MBABE wa kivita Ngudjolo Chui, alikuwa akituhumiwa kuhusika na mauaji,
ukatili na ubakaji katika eneo la Ituri mashariki ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo, muongo mmoja uliopita.
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu wa
kivita, ICC, yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi,
imemuondolea mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya
ubinaadamu mbabe wa kivita wa Kongo, Ngudjolo Chui.
Uamuzi huo ni wa pili katika historia ya mahakama hiyo ya uhalifu na ni
uamuzi wa kwanza wa kufutiwa mashtaka mtuhumiwa, hatua ambayo inaonekana
kama ni pigo kwa waendesha mashtaka wa ICC ambao kwa mujibu wa majaji
wameshindwa kutoa ushahidi wa kumuhusisha Ngudjolo moja kwa moja na
mauaji ya Kaskazini Mashariki ya Kongo yaliyotokea mwaka 2003.
Aidha
uamuzi uliotolewa leo Jumanne pia unazusha mashaka kuhusu
kesi dhidi ya mtuhumiwa mwengine wa mauaji hayo mbabe wa kivita, Germain
Katanga, anayeshtakiwa kwa makosa kama yaliyokuwa yakimkabili Chui.
Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou Bensouda.
Ushahidi mzito wakosekana
Mwezi uliopita majaji waliahirisha kesi ya Katanga katika hatua ambayo
baadhi ya wasomi wanasema huenda ikarahisisha kumtia hatiani.
Mapigano
ya Kaskazini mashariki mwa mkoa wa Ituri yalikuwa ni mapigano ya
kikabila yaliyochochewa na suala la ardhi na mali, mojawapo ya chanzo
cha mizozo iliyozuka katika nchi nzima ya Kongo katika mwaka 1998 hadi
2003 na iliyozihusisha nchi jirani.
Halikadhalika mapigano ya Ituri
yanamuhusisha pia Bosco Ntaganda ambaye anatakiwa na mahakama hiyo ya
ICC kwa kutuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita katika mzozo huo.
Waendesha mashtaka wanasema Ngudjolo Chui alitoa amri kwa wapiganaji
kuzifunga barabara za kuingia na kutoka kijiji cha Bogoro mnamo mwezi wa
Februari mwaka 2003 kwa lengo la kufanyika mauaji ya raia waliokuwa
wakijaribu kukimbia.
Inadaiwa wanawake na watoto walichomwa wakiwa hai
ndani ya nyumba zao na kusababisha vifo vya watu 200 wakati na baada ya
mashambulizi dhidi ya kijiji hicho wakati wapiganaji wa kabila la
Walendu na Ngiti walipodaiwa kuziteketeza nyumba za wakaazi wa kijiji
hicho ambao wengi walikuwa ni kutoka kabila la Wahema.
Rufaa itafanikiwa?.
Jean Bosco Ntaganda kiongozi wa M23 ahusishwae na vita vya Ituri.
Wakili wa mahakama, Nick Kaufmann, amesema tukio hilo lilikuwa fupi
na la kusikitisha lakini upande wa waendesha mashtaka umeshindwa
kuchunguza ipasavyo mamlaka ya uongozi na utoaji amri kuhusiana na
shambulizi hilo la kijiji cha Bogoro.
Mashahidi waliosimama dhidi ya
Ngudjolo hawakutoa ushihidi wa kutosha kuwashawishi majaji.
Fatou
Bensouda ambaye ni mwendesha mashataka mkuu mpya wa ICC tangu mwanzoni
mwa mwaka huu, hata hivyo amewaomba majaji kumuweka kizuizini Ngudjolo
hadi pale itakapokatwa rufaa.
Pamoja na hilo lakini wataalamu wa kisheria wanasema itakuwa vigumu
kuubatilisha uamuzi wa mahakama kwa sababu hakuna ushahidi mpya
utakaoweza kutolewa wakati wa kusikilizwa rufaa.
Watetezi wa haki za
binadamu kama vile Shirika la Human Rights Watch kwa hivyo wanahisi
uamuzi wa majaji wa ICC wa kumuondolea mashtaka Ngudjolo unawaacha
wahanga wa Bugoro na wa maeneo mengine ambako vikosi vyake vilifanya
mauaji, kutotendewa haki.
Makaburi ya pamoja Ituri.
Mkurugenzi wa shirika hilo anayehusika na masuala ya sheria za
Kimataifa, Geraldine Mattioli-Zeltner, ametoa mwito kwa waendesha
mashataka wa ICC kuimarisha uchunguzi wake kuhusiana na wahusika wa
mauaji ya Ituri ikiwa ni pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa Kongo,
Rwanda na Uganda.
0 comments:
Post a Comment