VYAMA vya upinzani nchini vikiongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vimetakiwa kubadilika kwa vile mfumo wa vyama hivyo kwa sasa ndiyo unavikwamisha kuchukua madaraka ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambaye ni mtaalamu wa masuala ya siasa, Dk. Benson Bana alipozungumza na MTANZANIA Jumapili jana kuhusiana kuhusu maadhimisho ya miaka 51 ya uhuru wa Tanganyika leo.
Dk. Bana alisema ingawa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza mvuto kwa wananchi lakini vyama vya upinzani navyo havina budi kubadilika.
Alisema hadi sasa vyama vya upinzani nchini vimekuwa vyama vya uharatakati zaidi na vimekuwa vikishikilia sera moja ambayo haitavisaidia kuingia Ikulu.
“Kwa upande wa siasa bado hatujapiga hatua kwa sababu naona kuna utitiri tu wa vyama ambavyo bado havijaweza kufanya siasa zao sawasawa.
“Vyama hivyo vikiongozwa na CHADEMA vimekuwa vikizungumzia jambo moja tu la ufisadi na kuacha mambo mengine ya msingi...Chadema wajue kwamba ufisadi peke yake hautawafikisha Ikulu, ni lazima waweke kibwagizo kingine.
“Kibwagizo hiki kwa sasa kimetosha lazima waje na kingine... hebu wazungumzie mambo muhimu kwa maisha ya mtanzania wa kawaida, waje na sera ya maji, elimu, afya na mambo mengine lakini kama hawana kibwagizo kingine basi wakae kimya kwa sababu hili la ufisadi peke yake sidhani kama litawafikisha Ikulu,” alisema Profesa Bana.
Akiizungumzia CCM Dk. Bana alisema: “Kwa sasa hiki chama kimepoteza mvuto kwa wananchi... hiki ndicho chama kikongwe ambacho kilipaswa kije na sera nzuri kwa manufaa ya watanzania.
“Lakini hivi sasa kimekuwa chama cha kukumbatia rushwa na makundi, CCM kilikuwa chama kizuri lakini kimepoteza mwelekeo na kimeshindwa kujipanga vizuri,” alisema.
Kuhusu mafanikio na changamoto katika miaka 51 ya uhuru alisema hadi sasa watanzania hawawezi kusema wamepoteza sana.
“Tunacho kitu cha kujivunia kwa sababu yapo maeneo tumefanya vizuri na mengine tumefanya vibaya, maeneo tuliyofanya vizuri ni pamoja na kuulinda uhuru wetu.
Nchi nyingi ambazo tulipata nazo uhuru zimepoteza uhuru wao ama kwa kunyang’anywa au kwa kupinduliwa, Tanzania tumeingia katika uhuru tukiwa na makabila 125 lakini hadi leo tunasikilizana, hii ni tunu ambayo hatuwezi kuibeza.
“Ukiangalia uchumi wetu haujakua sana lakini huwezi kuufananisha na wakati tunapata uhuru...changamoto zipo kwani katika suala la elimu, afya, miundombinu serikali imeweza tu kupanua hizo huduma lakini hazijakidhi mahitaji ya watanzania.
“ Ukiangalia katika suala la kumiliki ardhi pia nalo ni tatizo kwa sababu watanzania wachache ndiyo wameweza kumiliki ardhi.
“Lakini changamoto nyingine kubwa ni suala la ubinafsishaji lilivyotekelezwa... hadi sasa ukiwauliza mmepata shilingi ngapi katika uwekezaji na viwanda vingapi vimejengwa, huwezi kupata majibu.
“ Lakini pia watanzania wamekuwa ni watu wa kupiga kelele tu lakini si watu wa kufanya kazi, ukiangalia ofisini watu ni wavivu hawataki kufanya kazi.
“Tabia hii inazidi kukua tumesahau kwamba lengo letu la uhuru lilikuwa kila mtu afanye kazi kwa juhudi na maarifa lakini watu wamekuwa wavivu wanapiga tu kelele ya mafisadi huku hatawaki kufanya kaz. Lazima tubadilike kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi yetu,” alisema Dk. Bana.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema ingawa watanzania wana kitu cha kujivunia katika maadhimisho hayo ya miaka 51 ya uhuru wa Tanganyika lakini changamoto kubwa nia ajira kwa vijana.
“Kujitawala wenyewe ni jambo kubwa na la kujivunia kwa vile kutawaliwa ni jambo la fedheha, lakini zipo changamoto ambazo serikali haiwezi kuzikwepa na kubwa ni katika uchumi takwimu za taifa na mataifa zinaonyesha mtanzania bado ni maskini wa kutupwa.
“Lakini pia bado kuna tatizo kubwa katika suala la ajira kwa vijana, hili ni bomu linalosubiri kupasuka.
“Ukiangalia jiografia ya nchi yetu inaruhusu kuwa na ajira za kutosha, tuna bandari na vitu vingi, tunatakiwa kuongeza uzalishaji kwa kujenga viwanda vya nguo, viatu, vifaa vya umeme.
“Hivi vyote vinawezekana kwa sababu tuna umeme wa kutosha lakini tatizo kubwa ni ufisadi katika sekta hii,” alisema Profesa Lipumba.
0 comments:
Post a Comment