsimamisha kazi na baadaye mtumishi huyo kukata rufaa tume ya utumishi wa umma na kwamba baada ya tume hiyo kupitia rufaa yake tume hiyo iliamru Halmashauri imfukuze kazi kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi.
“Kumbe hasa sisi tulikosea kumsimamisha kazi kama adhabu kwa mtumishi huyo, tume imeamuru mtumishi huyo kufukuzwa kazi kuanzia leo na kwamba kama mtumishi huyo hataridhika na maamuzi ya tume ana haki ya kukata rufaa kwa mheshimiwa rais,” alisema Kingu.
Aliongeza kuwa hatua ya kukata rufaa kwa rais pia inaweza kuchukuliwa na Halmashauri hiyo ikiwa itaona maamuzi ya kumfukuza kazi mtumishi wake hayakuwa harali katika kipindi cha siku 30 kuanzia jana wakati rufaa ya mtumishi huyo itakuwa halali katika kipindi cha siku 45 kuanzia jana.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo aliyataja majina ya waliosimamishwa kazi kuwa ni pamoja na mweka hazina, Zakaria Sekimweri, mhasibu Frida Mallya, Kaimu ofisa mipango, Philbert Mgwassa, ofisa utumishi Atuganile Swilla, mhasibu wa mishahara Emmanuel Lyapa na mhasibu Magreth Kapinga na aliyekuwa kaimu mganga mkuu wa Wilaya hiyo, Debora Kabudi aliyesimamishwa kazi miezi miwili iliyopita.
Alisema kuwa watumishi hao wamebainika kutumia fedha za Serikali kinyume cha taratibu na kushindwa kutekeleza wajibu wao kisheria hali ambayo imesababisha Halmashauri hiyo kupata hati chafu.
Fedha zilizodaiwa kupotea ni pamoja na Sh16.2 milioni za miradi ya maendeleo, matumizi ya Sh19.8 milioni kinyume cha taratibu na upotevu wa mishahara ya watumishi wa Halmashauri hiyo Sh27.6 milioni na upotevu wa fedha za ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Morogoro Sh100 milioni.
Alisema kati ya watumishi hao wako waliotiwa tuhumani na kusimamishwa kazi kutokana na kushiriki kwa namna moja au nyingine katika mchakato wa upotevu wa fedha ikiwa ni pamoja na kubadili matumizi ya fedha, kushiriki kutoa fedha hizo, kushindwa kusimamia vilivyo malipo ya mishahara na kulipa mishara hewa.
Alisema kuwa katika taarifa ya mkuguzi wa nje wa Hesabu za Halmashauri imebaini kuwa mtendaji kata wa kata ya Tegetero, Betrice Kapinga, mtendaji kata ya Lundi, mtendaji wa kijiji cha Bungu, Gasper Sikuyaleo, mwenyekiti wa kijiji cha tegetero, Mussa Amri walishirikiana katika kupoteza jumla ya Sh800,000 zilizotengwa kwa miradi ya maendeleo ya kata hiyo hivyo baraza pia limewasimamisha kazi.
Katika tuhuma hiyo pia yumo diwani wa kata hiyo, Stephen Makala, ambaye kwa mujibu wa mwenyekiti huyo taarifa za kushiriki kwake katika upotevu wa fedha hizo zitapelekwa kwenye kikao cha kamati ya nidhamu ili hatua zaidi kuweza kuchukuliwa.
Aidha mwenyekiti wa halmashauri hiyo, aliwataja watumishi waliopewa onyo kutokana na makusa mbalimbali ambayo pia yamechangia hati chafu kwa halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kukaa na vitabu vya kukusanyia fedha za kodi na ushuru mbalimbali kuwa ni wachumi, Emmy Hongoli na Aniccetus Mramba.
Wengine ni mhasibu wa mapato, Tumaini Njeleka, kaimu mkaguzi wa ndani, Isaya Sisya, karani wa fedha, C.Komba, mtendaji kata ya Kiroka, Kilion John, mtendaji kata ya Selembala J. Ngalawa, mtendaji wa kijiji cha Kidunda R Mnemvu, Mtendaji kata ya Kasanga stendi E Msimbe, mtendaji kata ya Kiroka H Idd mhasibu wa Halmashauri, Tegemea Lossi na kaimu mtendaji kata ya Mkuyuni S. Wikeld.
Akihitimisha baraza hilo lililochukua masaa manne, mwenyekiti huyo alisema kuwa Halmashauri hiyo haitakuwa tayari kuwaonea haya wabadhirifu na wezi wa fedha za Serikali kwa namna yeyote ile na kwamba amewataka watendaji kufanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa.
Aliongeza kuwa wakaguzi kutoka ofisi ya CAG walioanza kazi yao jana wamejikita katika kukagua fedha Sh100 milioni za ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Morogoro zaidi na kwamba baada ya kukamilika kwa ukaguguzi huo ndiyo kutatoa majibu ya upotevu huo wa fedha.
Hata hivyo kingu alisema kuwa makosa yaliyofanyika katika fedha hizo ni kwa kaimu mganga huyo kubadilisha matumizi ya fedha hizo pasipo idhini ya baraza na hatua hiyo itaweza pia kutazamwa na wakaguzi hao na kutoa taarifa kabla ya maamuzi mengine kuchukuliwa.
0 comments:
Post a Comment