Na Anna Nkinda – Maelezo, Mwanza
UMOJA
wa waendesha pikipiki wa mkoa wa Mwanza wameiomba Serikali kuwapa
mafunzo ya uongozi pamoja na mikopo yenye masharti naafuu ili waweze
kununua pikipiki zao binafsi na kujiajiri wenyewe nahivyo
kujiinua kiuchumi tofauti na ilivyo sasa kwani wengi wao wameajiriwa na
hivyo kuwatajirisha waajiri wao.
Waendesha
pikipiki hao ambao wengi wao ni vijana wametoa ombi hilo hivi karibuni
wakati wakiongea na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana James Kajugusi wakati alipowatembelea ofisini kwao maeneo ya Mlango mmoja jijini Mwanza ili kuona shughuli zinazofanywa na umoja huo.
Akiongea
kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Umoja huo Makoye Bunoro alisema kuwa
kuna makampuni yanayokopesha pikipiki kwa riba kubwa jambo
linasababisha mkopaji kuchukua muda mrefu wa kulipa deni na kutokupata faida na kuyaomba makampuni hayo yakopeshe kwa riba ndogo ila nao wapate faida.
“Tatizo
kubwa linalowakabili waendesha pikipiki ni kutokuwa na elimu, kama
Serikali itatoa mafunzo kwa waendesha na wapanda pikipiki wote ajali za
barabarani zitapungua kwa kiasi kikubwa kwani ajali nyingi zinatokana na kutoelewa sheria za usalama barabarani kwa watumiaji wa vyombo hivyo”, alisema Bunoro .
Aliendelea kusema kuwa chama hicho kinasimamia upatikanaji wa leseni, hadi sasa waendesha
pikipiki 2034 ambao ni wanachama na siyo wanachama wameshapata leseni
pamoja na mafunzo yaliyotolewa na Chuo cha ufundi VETA kwa
gharama naafuu jambo ambalo limeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali
za barabarani zinazotokana na waendesha pikipiki katika mkoa huo.
Wilaya
ya Magu waliopata mafunzo na leseni ni 190, Sengerema 172, Misungwi 57,
Ukerewe 106, Kwimba 28, Nyamagana na Ilemela 1484.
Bunora alisema, “Ndani
ya Chama chetu kuna kitengo cha Polisi Jamii ambacho kimekuwa
kikipambana na matukio ya uhalifu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na
tumeweza kuwakamata wahalifu ambao walishindikana na wengine walikuwa
wanatafutwa kwa muda mrefu”.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Kajugusi aliwataka vijana hao kuimarisha umoja
wao na kutokubali kutumiwa na makundi ya watu kwa manufaa ya watu hao
kwani vijana wananguvu za kutosha hivyo watu wengi wanapenda kuwatumia,
bali wao watumie nguvu zao kutafuta ajira ambazo zitawainua kiuchumi na kuleta maendeleo ya nchi yao.
Alisema
kuwa Serikali iliamua kuruhusu pikipiki kuwa chombo cha kuendesha
abiria ili zisaidie katika masuala ya usafirishaji na kuongeza fursa ya
upatikanaji wa ajira binafsi kwa vijana ili waweze kujiajiri wao wenyewe
hivyo watambue kuwa biashara wanayoifanya ni halali jambo la muhimu ni
kufuata sheria zilizopo.
Kajugusi alisema, “Ninachowashauri muanzishe chama cha Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) yenu
ambayo itawawezesha kupata mkopo kirahisi kwani hivi sasa kuna fedha za
mkopo wa mfuko wa vijana ambazo kupitia Halmashauri za wilaya
zimewasaidia vijana wengi hapa nchini nanyi kama vijana mnastahili
kupata fedha hizi”.
Alimalizia kwa kusema kuwa Idara ya vijana kwa kupitia vituo vyake vya kuwajengea uwezo vijana itaangalia uwezekano wa kutoa mafunzo kwa viongozi wa wapanda pikipiki wa wilaya ili wakawafundishe wenzao.
Umoja huo ulianzishwa mwezi wa pili mwaka 2011 na
unajumla ya wanachama waliosajiliwa 1034 kutoka wilaya za Nyamagana
484, Ilemela 204, Sengerema 87, Ukerewe 51, Magu 123, Misungwi 57 na Kwimba 28.
0 comments:
Post a Comment