Mwendesha mashtaka mkuu mpya wa ICC. Fatou
Bensouda
MAHAKAMA ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) yenye makao yake makuu, The Hague, Uholanzi inatafakari uwezekano wa kuiingiza Tanzania katika orodha ya nchi zinazopaswa kuchunguzwa kutokana na makosa ya uhalifu wa kijinai, Mtanzania limebaini.
ICC ambayo bado haijafikia uamuzi wowote kuhusu hatima ya Tanzania, imeeleza msimamo wake huo katika barua yake ya Novemba 27 mwaka huu iliyoituma kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Taasisi hiyo huru ya kimataifa ambayo tayari imeibua mizozo ya kisheria na kisiasa katika mataifa kadhaa ya Kiafrika imeandika barua hiyo ikijibu barua ambayo ilitumwa kwao na LHRC miezi miwili iliyopita.
LHRC ilituma barua ICC Oktoba mwaka huu, ikilalamikia kile ilichokieleza kuwa ni kukithiri kwa matukio ya raia kuuawa na baadhi ya maofisa za taasisi za dola, wakiwamo askari polisi katika kipindi cha kati ya mwaka 2004 na sasa.
Kwa mujibu wa barua hiyo, iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uchunguzi cha Mpelelezi Mkuu wa ICC, M.P. Dillon ambayo MTANZANIA imeiona, uamuzi wa ama kuiingiza Tanzania katika uchunguzi huo wa makosa ya uhalifu wa kijinai au la utafikiwa iwapo mambo kadhaa yatatekelezwa.
Dillon katika barua hiyo anayataja mambo ambayo yanaweza yakasababisha uchunguzi huo kuanza kuwa ni pamoja na iwapo itathibitika kwamba makosa yanayopaswa kufuatiliwa yanaangukia katika kifungu cha 53 cha Mkataba wa Rome, uliosababisha kuundwa kwa ICC yenyewe.
Barua hiyo pia, inayataja masuala mengine katika orodha hiyo kuwa ni pamoja na uzito wa makosa yenyewe na iwapo taasisi za dola zinachunguza na kuchukua hatua zozote za kimashitaka dhidi ya watu wanaohusishwa na makosa husika.
“ICC inatafakari hali ya mambo kutokana na barua mliyoituma kwa kutumia barua na taarifa nyingine zilizopo. Chini ya kifungu cha 53 cha Mkataba wa Rome, Mwendesha Mashitaka (wa ICC) anapaswa kuangalia iwapo kuna sababu za msingi za kuamini kuwa makosa yaliyofanywa yanaangukia katika wigo wa mamlaka ya mahakama hii,” anasema Dillon katika barua yake hiyo.
Ingawa katika barua yake hiyo, Dillon anasema taasisi yake hiyo itachukua hatua ya kuyatafakari masuala hayo kwa haraka, anatahadharisha kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwa kazi hiyo kuchukua muda mrefu kabla ya kukamilika.
Hatua hiyo ya ICC inakuja wakati tayari uchunguzi wa namna hiyo umepata kuleta mitikisiko mikubwa katika katika mataifa mengine ya Kiafrika kama Kenya, Liberia na Ivory Coast.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Hellen Kijo Bisimba alieleza kuridhishwa na hatua hiyo ya ICC.
“Tunashukuru kuona barua yetu imepokelewa, tumeahidiwa kwamba kazi ya kuanza mchakato huu itaanza, baada ya kupitia madai yetu tulioainisha.
“Kama mnakumbuka kumekuwapo na matukio mengi ambayo raia wanauawa na vyombo vya dola kama vile jeshi la polisi, lakini kila tunapopiga kelele hatuoni kama Serikali inachukua hatua, zaidi ya kukaa kimya.
“Tunasubiri wapitie kwa kina madai yetu, tunataka kuona hatua zinachukuliwa ipasavyo, tunasikitika mno kuona hakuna utawala wa sheria,” alisema.
Akizungumzia tukio la kuuawa kwa polisi wawili katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Bisimba alisema kituo hicho kinalaani vikali tukio hilo.
“Tulipokea kwa mshtuko taarifa za kuuawa askari Koplo Paschal na Private Alex, hatupendi kuona wananchi wanajichukulia sheria mkononi.
“Tunapenda kuikumbusha jami na serikali kuwa, hali hii ni ya hatari kubwa kwa jamii na taifa kwa ujuimla, kwa sababu matendo haya ni doa kubwa katika dhana ya polisi jamii iliyoasisiwa na IGP Saidi Mwema.
“Hivyo tunatoa pole kwa jeshi la polisi, lakini tunaitaka serikali ichukue hatua kali dhidi ya wale wote waliohusika katika tukio hilo la kinyama na matukio mengine ya aina hii,” alisema.
Alisema mauaji ya raia wasiokuwa na hatia yamekuwa yakiongezeka, kwani mpaka sasa watu karibu 200 wameuawa.
“Takwimu zinaonyesha, mwaka 2004 watu wanne waliuawa, mwaka 2005 watu 36, mwaka 2006 watu 37, mwaka 2008 watu 14, mwaka 2008 watu watano, mwaka 2009 watu 17, mwaka 2010 watu 52 na mwaka 2011 watu 28.
“Watu hawa, wameuawa katika matukio mbalimbali kama vile kupigwa risasi migodini, kushambuliwa na askari wakidhaniwa ni mtuhumiwa wa ujambazi,
“Haya yote ni mauaji yanayotokana na ukosefu wa uadilifu ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na sababu kuu mbili, kwanza ni kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani jeshi la polisi lenyewe, mahakama na vyombo vingine, nawananchi kukosa imani na vyombo hivyo na kuamua kujichukulia sheria mkononi.
0 comments:
Post a Comment