BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BAJETI YA SARIKALI YA MWAKA 2012/2013.

Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa akionyesha begi lililobeba hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013, wakati akielekea kuingia katika ukumbi wa Bunge, mjini Dodoma jana.
 Picha na Edwin Mjwahuzi

SERIKALI jana ilitangaza Bajeti ya Sh15trilioni kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ambayo pamoja na mambo mengine, imelenga kudhibiti mfumuko wa bei kwa kutangaza kutoa vibali vya kuingiza chakula kutoka nje, huku ikiwabana matajiri kwa kuongeza kodi ya bidhaa zisizokuwa za lazima.


Akisoma bajeti hiyo bungeni Dodoma jana, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alitangaza pia kwamba Serikali imepanua wigo wa Kodi ya Mishahara (Paye) na sasa itawagusa wafanyakazi wenye kipato cha kuanzia Sh170,000 badala ya Sh135,000 ya awali, huku ikirejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kutenga Sh7 bilioni kwa ajili ya kuchukua vijana 5,000.

Dk Mgimwa katika Bajeti hiyo pia alitangaza ongezeko la kodi za bidhaa mbalimbali, ikiwamo, bia, soda, sigara, juisi zinazoingizwa kutoka nje huku ikifuta msamaha wa ushuru wa bidhaa kwa magari kwa wote waliokuwa wananufaika na msamaha huo.

Alifafanua kwamba kodi ya vinywaji baridi imepanda kutoka Sh69 kwa lita hadi Sh83 na mvinyo unaotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nchini kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, imeshuka kutoka Sh425 kwa lita hadi 145 kwa lita.

Kodi ya mvinyo unaotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, imepanda kutoka Sh1,345 kwa lita hadi 1,614 kwa lita.

Alisema kodi ya vinywaji vikali imepanda kutoka Sh1,993 kwa lita hadi Sh2,392 kwa lita, bia inayotengenezwa nchini kwa nafaka na ambayo haijaoteshwa, kodi yake imepanda kutoka Sh248 kwa lita hadi Sh310 kwa lita. Bia nyingine zote kodi imepanda kutoka Sh420 hadi Sh525 kwa lita.

Akizungumzia marekebisho ya ushuru kwenye bidhaa za sigara, Dk Mgimwa alisema zote zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kwa tumbaku inayozalishwa nchini, kiwango cha angalau asilimia 75, kodi imepanda kutoka Sh6,820 hadi Sh 8,210 kwa sigara 1,000.

Alisema Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kwa tumbaku inayopatikana nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kodi imepanda kutoka Sh16,114 hadi Sh19,410 na sigara nyingine zenye sifa tofauti na makundi hayo, kodi imepanda kutoka Sh29,264 hadi Sh35,117 kwa sigara 1,000.

Alisema tumbaku ambayo ipo tayari kutengenezwa sigara (cut filler) kodi yake imepanda kutoka Sh14,780 hadi Sh17,736 kwa bunda la sigara 1,000 wakati ushuru wa cigars unabaki kuwa asilimia 30.

Gharama za simu juu

Katika bajeti hiyo, Waziri Dk Mgimwa alisema muda wa maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi umeongezeka kutoka asilimia 10 hadi 12.

Alisema lengo la hatua hiyo ni kuoanisha ushuru wa bidhaa unaotozwa na huduma hiyo katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), kwa kipindi hiki ambacho nchi zipo katika Soko la Pamoja.

Alisema hatua hizo za ongezeko la ushuru wa bidhaa kwa pamoja, zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh144,054.9 milioni.

Misamaha ya kodi ya magari

Waziri huyo alipendekeza kufanyika marekebisho kwenye sheria husika za kodi ya matangazo ya Serikali yanayotoa msamaha wa kodi kwenye magari kwa walengwa mbalimbali ili kuweka ukomo wa umri wa miaka minane kwa magari hayo badala ya miaka 10.

Alisema magari yenye umri wa zaidi ya miaka minane yatatozwa ushuru wa bidhaa wa asilimia 20. Lengo la hatua hiyo ni kupunguza wimbi la uingizaji magari chakavu na kulinda mazingira.

Alitangaza pia marekebisho katika ushuru wa forodha, ikiwemo kufuta msamaha wa ushuru wa forodha katika vitu mbalimbali vikiwemo magari yenye ujazo wa CC 3000 huku pia ushuru wa forodha ukifutwa katika bidhaa nyingine nyingi muhimu.

Alisema katika kuhamasisha na kuchochea ukuaji wa sekta ya ufugaji wa nyuki, vifaa vinavyotumika katika ufugaji na kurina asali vimepewa msamaha wa ushuru wa forodha vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi na wafugaji wa nyuki.

Alisema msamaha wa ushuru wa forodha kwenye migahawa ya majeshi ya ulinzi utaendelea kutolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Alisema kumefanyika marekebisho katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya mwaka 2004 ili kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa wazalishaji wa vyakula vinavyotengenezwa mahsusi kwa lishe ya watoto wenye utapiamlo na watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi.

Alisema kuwa katika Bajeti hiyo, pia wametoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye malighafi zinazotumika katika kutengeneza vifaa vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa (medical diognastic kits) kwa kuwa vifaa hivyo hutozwa asilimia sifuri vinapoagizwa kutoka nje ya nchi.

