BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAKAMU MWENYEKITI CCM AZUSHIWA JAMBO NA ALIYEKUWA MBUNGE WA NJOMBE MAGHARIBI CCM.


KWA UFUPI
Alisema siku ya uchaguzi akiwa amekaa meza kuu, Mangula alipopewa nafasi ya kuhutubia, aliwaambia wajumbe kuhakikisha Kevela na mgombea mwingine Hamisi Nurdin hawapiti.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Philip Mangula.

ALIYEKUWA Mbunge wa Njombe Magharibi (CCM), Yono Kevela amemtuhumu Makamu Mwenyekiti wa CCM Philip Mangula kwa kuvuruga uchaguzi wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho, Wilaya ya Wanging’ombe kwa kuwabeba baadhi ya wagombea.

Katika madai yake ambayo ameyakatia rufani, Kevela amesema katika uchaguzi huo uliofanyika Julai 29 mwaka huu, mbali na kuwabeba wagombea hao, Mangula alishiriki kutengeneza makundi ya vitisho, rushwa na lugha za kejeli dhidi yake.
Alisema siku ya uchaguzi akiwa amekaa meza kuu, Mangula alipopewa nafasi ya kuhutubia, aliwaambia wajumbe kuhakikisha Kevela na mgombea mwingine Hamisi Nurdin hawapiti.
“Mangula alisema watu hao wasichaguliwe kwa kuwa wana malengo tofauti na yale ya kukitumikia chama,” alidai Kevela. 
Malengo yaliyodaiwa katika rufani hiyo ni kuwa Kevela anautaka ubunge wa Njombe Magharibi na Nurdin ana nia ya kutaka Makao Makuu ya Wilaya ya Wanging’ombe yawe Igwachanya.
Rufani hiyo imetaja tuhuma nyingine dhidi ya Mangula kuwa ni timu yake kutangaza kuwa Kevela amejitoa kwenye uchaguzi… “Hili liliathiri pia ushindi wangu katika uchaguzi huo.”

Rufani hiyo ya Kevela  nakala yake imepelekwa kwa Katibu Mkuu na Mwenyekiti wa CCM, Idara ya Usalama na Maadili ya CCM, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho na Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe.
Kevela katika rufaa yake hiyo, anataka matokeo ya uchaguzi huo yafutwe kwa kuwa ulikiuka vifungu kadhaa vya kanuni kikiwamo cha Miiko ya Shughuli za Uchaguzi na Uteuzi wa wagombea ukurasa wa 39, cha Kanuni za Uteuzi toleo la Februari 2010, Kifungu namba 22 (1-6). 
Hata hivyo, pamoja na kukata rufani hiyo, Kevela amesema ana shaka kwamba haki itatendeka kwani, mtu anayemlalamikia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, ambayo kulingana na Kanuni za Uchaguzi za CCM, ndiyo itakayopitia malalamiko hayo na kuyatolea uamuzi.

Kamati hiyo inatakiwa iwe imekamilisha kazi yake ndani ya miezi sita na Mangula alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo dhidi yake alisema hazijamfikia na wala hazijui.
“Hayo hayajanifikia na siyajui. Hata hiyo rufaa haiji kwangu. Malalamiko yote yanashughulikiwa na jopo la wataalamu kabla ya kufikishwa kwetu. 
Hivi sasa malalamiko yote yako katika hatua ya uchambuzi na kimsingi yatakayoshughulikiwa ni yale yanayohusu rushwa pekee.”
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo alisema asingeweza kufanya hivyo kwa kuwa alikuwa na siku chache tangu alipoanza kazi hiyo na kutaka aulizwe Katibu wake wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Alipoulizwa, Nape alimtaka mrufani kutokuwa na wasiwasi juu ya kutendewa haki akisema kwa kawaida rufani hazisikilizwi na mtu mmoja.
Alisema baada ya kuchambuliwa, rufani zote zinafikishwa katika kikao cha sekretarieti ambayo huzipitia na kuzipeleka katika Kamati ya Usalama na Maadili kisha Kamati Kuu na yapo ambayo huishia katika ngazi hiyo na mengine kupelekwa hadi Halmashauri Kuu kwa hatua zaidi.
Nape alisisitiza kuwa hakuna uamuzi utakaofanywa na mtu mmoja … “Labda aseme (Kevela), kuwa hana imani na Kamati Kuu ya chama chake na hapo ndipo labda tutaangalia kanuni zinasemaje lakini kwa sasa hali halisi ndiyo hiyo,” alisema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: