Kikosi cha Simba kitakachoivaa klabu ya Recreativo Libolo ya nchini Angola.
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetoa ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Simba ya Tanzania, ambayo ni klabu inayoaminika zaidi Afrika Mashariki kwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa inaanza Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza na Recreativo do Libolo ya Angola.
Azam FC, ambayo itacheza Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza mwakani imepangwa na vibonde Al Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Simba itaanza nyumbani jijini Dar es Salaam Februari 17 na itarudiana na mabingwa hao wa Angola wiki mbili baadaye jijini Luanda, Angola.
Simba ikivuka kigingi hicho cha mabingwa wa Angola, itakumbana ana kwa ana na El Merreikh ya Sudan ambayo inataka kumnunua Mrisho Ngassa wa Azam aliyekuwa akicheza Simba kwa mkopo.
Kwa upande wa Azam ambayo nayo itaanzia nyumbani Dar es Salaam ikicheza siku moja kabla ya Simba yenyewe ikivuka hatua hiyo ya kwanza itacheza na mshindi kati ya Johansens ya Sierra Leone dhidi ya Barrack Y. C. II ya Liberia.
Kwa upande wa Zanzibar, Jamhuri itacheza na St. Georges ya Ethiopia kwenye Ligi ya Mabingwa na ikivuka itakwaana na Djoliba ya Mali.
Hata hivyo kwa upande wa Simba watakuwa wakikutana na timu ambayo ilianzishwa mwaka 1942 na inayotumia Uwanja wa Manispaa unaoitwa Calulo wenye uwezo wa kubeba mashabiki 10,000.
Mabingwa hao wa Angalo ambao katika historia wametwaa ubingwa mara mbili tu mwaka 2011 na 2012 makao makuu yao yapo Libolo katika Jimbo la Cuanza Sul.
Baadhi ya wachezaji wa timu hiyo inayofundishwa na Kocha Zeca Amaral ni Mendes, Ze Kalanga, Yuri, Nuno Silva na Andres Madrid.
Kocha wa timu ya taifa ya Rwanda, Sredejovic Milutin 'Micho' alisema jana Jumatatu kuwa Simba imepangiwa timu ngumu.
"Ni ratiba ngumu sana kwa Simba, wana nafasi ndogo ya kusonga mbele. Hii timu ndio mabingwa wa Angola, ni wazuri sana," alisema Micho.
Simba ambayo makamu wake mwenyekiti Geofrey Nyange 'Kaburu' amesisitiza kwamba kesho Jumatano watamtangaza Kocha Mkuu, bado haijakamilisha usajili wake mdogo.
Simba na Azam ndizo zinazoiwakilisha Tanzania Bara mwakani huku Yanga ikiwa haina nafasi yoyote ya kushiriki michuano mikubwa zaidi ya Kombe la Kagame Julai nchini Sudan.
0 comments:
Post a Comment