Askari akiangalia ndege aina ya Cessina yenye namba 5 H F25C 182 ambayo
ina uwezo wa kubeba abiria wanne,ikiwa imeanguka nje kidogo ya Uwanja wa
ndege Mpanda mkoani Katavi kando ya Mto Nsemulwa juzi. Ndege hiyo
ilipata hitilafu ikiwa na rubani ambaye alinusurika.
NDEGE ndogo ya abiria mali ya Hifadhi ya Taifa ya Tanapa yenye uwezo wa kubeba watu wanne aina ya C 182, imeanguka katika eneo la Kasimba umbali wa kilometa moja kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda uliopo katika Mkoa wa Katavi na kumjeruhi rubani wa ndege hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja wa Uwanja
wa Ndege wa Mpanda, Maulid Mohamed alisema ajali hiyo ilitokea jana
majira saa 10 .55 jioni katika eneo la Kasimba lililopo ndani ya
Kijiji cha Nsemlwa wilayani hapo.
Mohamed aliitaja ndege hiyo iliyoanguka na
kusababisha majeraha kwa rubani aliyetajwa kwa jina la Adam Athuman
Kajwaa kuwa ni aina ya C182.
Mohamed alieleza kuwa ndege hiyo ilikuwa
imetoka katika uwanja wa ndege wa Mpanda ikielekea katika Hifadhi ya
Wanyamapori ya Katavi.
Hata hiyo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea
umbali wa kilometa moja na nusu kutoka Uwanja wa Ndege wa Mpanda
mara baada ya kuondoka katika uwanja huo ambapo imeharibika sana
sehemu ya bawa lake na upande wa injini.
Meneja wa uwanja huo wa ndege alisema taarifa
za awali zinaonyesha chanzo cha ajali hiyo kilitokana na kufeli
kwa injini ya ndege na kuwa rubani wa ndege hiyo alipata msaada wa
kuokolewa na wananchi waliokuwa wakifanya shughuli za kilimo
kwenye mashamba.
Mmoja wa wa mashuhuda wa tukio hilo Credo
Mwanisenga alieleza kuwa wakati akiwa anafanya shughuli zake za
kilimo ghafla aliona ndege hiyo ikiwa angani ikizimika na baada
ya muda mfupi ikaanguka jirani na mti wa mwembe.
Hata hivyo alisema kuwa zoezi la kumuokoa rubani huyo lilichukua muda kuanza kutokana na mti wa mwembe kuwa na nyuki wengi.
Hata hivyo alisema mara baada ya kufanikiwa
kumtoa rubani huyo, huku akiwa amepata majerahi makubwa sehemu ya
uso na maumivu sehemu ya kifua na kumkimbiza katika Hospitali ya
Wilaya ya Mpanda kwa matibabu zaidi.
Pia akiwa anakohoa damu, rubani huyo aliwahishwa
haraka katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda baada ya kupata msaada wa
gari la meneja wa uwanja wa ndege aliyefika eneo la tukio.
0 comments:
Post a Comment