*Yaondoka na Sh milioni 150, moja latiwa mbaroni.
MOJA YA AINA YA BUNDUKI.
Mtu anaedaiwa Kuhusika katika tukio la Ujambazi lililotokea Maeneo ya Kariakoo Jijini Dar es Salaam jana akiwa chini ya Ulinzi baada ya kukamatwa. Watu wawili waliuwawa jana na majambazi wakati wakipora fedha.
WATU wanaosadikiwa kuwa majambazi, wamewaua watu wawili, akiwemo mhasibu wa Kampuni ya Artan Ltd na kufanikiwa kupora Sh milioni 150, zilizokuwa zikipelekwa benki.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea mjini Dar es Salaam jana saa 4 asubuhi, katika eneo la Kariakoo.
Majambazi hao, waliwavamia watumishi wa kampuni hiyo ambao walikuwa ndani ya gari na fedha hizo, tayari kwa ajili ya kuzipeleka benki.
Watu waliouawa ni Ahamed Issa (55) ambaye ni mhasibu wa kampuni hiyo na Sadick Juma (38), msukuma mkokoteni.
Mbali ya hao, watu watatu walijeruhiwa vibaya kwa risasi zilizokuwa zikirushwa kati ya Jeshi la Polisi na majambazi hao.
Waliojeruhiwa kwa risasi katika mapambano hayo, ni Alhaji Mussa, ambaye ni msukuma mkokoteni katika eneo la Kariakoo, Salimu Athmani na mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Yusuph.
Kutokana na mapambano haya, majeruhi hao walikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema katika tukio hilo, polisi walifanikiwa kumtia mbaroni jambazi mmoja, Augostino Kayula (24).
Alisema kukamatwa kwa Kayula, kulitokana na uchunguzi uliofanywa na Polisi, ambapo baada ya kumkamata walimkuta akiwa na bastola iliyokuwa na risasi moja.
Alisema katika tukio hilo, majambazi wawili walifanikiwa kutoroka na fedha hizo, huku wakiiacha pikipiki yenye namba za usajili T 301 CCW, waliyokuwa wakiitumia.
Alisema katika tukio hilo, mlinzi wa kampuni hiyo, Ally Said (42) anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.
“Baada ya kuwajeruhi watu hawa, walipora fedha na kuondoka, lakini wananchi pamoja na askari wa doria walisikia milio ya risasi na walifika haraka na kuanza kuwasaka na kufanikiwa kumkamata jambazi mmoja.
“Ninapenda kutoa tahadhari kwa watu wenye nia ya kufanya uhalifu katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, wajue Jeshi letu tumejipanga kukabiliana nao.
“Hata hawa majambazi waliofanya tukio hili, tutahakikisha tunawatafuta usiku na mchana ili kuweza kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Wananchi na wafanyabiashara wasisafirishe fedha nyingi bila msaada wa ulinzi wa polisi, ni muhimu kwa madereva, hasa wa Dar es Salaam wahakikishe wanafunga vioo vya magari yao ili kuepuka adha ya watu mbao si wema kwao,” alisema Kova.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni linawashikilia watu watatu kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali, yakiwamo meno ya tembo matano.
Watuhumiwa hao, ni Lazaro Ndahani (32), Polias Ngahaki (24) na Neema Joseph (18), wote wakazi wa Kimara Suka.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi nyumbani kwa Lazaro Ndahaki, baada ya raia wema kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Mbali na tukio hilo, pia jeshi hilo limefanikiwa kuwatia mbaroni watu wanne kwa kosa la kujihusisha na wizi wa gari, ambao ni Kassim Juma (27), Martin Joseph (23), Queenida Salim (18) na Fatuma Khamis (19).
0 comments:
Post a Comment