Waziri mkuu wa zamani wa Mali aliyejiuzulu na kukamatwa Cheikh Modibo Diarra.
Bw. Traore amesema amepokea ombi lake rasmi la kujiuzulu kwa maandishi na amelikubali. Alimshukuru Bw.Diara kwa kazi yake na kusema Mali watamjua waziri wao mkuu mpya chini ya saa 24 zijazo na watakuwa na serikali mpya mwishoni mwa wiki.
Dakika chache tu baadaye Diango Cissoko mfanyakazi wa serikali wa siku nyingi ambaye aliwahi kushika nafasi katika utawala mbali mbali wa zamani alitajwa kuwa kaimu waziri mkuu mpya kutokana na amri ya rais iliyosomwa katika taarifa ya habari.
Jumatatu usiku wanajeshi walimkamata Diara nyumbani kwake wakati akijiandaa kwenda Ufaransa.
Saa chache baada ya kukamatwa Bw.Diara alijiuzulu wadhifa wake na kutangaza kwenye televisheni ya taifa.
Bw. Diarra alisema yeye na serikali wanaachia madaraka kwa maslahi ya amani na aliomba msamaha kwa watu wote wa Mali wanaotaabika kutokana na mzozo huo.
Aliwashukuru washirika wake na kuitakia mafanikio timu mpya ambayo inachukua madaraka baada yake.
Mali bado inajikokota kutokana na mapinduzi ya kijeshi ya Machi 22.
Wanamgambo wenye mahusiano na Alqaeda wamechukua nusu ya nchi sehemu ya kaskazini wakati kusini bado imegubikwa na mzozo wa kugombania madaraka kati ya raia na viongozi wa kijeshi.
Baraza tawala la kijeshi linasema Bw.Diara alilazimika kuondoka kwasababu aliruhusu ajenda yake binafsi ya kisiasa iingilie kati kwenye kazi zake za kitaifa.
Mkuu wa baraza la kijeshi Captain Amadou Sanogo alisema katika taarifa kwenye televisheni Jumanne usiku kwamba baraza lake halijamlazimisha Bw.Diarra kujiuzulu lakini walirahisisha kitendo hicho.
Sanogo anasema Bw.Diarra alikataa kutambua madaraka ya rais na kuwa hatari kwa Mali. Pia alimlaumu waziri mkuu huyo wa zamani kwa kuzuia juhudi za kulipatia upya jeshi silaha na vifaa vya kazi.
Sanogo alikataa kwamba Bw.Diarra yuko kwenye kifungo cha ndani Jumanne na kusema kwamba badala yake wanajeshi wanamlinda kwa ajili ya usalama wake.
Jumuiya ya kimataifa inalaani kukamatwa kwa Bw Diarra na na hatimae kujiuzulu kwake.
Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lilisema katika taarifa yake kwamba jeshi la Mali liache kuingilia kati kazi ya serikali ya muda na kutishia litachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuweka vikwazo maalum , dhidi ya wale wanaofanya kazi kuhujumu utawala wa kikatiba na uthabiti wa Mali.
0 comments:
Post a Comment