WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliungana na Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsavangirai kumpigia debe mgombea wa urais wa Kenya, Raila Odinga huku akisema mgombea huyo kupitia Chama cha Orange Democratic Party (ODM), anastahili kuwa Rais wa nchi hiyo kutokana na sifa zake za uongozi.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa ODM jana, Dk Magufuli alisema hakuna sababu zozote zitakazowafanya Wakenya wasimchague Odinga.
“Nataka kuwaambia Wakenya kwamba Odinga ni mcha Mungu, mnatakiwa kujua hilo. Kama mimi ningekuwa Mkenya ningempigia huyu jamaa kura ili aongoze nchi. Lakini sasa kwa kuwa siruhusiwi hata kupiga kura, basi nawaambia msiache kumchagua huyu atawaongozeni vizuri,” alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli alisema kati ya wagombea wote waliojitokeza kuwania kiti cha urais nchini Kenya, hakuna anayemfikia Odinga na hiyo inaonyesha kuwa wakimchagua atawasaidia bila ubaguzi.
Alisema na hata Odinga ambaye ni Waziri Mkuu wa Kenya akiamua kugombea ubunge katika Jimbo lake la Chato, hawezi kumshinda.
“Kwa hiyo nasimama hapa ndugu zangu wana ODM kuwapa pongezi kubwa sana, mmmefanya kitu kikubwa sana kwa sababu mmechagua jembe,” alisema.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wajumbe wa mkutano huo, Dk Magufuli alisema kama angekuwa akipiga kura angempa Odinga kura zake zote kwa sababu ni mtu mwenye upendo,
uvumilivu, asiye na makuu wala ubaguzi na anayependa kushirikiana na watu wote.
uvumilivu, asiye na makuu wala ubaguzi na anayependa kushirikiana na watu wote.
Alisema Odinga ni mpenda amani na kusisitiza kuwa amelisema hilo kwa sababu amani ni muhimu katika maendeleo ya Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.
Alikipongeza chama hicho kwa kuamua kushirikisha vyama zaidi ya 15 na kuweka nguvu zao pamoja ili kushinda katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Machi 4, 2013.
Akizungumzia uhusiano wake na Odinga, Dk Magufuli alisema walifahamiana tangu alipokuwa Waziri wa Ujenzi wa Kenya wakati yeye akiwa Waziri wa Ujenzi wa Tanzania.
“Uliwahi kufika Tanzania mara nyingi na hata kuhudhuria mazishi ya baba yangu mpendwa, ukaja na mawaziri zaidi ya watano pamoja na mke wako katika jimbo langu ninalotoka linaloitwa Chato,” alisema.
Bila kuwataja majina, aliwapiga vijembe baadhi ya wagombea wengine nchini Kenya akisema hawawezi kutembea nje ya nchi hiyo kutokana na kubanwa na sheria, huku akisema Odinga ana uwezo wa kutembea ulimwenguni kote bila pingamizi.
Kuhusu Muungano wa vyama vya kisiasa nchini humo, Dk Magufuli alisema hiyo inaleta changamoto kwa siasa za Kenya… “Huu ni muungano mzuri ambao naukubali sana, hususan walioungana na Odinga ni dhahiri kabisa kwamba wanamtabiria ushindi mkubwa.”
Alisema Wakenya wanatakiwa kuachana na uongozi wa makabila akisema hautawafikisha popote kwani ni kikwazo cha maendeleo na pia ndicho chanzo cha migogoro nchini humo.
“Msilete ukabila… mtakuwa mnaivuruga Kenya yote, watu watakufa, watakosa uhuru wa kuishi sehemu moja kama Waafrika wengine,” alisema.
Alisema vurugu zinazofadhiliwa na utawala uliopo madarakani na ukandamizaji wa washiriki wengine wa shughuli za kisiasa hauhalalishi uchaguzi kuwa huru na wa haki.
Aliwaonya wajumbe hao kutorudia tena kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyo sasa kwa kuwa Serikali ya aina hiyo hujenga chuki kati ya viongozi na kudhoofisha utendaji wa Serikali.
“Hakikisheni mnaipigia kura ODM kwa wingi ili ishinde Uchaguzi Mkuu ujao na kuunda Serikali moja ambayo itapimwa kwa kuzingatia programu zake.
Naye Tsavangirai aliwataka Wakenya kuepuka machafuko na wale ambao watakuwa wameshindwa katika kinyang’anyiro hicho cha urais, wakubali matokeo.
Aliungana na Dk Magufuli kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa akiwataka isiwepo kwa madai kuwa ni chanzo cha migogoro.
“Serikali ya Muungano ni chanzo cha migogoro kwani kila mgogoro uliopo Afrika unasabaishwa na Serikali ya Muungano,” alisema.
0 comments:
Post a Comment