WAZIRI wa Ujenzi, John Magufuli, ameiumbua Ofisi ya Waziri Mkuu na
Wizara ya Sayansi na Teknolojia kuwa inaongoza kwa kutumia magari ya
Serikali yasiyosajiliwa. Dk. Magufuli, alisema hayo jana alipokuwa
akizindua Bodi ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Bodi ya
Mfuko wa Barabara.
Alisema juhudi kubwa zinafanyika kuhakikisha magari yote ya
Serikali, yasiyosajiliwa yanatumia namba za kiraia, yanasajiliwa kwa
namba za Serikali.
“Hadi sasa magari 974, yaliyokuwa na namba za
kiraia yamesajiliwa kwa namba za Serikali, yako magari mengine 746 ya
Serikali hayajasajiliwa.
“Kuna wizara mbili zinaongoza kuwa na
magari ambayo hayajasajiliwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Sayansi na Teknolojia,”
alisema.
Alisema utaratibu wa kuhakiki magari yasiyosajiliwa,
unaendelea ili kuhakikisha magari yote, yanasajiliwa na yanatumia namba
za Serikali.
Alisema makusanyo ya Mfuko wa Barabara yameongezeka
kutoka Sh bilioni 47.252 mwaka 2000/01 na kufikia Sh bilioni 406.77
mwaka 2011/12, ikiwa ni ongezeko la asilimia 760.
Alisema mwaka
2012/13, lengo ni kukusanya Sh bilioni 429.664 kwa ajili ya matengenezo
ya barabara nchini, ambapo fedha hizo, zitakidhi asilimia 70 ya mahitaji
ya matengenezo hayo.
“Utafiti umefanyika katika halmashauri,
asilimia 40 hazina wahandisi waliosajiliwa, nawaambia Bodi ya Mfuko wa
Barabara, kuweni wakali kwa zile halmashauri zote ambazo hazina
wahandisi waliosajiliwa, msiwapelekee fedha.
“Wanatakiwa kuajiri
wahandisi waliosajiliwa, badala ya kuendelea kuwatumia mafundi mchundo,
hawataki kuajiri, wakinyimwa fedha watajifunza,” alisema.
Akizungumzia
wahandisi wa TANROADS, Dk. Magufuli aliwataka kufanya kazi kwa kubuni
mikakati, badala ya kupata vigugumizi wanapofikiria kuanza kutengeneza
flay over.
“Msiwe wanasiasa, mfanye yale yanayowezekana, barabara
ya Morocco kwenda Mwenge kuna nyumba zimewekewa alama ya X, kwa ajili
ya kubomolewa kupisha upanuzi wa barabara.
“Nyumba zile
zimebomolewa, wanaostahili kulipwa fidia walipwe fedha zimetengwa na
wale wasiostahili watupishe ujenzi wa barabara ya njia nne uanze.
“Habari
za tuko katika mchakato zimechokwa, mchakato ubaki kwa wana siasa nyie
mbaki kuwa watendaji zaidi,” alisema Dk. Magufuli.
“Bodi zote
mnatakiwa kuwa wakali, msiwahurumie watu waliochini yenu ili thamani ya
fedha ya Watanzania ionekane ikitumika ipasavyo katika barabara zetu,”
alisema.
Baada ya kusema hayo, Dk. Magufuli alizindua bodi mpya
ya TANROADS ambapo mwenyekiti wake ni Hawa Mmanga, wajumbe, Joseph
Nyamhanga, Bakel Sahel, Richard Rugimbana, Haron Kisaka, Eligius
Mwankenja na Elina Kayanda.
Bodi ya Mfuko wa Barabara, itaongozwa
na Mwenyekiti James Wanyancha, wajumbe, Helbert Musilango, Ramadhani
Kija, Jumanne Sigiri, Joseph Nyamhanga, Wilbis Mbogoro, Renatus Bube na
Peter Chisamilo.
Akizungumza Wanyancha alisema, watahakikisha
wanasimamia fedha za mfuko kwa umakini na kukagua vitabu vya mahesabu na
kazi za ujenzi wa barabara kama zinafanyika ilivyokusudiwa.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment