Bondia Nassibu Ramadhani kushoto akitunishiana misuri na bondia Francis Miyayusho wakati wa utambulisho wa mpambano wao utakaofanyika 9 Desemba katika ukumbi wa PTA Sabasaba Dar es salaam.
Promota wa mpambano wa Ubingwa wa WBF Mohamed Bawaziri Katikati akiwa na mkanda wa ubingwa watakaogombania mabondia Nassibu Ramadhani kushoto na Francis Miyayusho wakati wa utambulisho wa mpambano huo utakaofanyika katika ukumbi wa PTA Sabasaba tarehe 9 Desemba. Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com.
Wakati mabondia Francis Miyeyusho na Nassib Ramadhani wakitarajiwa kupima uzito Desemba 8 kabla ya kuvaana kuwania ubingwa wa Mabara wa WBF, viongozi waalikwa watakaoshuhudia pambano hilo wamefahamika.
 Promota wa pambano hilo litakalofanyika jijini Dar siku ya Desemba 9, Mohammed Bawazir amesema, miongoni mwa viongozi hao waalikwa ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo. Mgeni rasmi ni Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara
 Bawazir amesema, wengine waliothibitisha kushuhudia pambano hilo la uzani wa Bantam ni pamoja na Meya wa Manispaa ya Kinondoni Yusuf Mwenda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova na Katibu wa Itikidi na Uenezi-CCM Nape Nnauye.
Juu ya maandalizi ya pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kutokana na ubora na rekodi za mabondia hao wawili, Bawazir amesema yanaendelea vema japo wamekwama kupata wadhamini wa kuwapiga tafu.
Bawazir alisema pamoja na hayo bado wanaendelea kutoa wito kwa watu wenye mapenzi mema na mchezo wa ngumi kujitokeza kuwapa nguvu, huku akisema upimaji wa uzito na afya kwa mabondia utafanyika Desemba 8 katika uwanja wa Karume
 Pambano hilo litafanyika chini ya usimamizi wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania, PST na litatanguliwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
 Michezo hiyo ya utangulizi ni kati ya Fadhili Majia vs Juma Fundi, Mohammed Matumla dhidi ya Doi Miyeyusho, Ibrahimu Class ‘King Class Mawe’ vs Said Mundi, Fred Sayuni dhidi ya Deo Samwel na Hassan Kidebe dhidi ya Baina Mazola.