RAIS mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela (94) ambaye amelazwa hospitalini kwa siku kadhaa sasa, jana amezushiwa kifo.
Uvumi huo, ulionekana kushtua watu wengi, baada ya baadhi ya mitandao ya kijamii kudai Mandela amefariki dunia kutokana na afya yake kuzorota kila kukicha.
Uvumi huo wa jana, ulikwenda sambamba na madai kuwa salamu za rambirambi kutoka duniani kote, zinamiminika nchini Afrika Kusini kutokana na kifo cha kiongozi huyo mstaafu anayeheshimika duniani kote.
Taarifa hizo zilileta mshituko mkubwa kabla ya Msemaji wa Hospitali ya Kijeshi Mjini Pretoria alikolazwa Mandela kujitokeza hadharani na kuukana uvumi huo.
Msemaji huyo, alisema Mandela kipenzi cha watu duniani maarufu kama Madiba, anaendelea vema na matibabu dhidi ya maradhi ya mapafu yanayomsumbua.
Mandela anajulikana kama shujaa wa demokrasia na pengine ndiye kiongozi anayependwa kuliko wote duniani.
Mandela, alifungwa jela miaka 27 wakati wa utawala wa kibaguzi wa makaburu nchini humo na aliachiwa huru mwaka 1990, akiwa na umri wa miaka 71.
Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini miaka minne baadaye na ndiye aliyekuwa rais wa kwanza mweusi wa taifa hilo lililokuwa limejaa sera za kibaguzi.
Alistaafu kutoka maisha ya umma miaka kadhaa iliyopita na alionekana hadharani kwa mara ya mwisho wakati wa sherehe za ufunguzi wa michuano ya Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini humo, mwaka 2010.
Hata hivyo, aliendelea kutembelewa na marafiki na viongozi wakuu wa dunia mara kwa mara.
Wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton alipozuru Afrika Kusini wakati wa kiangazi mwaka huu, alimtembelea Mandela nyumbani kwake katika Kijiji cha Qunu, jimbo la Cape Mashariki.
Katika picha waliyopiga pamoja Mandela kama kawaida yake, alionekana na tabasamu usoni, huku afya yake ikionekana kuwa dhaifu wakati akiwa katika kiti cha kusukuma kwa mkono.
Pamoja na kwamba umri umemfanya apotee machoni mwa watu, Mandela bado ameendelea kuwa mtu muhimu kwa taifa la Afrika Kusini na Bara la Afrika kwa ujumla wake.
Kwa wengi, bado ni lulu, kiongozi mcheshi, mkarimu na aliye tayari kujishusha tofauti na watangulizi wake wa kisiasa.
Mandela ndiye Baba wa Taifa hilo ambaye fikra zake zinaendelea kutumika kuijenga Afrika Kusini.
Wakati uvumi ukiwa unasambaa mara kwa mara kwa miaka mingi kuhusu afya ya Mandela, taasisi yake ya Nelson Mandela imekuwa ikiutoa umma wasiwasi au kuuomba umwache Madiba apumzike katika maisha yake ya ustaafu. Lakini wasiwasi kuhusu hali yake ya kiafya ulienea.
Januari 2011, alikimbizwa hospitali kutokana na maambukizo katika njia ya hewa na kuzua mshtuko mkubwa nchini humo.
Mapema wiki hii, Rais Jacob Zuma alitangaza kuwa Mandela amelazwa kutokana na maambukizo katika mapafu lakini anaendelea vema na matibabu.
Hii ni mara ya pili, mwaka huu kukimbizwa hospitalini kwani Februari, alilazwa kwa ajili ya kuchukuliwa vipimo baada ya kulalamika maumivu makali ya tumbo.
Nelson Rolihlahla Mandela, alizaliwa Julai 19, 1918, huko Umtata katika eneo la Transkei la Cape Mashariki ambako baba yake alikuwa Chifu wa watu wa Kabila la Xhosa.
Alihudhuria shule za Methodist na baadaye Chuo Kikuu cha Fort Hare mwaka 1938.
Lakini alitimuliwa mwaka 1940 kwa kuwaongoza wanafunzi wenzake katika mgomo. Wakati huo alikuwa pamoja na mwenzake Oliver Tambo ambaye walijenga naye uanaharakati na urafiki mkubwa.
Mandela, ambaye ana urefu wa futi sita na inchi mbili, aliwahi kuwa na uzito wa pauni 245 akiwa kama bondia wa uzito wa juu kipindi fulani cha ujana wake.
Pia alisomea sheria kwa njia ya posta katika Chuo Kikuu chenye watu weupe zaidi cha Witwatersrand na kujipatia shahada yake ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini mwaka 1942.
0 comments:
Post a Comment