Timu ya taifa ya soka ya  Ertrea iliyokuwa imetoweka nchini Uganda imeibuka na kuomba ukimizi wa kisiasa nchini humo.
Waziri anayeshughulikia Wakimbizi nchini Uganda Musa Ecweru amesema timu hiyo yenye watu 18 imewaambia kuwa nchi yao sio salama kwa maisha yao pindi watakaporejea huko na kuomba kupewa ukimbizi wa kisiasa.
Ameongeza kuwa kwa sasa wako mikononi mwa serikali ya Uganda na Umoja wa Mataifa na kuwa wamepatiwa ulinzi.
Kwa mujibu wa CECAFA polisi nchini Uganda walitaarifiwa baada ya wachezaji wa timu hiyo kutoonekana baada ya mechi yao na Burundi ambayo walifungwa 2-0 katika michuano ya kombe la klabu bingwa kanda ya Afrika Mashariki na Kati Cecafa inayoendelea.
Mwaka 2007 wachezaji 6 wa timu ya taifa ya soka ya Eritrea waliomba ukimzi wa kisiasa nchini Angola baada ya mchezo wao, huku mwaka 2009 wachezaji 12 wa timu ya taifa ya soka ya Eritrea nao waliomba ukimbizi baada ya kumaliza mechi nchini Kenya.
Mwaka jana wachezaji 13 wa klabu ya soka ya Red Sea ya Eritrea waliomba ukimbizi nchini Tanzania.