DK SLAA.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa wako radhi kuchukiwa kwa uamuzi wao mgumu wa kuwafukuza mafisadi ndani ya chama hicho.
Akizungumza jana katika mahojiano na moja ya kituo cha runinga, Dk. Slaa alisema Kamati Kuu ya chama hicho ilifikia uamuzi kuwachukulia hatua baadhi ya madiwani akiwemo mmoja wao aliyekiri mbele ya kamati hiyo kuwa alipewa sh milioni 20 na CCM.
Dk. Slaa alisema kuwa litakuwa ni jambo la ajabu kwa chama hicho kukubali kukumbatia mafisadi na walarushwa wakati kila siku wamekuwa wakipigania matatizo hayo yaondolewe ndani ya serikali.
“CHADEMA haimuonei mtu, inatenda kwa mujibu wa katiba; hivi kweli tunaweza kumvumilia kiongozi ambaye amekiri hadharani kupokea kiasi cha fedha kama rushwa kutoka CCM? Hii itakuwa ni aibu kwa chama ambacho kinawanyooshea kidole kila siku walarushwa na kutaka waondolewe serikalini,” alisema.
Kuhusu kuwepo kwa watu wanaolalamikia ukali wake, Dk. Slaa alisema kuwa kwa nafasi aliyonayo ni lazima awe mkali kutokana na kulazimika kusimamia misingi ya chama.
Dk. Slaa alisema kuwa afadhali achukiwe na watu wachache, lakini apendwe na Watanzania walio wengi.
Alisema kuwa, suala la madiwani wa Karatu hawezi kulizungumza kwa kuwa Kamati Kuu iliunda tume ya uchunguzi ili kuchunguza suala hilo ambapo jukumu hilo amepewa mwenyekiti wa chama hicho.
“CHADEMA hatuwezi kuvumilia harufu yoyote ya ubadhirifu inayotajwa mahali popote …tunalazimika kuchukua hatua ili kuhakikisha tunalijenga taifa lililo na misingi kama ile iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.
Alisema kuwa hawawezi kuinyooshea kidole CCM halafu ndani ya CHADEMA waachie uozo.
Dk. Slaa alitolea mfano uamuzi ya Kamati Kuu iliyoamua kuwafukuza madiwani watano wa jijini Arusha na hata uamuzi wa mahakama ulipotoka ilionekana kuwa chama kilisimamia haki.
Alisema kuwa ni vizuri kuwa na watendaji wachache wanaozingatia maadili.
“Hata Mwalimu Nyerere aliwahi kuwafukuza wabunge sita wa CCM walioshindwa kuzingatia maadili, lakini kwa sasa wameamua kulindana ndiyo maana wanashindwa kuwachukulia hatua mafisadi wa Meremeta, walioweka fedha zetu Uswisi, Fedha za Richmond, EPA na hata zile za rada,” alisema.
Alisema kuwa ni lazima Watanzania wadai fedha zao ambazo wanaamini zinawafaidisha watu wachache tu.
0 comments:
Post a Comment