Katika marekebisho hayo, utatolewa msamaha kwenye mitambo (machinery) na vipuri vyake vinavyotumika kwenye uchimbaji wa madini lakini hautahusisha vipuri vya magari vitakavyoagizwa na makampuni yanayojihusisha na uchimbaji wa madini.

Katika bajeti hiyo, pia umetolewa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye vyuma vinavyowekwa kwenye kingo za barabara na lengo lake ni kutoa unafuu katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Alisema ushuru wa forodha umepunguzwa kwa ving’amuzi kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri ili kuwezesha mabadiliko katika teknolojia ya analogia na kwenda katika teknologia ya digitali.

Alisema katika Bajeti hiyo, pia ushuru wa ngano umeondolewa kuwa asilimia 0 badala ya asilimia 35

Alisema Serikali pia imesamehe VAT katika mashine za kutolea stakabadhi (electronic fiscal devices), ili kupunguza bei yake na kuwezesha wafanyabiashara wengi kuwa nazo, kuhamasisha matumizi yake na hivyo, kuongeza mapato ya Serikali.

Katika eneo hilo, Serikali imeondoa VAT kwa vifaa mbalimbali vya kuhifadhia, kusafirisha na kusambaza gesi asilia ili kuongeza matumizi ya nishati hiyo katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kwenye magari, majumbani na viwandani.

Kodi kwa wafanyabiashara

Wafanyabiashara ambao mapato yao hayazidi Sh3,000,000 hawatalipa kodi kuanzia Julai Mosi, mwaka huu. Dk Mgimwa alisema mpango huo umefanywa kulinda mapato ya Serikali.

Kabla ya msamaha huo, wafanyabiashara hao ambao mapato yao hayazidi Sh3,000,000 walikuwa wanalipa Sh35,000.

Marekebisho mengine ya kodi ya mapato ni kuwa wenye mapato kati ya Sh3 milioni –Sh7.5 milioni watalipa Sh100,000 badala ya Sh95,000.

Malengo ya Bajeti

Waziri Mgimwa alisema Bajeti hiyo imejielekeza katika Kukuza Pato la Taifa kwa asilimia 6.8 mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.4 mwaka 2011.

Malengo mengine ni kuimarisha miundombinu ya uchumi, ikijumuisha umeme, barabara, reli na bandari, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia 18 kwa mwaka 2012/13 kulinganisha na mwelekeo wa asilimia 16.9 mwaka 2011/12.

Dk Mgimwa alitaja malengo mengine kuwa ni pamoja na kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei ili urudi kwenye viwango vya tarakimu moja na kuwa na kiwango tengemavu cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.

Malengo mengine ni kukuza mikopo kwa sekta binafsi kwa kiwango cha asilimia 20 ya Pato la Taifa ifikapo mwishoni mwa Juni 2013, sambamba na jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei, kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo na wa kati, kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta za huduma za jamii, kuimarisha utawala bora na uwajibikaji na kujenga uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na kifedha pamoja na kushiriki kwa ufanisi katika ushirikiano kikanda na kimataifa.

Matumizi ya Maendeleo

Kuhusu matumizi ya maendeleo, Waziri Mgimwa alisema itazingatia vipaumbele vya miundombinu ya umeme - mkazo ukiwa upatikanaji wake kwa kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji na jumla Sh498.9 bilioni zimetengwa.

Serikali pia itatekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China wenye thamani ya Dola za Marekani 1.2 milioni utakaosimamiwa na TPDC.

Kuhusu usafirishaji na uchukuzi, alisema mkazo katika sekta hiyo utakuwa ni kuimarisha reli ya kati ikijumuisha ukarabati wa injini na mabehewa ya treni.

“Kwa upande wa barabara, miradi inayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi. Katika usafiri wa anga na majini, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa gati ya Ziwa Tanganyika. Jumla ya Sh 1,382.9 bilioni zimetengwa katika eneo hili,” alisema.

Kuhusu maji safi na salama, alisema lengo ni - kuongeza upatikanaji wake mijini na vijijini na kwamba kiasi cha Sh568.8 bilioni kimetengwa.

Kwa upande wa kilimo, uvuvi na ufugaji alisema katika sekta hizo, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itawekeza katika kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kilombero na Malagarasi pamoja na kuongeza tija na thamani, kubadilisha mfumo wa kilimo na kukuza kilimo cha misitu.

Kuhusu kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na kuhakikisha uhakika wa chakula, Serikali itaimarisha utekelezaji wa dhana ya Kilimo Kwanza kwa kuhakikisha nguzo zake zote zinaendelea kuzingatiwa.

Alisema mikoa inatakiwa kuendelea kutenga ardhi na vijiji kutakiwa kupima na kurasimisha ardhi kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje na kwamba kiasi cha Sh192.2 bilioni kimetengwa katika eneo hilo.

Akizungumzia maendeleo ya viwanda, alisema Serikali inakusudia kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini; viwanda vinavyoongeza thamani ya madini; viwanda vikubwa vya saruji na viwanda vya eletroniki na Tehama pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji mijini na vijijini na kukuza ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: